By Fredrick Nwaka, Mwananchi
fnwaka@mwananchi.co.tz
Dar es
Salaam. Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amesema
mshikamano wa wabunge ulioweka pembeni tofauti za kiitikadi unaonyesha Bunge
linaweza kurejesha nguvu zake iwapo halitaingiliwa katika utendaji.
Mchungaji
huyo wa Kanisa la Vineyard amesema hata uamuzi wa Rais John Magufuli kumteua
Rogers Sianga kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za
Kulevya umedhihirisha nguvu hiyo ya Bunge.
Msigwa
alikuwa akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu jijini Dar es Salaam
wiki iliyopita.
Mbunge
huyo wa Iringa Mjini alisema Rais Magufuli alifanyia kazi hoja za wabunge baada
ya kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutangaza majina ya
watu akiwahusisha na dawa za kulevya, kulalamikiwa na wabunge.
Makonda
alitangaza majina ya wasanii, wanasiasa, wafanyabiashara na viongozi wa dini
akiwataka kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam kwa ajili ya
mahojiano kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya, jambo lililopingwa na
watu wengi, na hasa wabunge.
Wakizungumza
katika mkutano uliopita, wabunge walisema wanaunga mkono vita hiyo, lakini
hawakubaliani na kitendo cha kutangaza watuhumiwa na wengine wakasema chombo
kinachostahili kuendesha vita hiyo ni mamlaka ambayo tangu iundwe kisheria
haikuwa imepata watendaji wake.
Siku
chache baadaye, Rais Magufuli alimteua Sianga na watendaji wengine, ambao mara
moja wakaanza utekelezaji wa majukumu yao.
Uteuzi huo
umemfanya Msigwa kuamini kuwa Bunge linaweza kuwa na sauti moja lisipoingiliwa
kiutendaji.
“Hakuna
asiyeunga mkono vita hii lakini approach (mbinu) ya Makonda haikuwa na mamlaka
kisheria na ndiyo maana Rais ametusikiliza (wabunge) na kumteua mtu
atakayesimamia jambo hilo kisheria,” alisema Mchungaji Msigwa.
“Vita hii
inatuhitaji wote; kuanzia kamishna, vyombo vingine vya usalama, viongozi na
wananchi wote na si kwa kuitana kwa kutumia redio na televisheni, huko
hatutafika zaidi ya kuishia kudhalilishana na kuchafuana,” alisema mbunge huyo
machachari.
Aidha,
Msigwa ambaye aliingia bungeni kwa mara ya kwanza 2010, alifananisha hatua ya
Makonda na baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa nchini kujitwisha mamlaka ya
kuwaweka mbaroni wananchi na waandishi wa habari, akisema wengi wanaendeleza
chuki baada ya kuangushwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM.
“Wengi wao
ni wale walioshindwa kwenye kura za maoni ndiyo wanawaharibia sifa wabunge
waliochaguliwa majimboni,” alisema
Chaguzi
ndani ya Chadema
Mchungaji
Msigwa pia alizungumzia chaguzi za ndani ya Chadema kwa ajili ya kusimika
viongozi wa kanda, ukiwamo wa Desemba mwaka jana uliompa mbunge huyo uenyekiti
wa Kanda ya Nyasa inayojumuisha mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa na Songwe.
Uchaguzi
huo nusura uingie dosari baada ya kamati kuu kuondoa jina la Makamu Mwenyekiti
wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosospi.
“Uchaguzi ulikuwa
na kashikashi kwa kuwa kuna watu wako nje ya Chadema na hawakutaka
nichaguliwe,” alisema Msigwa akidai kuwa hoja ya waliokuwa wakitaka asigombee
ni kutokana na kuwa mbunge.
“Mbona
(John) Heche ni mbunge na Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti? (Cecil) Mwambe ni
mbunge na Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini na (Kasuku) Bilago ni mbunge na
Mwenyekiti wa Kanda ya Magharibi?.
“Katiba
yetu iko wazi, Kamati Kuu ndiyo yenye mamlaka ya mwisho ya kuteua wagombea.
