By Bakari Kiango, Mwananchi
bkiango@mwananchi.co.tz
Dar es
Salaam. Wakati Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe akikumbwa na misukosuko
baada ya kukamatwa na polisi wiki hii, kuliibuka jambo jingine jipya.
Miss
Tanzania 2006 na msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu alibadili upepo wa siasa
nchini kwa kutangaza kuihama CCM na kuhamia Chadema jambo ambalo limejadiliwa
na wasomi na wachambuzi wa siasa kwa mitazamo tofauti.
Ilianza
kwa mwanasheria wa Chadema, Tundu Lindu kujitokeza mahakamani kumtetea Wema
Sepetu katika kesi ya kudaiwa kukutwa na bangi. Lilionekana ni jambo la
kawaida.
Lakini,
kitendo cha Wema kumsindikiza Mbowe mahakamani kikashtua wengi.
Na hata
alipotangaza kuhamia chama hicho cha upinzani pamoja na mama yake, mjadala
ukawa mkubwa zaidi katika vijiwe, sehemu za starehe na mitandao ya kijamii.
Wakati
mijadala hiyo ikiendelea, Wema akiwa na viongozi hao wa Chadema walikuwa
miongoni mwa mashabiki waliojitokeza kushuhudia mechi ya watani wa jadi, wakati
Simba ilipoifunga Yanga mabao 2-1 katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam
jana.
Hali
ilivyokuwa
Mbowe
atakuwa anamaliza mapumziko ya mwishoni mwa wiki, akitafakari msukosuko
uliohusisha kukamatwa na vyombo vya dola na kufikishwa mahakamani, lakini
akijiliwaza baada ya chama chake kupata mwanachama mpya mwenye umaarufu mkubwa
nchini, Wema Sepetu.
Kiongozi
huyo wa Kambi ya Upinzani Bungeni alitakiwa kuripoti kituo kikuu cha polisi cha
Dar es Salaam tangu Februari 10, lakini akakaidi, akisema kuna taratibu za
kuita watu polisi na hivyo kuendelea na shughuli za Bunge mjini Dodoma hadi
lilipomalizika.
Mbowe ni
miongoni mwa watu 65 waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
ambaye aliwataka waripoti kituo hicho cha polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusu
biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Orodha ya
watu hao inahusisha pia wafanyabiashara, wasanii na viongozi wa dini.
Lakini,
kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisisitiza
wito wa Mbowe kuripoti polisi, akisema walijaribu kumtafuta kwa njia ya simu
hakupatikana na wala hawakuweza kumpata nyumbani kwake.
Kamishna
Sirro alitoa saa 48 kwa Mbowe awe ameripoti polisi na asipofanya hivyo,
atatafutwa kwa namna ambayo jeshi hilo litaona inafaa.
Siku moja
kabla ya Mbowe kukamatwa, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliliambia
gazeti hili kuwa ingekuwa ni kumshauri, angemwambia asiripoti polisi hadi
taratibu zitakapofuatwa.
Baada ya
kurudi jijini Dar es Salaam, Mbowe alikamatwa Jumatatu wiki hii na kupelekwa
kituo kikuu cha polisi ambako alihojiwa na pia kupelekwa nyumbani kwake
kupekuliwa na kuachiwa saa 7:00 usiku, kwa mujibu wa mwanasheria wa Chadema,
Tundu Lissu.
Taarifa za
Mbowe kuwa polisi zilikuwa za aina tofauti; viongozi wa Chadema wakisema
mwenyekiti wao alijipeleka kituoni wakati polisi ilisema ilimkamata.
Ofisa
Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema mwenyekiti huyo alikuwa katika gari
akitoka nyumbani kwake Kawe, ndipo alipokutana na gari la polisi na kutakiwa
kusimama.
Baadaye,
Wakili wa mwenyekiti huyo, Frederick Kihwelo aliyekuwa naye siku hiyo, alisema
baada ya kutoka kituoni hapo polisi wapatao 10 walikwenda kufanya upekuzi
nyumbani kwa kiongozi huyo.
Hatua ya
Mbowe kukamatwa ilisababisha Edward Lowassa (waziri mkuu wa zamani na mjumbe wa
kamati kuu wa Chadema), kukatiza mapumziko yake mkoani Arusha na kurejea Dar es
Salaam.
Siku
iliyofuata, Mbowe alilazimika kwenda Mahakama Kuu ambako amefungua kesi dhidi
ya Makonda, Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda ya Maalumu ya Dar es
Salaam(ZCO), Camillius Wambura.
Katika
kesi hiyo, Mbowe anapinga mamlaka yao ya kuamuru kukamatwa kwa wananchi na
kuwekwa mbaroni huku akikitaka chombo hicho cha sheria kutamka Sheria ya Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa inayowapa mamlaka hayo kuwa ni batili kwa kuwa
mazingira yaliyofanya iundwe, hayapo tena.
Mbowe
alifungua kesi hiyo namba 01/2017 baada ya Makonda kumtaka aripoti polisi kwa
mahojiano kuhusu biashara ya dawa za kulevya na matumizi.
