Social

Thursday, February 23, 2017

Wivu kati ya utawala, upinzani tatizo kubwa barani Afrika



By LUQMAN MALOTO
Lipo tatizo la kutoachiana nafasi ya kisiasa kati ya vyama tawala na wapinzani. Hali hii inasababishwa na vyama kuoneana wivu. Uchaguzi umekwisha, kila upande unakuwa umevuna stahiki yake. Hata hivyo chuki na kuoneana gere za kisiasa vinadumu miaka na miaka.
Binafsi naamini katika dini na Mungu mmoja. Naamini kuwa Mungu ni sababu ya kila kinachojiri duniani, hivyo hawezi kupatikana kiongozi iwapo Mungu hajataka. Kwa mantiki hiyo, nidhamu ya kwanza ya kimaisha ni kutambua uwepo wa kiongozi na kumheshimu kwa nafasi yake.
Kumtambua na kumheshimu kiongozi kwa nafasi yake ni ufunguo wa nafsi yako kuwa na mawazo chanya juu yake hata kama hukubaliani naye. Ukishatambua ni kiongozi, mpe thamani yake.
Unapompa thamani kiongozi, basi atakapofanya vizuri utamsifia hata kama kiitikadi mnapishana, maana hafanyi kwa ajili yake bali kwa taifa zima. Kwa thamani hiyo hiyo, akikosea utamsahihisha kwa namna bora ili afanye vizuri.
Unapomsahihisha kiongozi ili afanye vizuri au unapomsifia anapofanya vema, usitazame kwa jicho la kumjenga, bali fikiria kwa jicho la ujenzi wa nchi. Anapoitwa kiongozi maana yake amebeba matarajio kwa kipindi husika.
Mathalan, kwa sasa Rais wa Tanzania ni Dk John Magufuli, hata kama hukubaliani naye ndiye Rais mpaka mwaka 2020 na Mungu akipenda atafika mwaka 2025. Je, ni gharama kubwa kiasi gani kwa nchi kama Rais hatafanya chochote?
Suala la maendeleo ya nchi na huduma kwa raia ni muhimu kuliko tofauti za kiitikadi na matamanio ya madaraka. Viongozi waliopo wanaposhindwa kufanya vizuri haitakiwi iwe kicheko kwa baadhi ya watu, bali kilio kwa taifa zima. Maana ni hasara ya taifa zima siyo waliopo madarakani peke yao.
Mfano mwingine; hivi sasa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inaongozwa na Chadema na Ukawa. Haitakiwi kuwapiga ‘misumari’ ili washindwe kulifanya jiji lipige hatua kulingana na matarajio yao, maana maendeleo watakayoyafanya yanahusu wakazi wote wa Dar es Salaam na taifa kwa jumla. Wakifeli, wananchi ndiyo hasara yao.
Tafakari mwenyewe ni kiasi gani Jiji la Dar es Salaam litakuwa kwenye hasara kubwa kama halmashauri ya jiji itashindwa kufanya kazi zake sawasawa kwa kipindi chake cha uongozi mpaka mwaka 2020.
Wivu na mipaka yake
Tunahitaji nchi isonge mbele, kwa hiyo ni vizuri wenye ridhaa ya kuongoza wawe wanapewa nafasi ili watekeleze yale yaliyomo kwenye ilani zao. Kuendekeza wivu wa kisiasa husababisha muingiliano usio na sababu.
Humpendi Rais Magufuli lakini ni wakati wake kuongoza nchi. Anapaswa kupewa nafasi, aungwe mkono na aombewe ili aipeleke nchi palipo na maono yake. Huo ndiyo msingi wa awamu za uongozi unavyotaka.
Kwa sasa Rais Magufuli na chama chake (CCM), wanalo deni kubwa kwa Watanzania. Utakapofika mwaka 2020 watatakiwa kuwa na majibu ya kile ambacho wamefanya ili warejeshewe nchi kwa mara nyingine.
Majibu rahisi kwa wapigakura ni maendeleo ya miundombinu kutoka walipoichukua nchi mpaka watakapokuwa wanaomba ridhaa nyingine. Wamejenga na kuboresha nini? Maisha ya Watanzania yatakuwa na unafuu mkubwa kiasi gani? Takwimu na matokeo ya kimazingira ndivyo vitawabeba.