Hata kwenye uchaguzi mkuu kuna wagombea walishinda katika kura za maoni, lakini
Kamati Kuu iliwaengua.”
Msigwa
alidai kuwa kuna watu hawakutaka awe mwenyekiti ili wakimalize chama Kanda ya
Nyasa, lakini akasema “wana bahati mbaya”.
Msigwa
alisema kuchaguliwa kwake kuongoza Kanda ya Nyasa kunalenga kuhakikisha Chadema
inavuna ushindi mnono katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.
“Tumedhamiria
kuhakikisha Kanda ya Nyasa inashinda kata na majimbo mengi kuliko kanda yoyote
ili kurahisha ushindi wa kiti cha urais. Hizi ni salamu kwa wote wenye nia
mbaya na chama hiki,” alisema.
Utawala wa
Awamu ya Tano
Kuhusu
utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli, mbunge huyo
alisema umewafanya watu kuwa na hofu, huku akidai kuwa mkuu huyo wa nchi
haiamini CCM.
Msigwa
alisema Serikali ya Awamu ya Tano haikubali kukosolewa.
“Mwalimu
Nyerere hakujenga majengo, lakini fikra zake zinadumu mioyoni mwa watu. Utawala
huu ni wa watu waoga,” alisema Msigwa. “Haujiamini na hauko tayari kukosolewa.
Wamevuruga Bunge kwelikweli.”
Alikuwa
akizungumzia uamuzi wa Serikali wa kutoruhusu baadhi ya shughuli za Bunge
kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni, kupiga marufuku mikutano ya
hadhara ya kisiasa na kukamatwa mara kwa mara kwa viongozi wa upinzani.
Pia
alisema Rais Magufuli haiamini CCM na ndiyo maana amefanya mabadiliko ya katiba
ya chama hicho yaliyopunguza idadi ya wajumbe wa vikao vikuu na kuondoa baadhi
ya nafasi za utendaji.
“Rais
Magufuli haamini CCM inapigania nini na inataka nini,” alisema.
“Anafanya
vitu vinavyotofautiana na Chama cha Mapinduzi. Watendaji wa chama
hawaheshimiwi. Haya mabadiliko yaliyofanywa yanalalamikiwa na watendaji wa
chini ambao wanatumia muda mwingi kufanya kazi za chama.
“Chama ni
chambo tu, Magufuli anaamini kuna vyombo vilivyojificha chini ya CCM kuwa
ndivyo vinaendesha nchi.”
Hata
hivyo, Mabadiliko anayozungumzia Msigwa, yalipendekezwa na Kamati Kuu ya CCM na
baadaye kupitishwa na kikao cha Halmashauri Kuu kilichofanyika Desemba 13, 2016
na sasa yanasubiri baraka za Mkutano Mkuu.
Miongoni
mwa mabadiliko hayo ni kupunguza wajumbe wa Halmashauri Kuu kutoka 388 hadi
158, na wajumbe wa Kamati Kuu kutoka 34 hadi 24.
Utumishi
kwa wananchi wa Iringa Mjini
Akizungumzia
kipindi chake cha kuwatumikia wananchi wa Iringa Mjini, Mchungaji Msigwa
alisema kazi yake ni kuhakikisha anakuwa daraja bora kati yao na Serikali.
“Ninajivunia
wananchi wangu wa Iringa. Kazi kubwa tunayofanya ni kuhamasisha wananchi
kutambua wajibu na haki zao. Nimelia nao na nimecheka nao katika vipindi vyote.
Nimekamatwa na kuwekwa ndani lakini sijaacha kuwatumikia,” alisema Msigwa.
Alisema
hivi sasa huduma ya majisafi na salama inapatikana kwa zaidi ya asilimia 90 ya
wananchi wa jimbo lake.
“Tumegusa
maeneo yote, huduma za afya na elimu pia zimeimarika kwa ushirikiano wa
viongozi na wananchi. Bado kuna muda mrefu kutekeleza mambo mengine,” alisema
Msigwa.
0 comments:
Post a Comment