By Kalunde Jamal, Mwananchi
kjamal@mwananchi.co.tz
Dar es
Salaam. Wanasheria wamekosoa utaratibu unaotumiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda kuwatangaza watu anaowatuhumu kuhusika na uuzaji, utumiaji
wa dawa za kulevya au anaodhani wana taarifa muhimu zinazoweza kusaidia Jeshi
la Polisi kuwakamata.
Tangu
mapema wiki hii, Makonda amekuwa akitangaza majina ya watu hao, wakiwemo
wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa na wadogo na wasanii, akiwataka wakutane
naye Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam kwa mahojiano.
Pamoja na
kujitetea kuwa ana mamlaka hayo na kwamba asiye na hatia atakuwa amesafishwa
baada ya mahojiano na polisi, wanasheria wanaona mteule huyo wa Rais anakiuka
taratibu.
“Kinachofanyika
sasa kwa kuwataja hadharani watuhumiwa wa dawa za kulevya, kinafanyika kisiasa
ndiyo maana hakifuati sheria inayowaruhusu watu maalumu kuita na siyo mkuu wa
mkoa,” alisema Dk Onesmo Kyauke, mhadhiri mwandamizi wa sheria wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Alisema
polisi, hakimu, mtu wa kawaida wanaweza kumkamata mtuhumiwa bila kuwa na hati
ya kukamata iwapo mtuhumiwa amefanya kosa mbele yao.
“Kuna
(mkuu wa upelelezi wa wilaya) DCI, (wa mkoa) RCO, kikosi maalumu cha dawa za
kulevya, hao ndiyo wana wajibu wa kufanya hivyo kwa sababu ni wataalamu na
wamebobea katika kupeleleza, kuagiza watuhumiwa wajisalimishe na hata
kukamata,” alisema Dk Kyauke.
Alisema
pamoja na ukweli kwamba mkuu wa mkoa ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na
usalama, kisheria hatambuliki na suala hilo linasababisha ukakasi, kitu ambacho
kinaweza kufanya hata walioitwa kukakataa wito kwa kuwa hakuna sheria
inayowabana.
“Kwa jinsi
hii shughuli inavyoendeshwa bila kufuata sheria wala kujali madhara ya kisheria
yatakayotokea ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kesi, inaharibu nia njema ya
kukomesha maharamia wa dawa za kulevya,” alisema Dk Kyauke.
“Badala
yake (kazi hii) inakuwa kichekesho. Ukitazama, kuna watu wameitwa jina moja
moja, wasipokuja hawatalaumiwa kwa sababu wenye majina hayo wapo wengi kila
mmoja akikana, hakuna atakayekuwa na jibu.
“Ikiendeshwa
kwa kufuata sheria na taratibu ni jambo jema ambalo lilikuwa linasubiriwa na
Watanzania wengi tena wenye mapenzi mema na nchi na mustakabali wa vijana.”
Maoni kama
hayo alikuwa nayo mwanasheria wa jijini Dar es Salaam, Faraja Mangula ambaye
alisema kisheria mamlaka ya kukamata au kuita mtu kituoni ni ya Jeshi la Polisi
na watendaji wa vyombo vingine kulingana na kosa, lakini kuna taratibu zake.
Mangula
alizitaja baadhi ya hatua zinazotakiwa kufuatwa na polisi ili mtu akamatwe kuwa
ni pamoja na kumchunguza na kujiridhisha kuwa mtuhumiwa amefanya au amehusika
na kosa analotuhumiwa.
Aliitaja
hatua ya pili ni kumkamata mtuhumiwa huyo baada ya kujiridhisha na
anayeruhusiwa kufanya hivyo ni polisi. Alisema ya tatu ni kupeleka faili lake
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama upelelezi umekamilika ili lipelekwe
mahakamani. Alisema katika sheria hakuna mahali popote panapomtaja mkuu wa mkoa
wala mtu mwingine yeyote katika kuwaita watu kwa ajili ya mahojiano zaidi ya
Jeshi la Polisi, hivyo mkuu wa mkoa anapofanya hivyo anajishushia hadhi kwa sababu
yeye yupo juu na anachotakiwa kufanya ni kuwaelekeza polisi cha kufanya badala
ya kufanya kazi yao.
“Haki
inayomtambua kisheria moja kwa moja ni ya kumuweka mtu ndani saa 48 na si
kumwita mtuhumiwa polisi kwa ajili ya mahojiano,”alisema Mangula.
Naye wakili
wa kujitegemea Bernard Otieno alisema kuwa kuna mahitaji ya kisheria kabla
ya kumkamata mtuhumiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya
Jinai. Alisema mambo hayo ni ukamataji wa kutumia hati (warrant of arrest) na
ukamataji bila hati (without warrant of arrest).
Alisema
hati hiyo hutolewa na polisi kwa ajili ya kumkamata mtu anayetuhumiwa kwa kosa
la jinai baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa mlalamikaji.
Alitaja
baadhi ya vitu vinavyotakiwa kuwa ndani ya hati hiyo iwe imetolewa na mkuu wa
kituo cha polisi au hakimu, lazima iwe na mhuri wa polisi au mahakama, iwe
imesainiwa, iwe na maelezo ya mtuhumiwa kama jina kamili, kabila, dini na
ieleze mtuhumiwa akikamatwa anafikishwa kwenye vyombo vya kisheria.
“Watu wa
kawaida na hakimu wana haki ya kumkamata mtuhumiwa bila kuwa na hati hiyo iwapo
wamemuona akitenda kosa hilo mbele yao, vinginevyo anayeruhusiwa kufanya hivyo
ni polisi na kwa kufuata utaratibu maalumu,”alisema Itieno.
Akizungumzia
hatua hiyo ya kukomesha watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya, Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu alisema vita hiyo haipo Dar es
Salaam peke yake bali nchi nzima.
Alisema
makamanda wa mikoa wa polisi wanatambua suala hilo na tayari wameanza
kulitekeleza.
Akizungumzia
kitendo cha watuhumiwa kutajwa hadharani, mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alisema ili mtu
asiharibiwe jina lake kwa kosa ambalo hajatenda, angalau kuwe na ushahidi
unaomuhusisha na tuhuma hizo. Alisema kuwataja bila kuwa na ushahidi wa
kujiridhisha walau kidogo, baadaye ikathibitika hawakuwa na hatia wala ushahidi
kuonyesha kama wanahusika, taswira yake na utu wake katika jamii utakuwa
umeondoka.
“Kwa mfano inawezekana wafanyabiashara, viongozi wa siasa na wananchi wa
kawaida, walikuwa wanaheshimika na jamii zao, wanatajwa hadharani na inabainika
hawakuwa na kosa, zilikuwa tuhuma tu, nani atawasafisha? Ina maana itakuwa
ndiyo basi utu wao umeingia dosari, ”alisema Dk Bisimba
0 comments:
Post a Comment