Mwaka 2020, Chadema watakuwa na kibarua kingine cha kuwashawishi wakazi wa Dar es Salaam ili wapewe tena dhamana ya kuongoza halmashauri ya jiji. Kwa hiyo wasipopewa nafasi ili watimize kile walichokiahidi kwa wananchi wa Dar es Salaam, hasara ni kubwa.
Hiyo siyo kwa Halmashauri ya Dar es Salaam peke yake bali nyingine zote, walioshinda waachwe wafanye kazi zao kwa mujibu wa mipango yao. Kuwawekea vizingiti ni tatizo linalowaumiza wananchi wa maeneo husika na taifa kwa jumla.
Vizingiti si kwa masilahi ya wananchi bali kwa vyama. Taifa haliwezi kunufaika kwa wenye vyama kutetea masilahi ya vyama vyao kuliko ya wananchi. Siasa za vyama vingi hazikuwekwa ili kuwepo na misuguano ya aina hiyo.
Vyama vingi vipo kwa ajili ya kushindana kwa hoja kuhusu namna bora ya kuwaongoza wananchi. Wapigakura wanasikiliza vyama na wagombea kisha wanaamua upande ambao wanaridhika nao.
Ni vizuri kwamba wakati wale ambao wamepewa nafasi wanapokuwa kazini wanatakiwa kuungwa mkono, kusahihishwa wanapokwenda nje ya mstari kwa lengo la kujenga nchi moja. Hizo ndiyo siasa.
Wivu unaoumiza wananchi
Rais Magufuli anapotekeleza wajibu wake kama kuna mahali anakuwa amekosea, haitakiwi wapinzani wake washangilie, bali watoe hoja zenye kumsahihisha vizuri zaidi. Maana nchi inajengwa kwa ushirikiano mkubwa wa wananchi, chama tawala, wapinzani na hata wasio na vyama.
Wapinzani wanapokosoa wanaonekana kuwa hawana nia njema kwa Serikali. Matokeo yake kunakuwa na mvutano wa pande mbili, wakati nchi inayojengwa ni moja.
Siasa za kugombea fito ndizo ambazo zimekithiri Afrika nzima. Kila mahali hutaona mshikamano wa kisiasa kati ya utawala na upinzani. Nyakati zote watu huwaza uchaguzi.
Zipo nchi, viongozi waliopo madarakani huhakikisha upinzani unakufa ili kuwa na wakati mzuri wa vyama tawala kufanya siasa bila kusumbuliwa na presha za wapinzani.
Huo ndiyo wivu wa kisiasa ambao huumiza wananchi. Uwepo wa vyama vingi vya siasa ni kukaribisha mseto wa mawazo ya kujenga nchi. Wakati mwingine watawala wanaweza kuwa na mawazo ambayo siyo sahihi, hivyo wananchi wakaona upo unafuu mkubwa kama watabadili chama kwenye uchaguzi.
Inawezekana pia vyama tawala wakati wakiwa madarakani wakawa wanaazima mawazo ya wapinzani katika kuendesha nchi. Na matokeo huzaa faida kwa nchi nzima.
Ifahamike pia kuwa vyama vya upinzani uwepo wake ni chachu ya vyama tawala kuwajibika zaidi. Kwamba watawala wanaona kuwa wakichezea nafasi waliyonayo wananchi watawaweka pembeni na kuchagua wapinzani.
Kwa maana hiyo, badala ya vyama vya siasa kujikita katika kuoneana wivu au hata kuharibiana katika utendaji, vinapaswa kutambua na kuheshimu nafasi ya mwenzake.
Afrika upinzani wa kisiasa ni kama uadui. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, hivi karibuni alisema wapinzani wake hawamkosoi kwa njia ya kusahihisha na kuelekeza namna bora ambayo Serikali yake inatakiwa kushughulikia masuala ya maendeleo.
Bali alisema wapinzani wake wanataka aharibikiwe ili ionekane alishindwa, pia wanafanya jitihada za kumfanya ashindwe.
Luqman Maloto ni mwandishi wa habari, mchambuzi na mshauri wa masuala ya kijamii, siasa na sanaa. Ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius inayopatikana kwa anwani ya mtandao www.luqmanmaloto.com

0 comments:

Post a Comment