Katika
kesi hiyo, Mbowe pia aliiomba Mahakama Kuu itoe amri ya muda ya kuzuia polisi
kumkamata na kumuweka mbaroni hadi shauri kuu litakapotolewa uamuzi.
Hali
ilianza kubadilika Alhamisi wakati Mbowe alipokwenda Mahakamu Kuu kuendelea na
kesi hiyo, akitegemea uamuzi kuhusu maombi yake ya kupewa kinga ya muda. Siku
hiyo, Mbowe alienda mahakamani akisindikizwa na msanii nyota wa filamu, Wema
Sepetu.
Kitendo
cha Wema kumsindikiza kiongozi huyo wa upinzani kilibadili mwelekeo wa suala
hilo, kutokana na macho ya wengi kuelekea kwa mshindi huyo wa taji la Miss
Tanzania la mwaka 2006 ambaye katika kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka juzi
alizunguka kushawishi vijana kuipigia kura CCM.
Siku hiyo,
Serikali iliwasilisha pingamizi dhidi ya ombi la Mbowe la kutaka kinga ya muda
ya kukamatwa na polisi na hivyo Mahakama Kuu kuamua kuwa uamuzi wa suala hilo
utatolewa machi 2.
Picha za
Wema akiwa na Mbowe mahakamani zilisambaa kwa haraka kwenye mitandao ya kijamii.
Wema anaonekana kwenye picha hizo akiwa anatabasamu huku akiwa amenyoosha
vidole viwili na vingine kuvikunja, ikiwa ni ishara ya Chadema, na pembeni yake
akiwepo Mbowe, mbunge wa Bunda Ester Bulaya na mama wa msanii huyo.
Wakati
Mbowe akienda mahakamani, ofisa uhusiano wa Chadema, Boniface Makene alitoa
taarifa kwa vyombo vya habari akisema Wema ameamua kujiunga na chama hicho na
kwamba angekabidhiwa kadi siku iliyofuata.
Badala
yake, Wema, ambaye ni mtoto wa marehemu Balozi Isaack Sepetu, alitangaza uamuzi
huo akiwa nyumbani kwao Mwananyamala, akisema ameamua “kuvaa gwanda” kwa hiari
yake, hasa kwa kuwa ni mwanademokrasia.
Wema
alisema kuna watu wengi nyuma yake, huku mama yake akisema ndugu zake wote
wameamua kuihama CCM na kujiunga na Chadema.
Wasomi
wamjadili Wema
Akizungumzia
hatua hiyo ya Wema, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania (OUT), Salim Hamad alisema huo ni mchezo wa siasa utakaoiathiri CCM.
“Safari ya
Wema itakuwa na athari kwa kutegemea jinsi kila chama kinavyocheza karata yake
ya mwisho,” alisema.
“Wema kama
msanii ana wafuasi wengi pamoja na wasanii wenzake wenye ushawishi mkubwa.
Athari yake pia itategemea jinsi wasanii wenzake watakavyomuunga mkono.
“Ulimwengu
mzima, vyama vya siasa vinategemea celebrities (watu maarufu) kujitangaza.
Zamani vyama viliandaa makada kwa kuwapa mafunzo na kuunda vikundi
vilivyohamasisha. Siku hizi wasanii ndiyo wanategemewa kutangaza vyama vya
siasa.”
Maoni ya
Hamad yanalingana na mhadhiri mwingine wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, Richard Mbunda.
“Kwa sasa
unaweza usione athari kubwa, lakini kwa kuwa Wema ni msanii mwenye wafuasi
wengi hasa vijana na wao ndiyo wapiga kura, atakuwa na athari kwa CCM,” alisema
Mbunda.
“Ukitaka
kujua umuhimu wa Wema katika siasa ni pale CCM wenyewe walipomtumia kwenye
kampeni za uchaguzi za mwaka 2015 kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Hatuwezi kuona sasa kwa sababu si wakati wa uchaguzi, lakini kuna athari kubwa
kisiasa.”
Hata hivyo,
wasomi hao wanatofautiana na mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, Bubelwa
Kaiza aliyesema kuondoka kwa Wema CCM kunaweza kuwa ni kujisafisha na tuhuma za
kutumia dawa za kulevya.
“Chadema
inajijengea taswira kwamba viongozi na wanachama wake wananyanyaswa katika vita
ya dawa za kulevya, kwa hiyo watu kama Wema wataona kuwa huko ni sehemu ya
kujioshea dhambi zao,” alisema Kaiza.
Kada wa
Chadema na mchambuzi wa masuala ya siasa, uchumi na jamii, Albanie Marcosy
alimzungumzia Wema kuwa miongoni mwa vijana walimbwende na wanapiganaji
aliyejiweka wazi kushiriki na kupambania siasa ambaye atarudisha vijana
waliowapoteza wakati wa uchaguzi.
“Ni kati
ya watu waliofanikiwa kuwavuta nyuma vijana na hasa wasichana na kuacha kuunga
mkono Chadema na tukapoteza sana ushawishi kwao,” alisema.
0 comments:
Post a Comment