By Elizabeth Edward, Mwananchi
eedward@mwananchi.co.tz
Dar es
Salaam. Siku chache baada ya sauti ya msanii wa filamu, Steve Nyerere kusambaa
kwenye mitandao ya kijamii akisikika akizungumza na Mariam, ambaye ni mama
mzazi wa Wema Sepetu, mwigizaji huyo wa sauti za viongozi, amejitokeza na
kuwaomba radhi viongozi wote aliowataja.
Viongozi
hao ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Nape Nnauye na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba. Wengine
ni wabunge, Freeman Mbowe, Joseph Msukuma, Zitto Kabwe na Halima Bulembo.
Katika
mazungumzo hayo yaliyorekodiwa pasi na yeye kujua, Nyerere anasikika akieleza
jitihada alizofanya kuwashawishi wabunge na mawaziri kumsaidia Wema aliposhikiliwa
na Polisi kutokana na tuhuma za kutumia dawa za kulevya.
Alisikika
akisema baada ya Wema kukamatwa aliweka kambi bungeni Dodoma na kuwashawishi
wabunge kuanzisha mjadala wa kumnasua katika sakata hilo.
Akizungumza
na vyombo vya habari Dar es Salaam jana, msanii huyo alikiri kuwa sauti hiyo ni
yake na kwamba alitoa kauli hizo kumridhisha mama Wema ambaye alikuwa akimlaumu
kwa kushindwa kumsaidia bintiye licha ya ukaribu walionao.
“Naomba
ukweli usipindishwe sauti ile ni yangu, maneno yale yalikuwa ya uongo niliyatoa
kumtuliza mama na kujaribu kumzuia Wema asiondoke CCM maana walishaanza kusema
akitoka ndani wanahamia Chadema.
Namuomba
radhi Rais (John) Magufuli kwa kuwahusisha katika suala hili mawaziri wake
aliowaamini na kuwateua kwenye nafasi nyeti, nilifanya hivyo kwa kulinda
heshima ya chama changu maana sikuwa na namna ya kufanya kama binadamu.”
Alisema
hana mpango wa kukihama chama hicho tawala na ataendelea kukipigania kwani
ndicho ambacho kimemkuza.
Kuhusu
madai ya kuwashawishi wabunge wajadili suala la Wema bungeni Nyerere alisema,
“Namuomba radhi Spika kwa kusema niliwashinikiza wabunge kwa kuwa sina uwezo,
ujanja wala mamlaka hayo, nilisema uongo.”
Alikanusha
pia kuwa amevunja uhusiano na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda baada
ya kutokea kwa sakata hilo kama alivyosikika kwenye sauti na kudai kuwa hana
tatizo lolote na kiongozi huyo.
“Nje ya
kazi yake Makonda ni ndugu yangu, siwezi kugombana naye tunazungumza vizuri
kabisa, niko naye bega kwa bega na ninaunga mkono jitihada zake za kupambana na
dawa za kulevya.”
Wasanii
kuidai CCM
Nyerere
ambaye alikuwa mwenyekiti wa wasanii walioshiriki kwenye kampeni za CCM na
kaulimbiu yao ya “Mama Ongea na Mwanao” alisema hakuna hata mmoja ambaye
hakulipwa kama inavyodaiwa.
Juzi,
wakati akitangaza uamuzi wake wa kuhamia Chadema, Wema alisema yeye na wenzake
wanadai fedha zao CCM na kila wanapofuatilia wamekuwa wakizungushwa na kuambiwa
wamfuate Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
“Kama yupo
msanii ambaye alikuwa kwenye timu ya Mama Ongea na Mwanao na anaidai CCM
ajitokeze, mimi nilikuwa mwenyekiti, wote tulilipwa inavyostahili, tena Wema
ndiye anayeongoza kwa kulipwa vizuri akiwa kama Makamu Mwenyekiti,” alisema
Nyerere.
Wakati
akiendelea na mazungumzo hayo, msanii huyo alidondosha machozi huku akimtupia
lawama Mama Wema kwa kitendo cha kumrekodi na kusambaza mazungumzo yao. “Hadi
sasa najiuliza kwanini nirekodiwe? Mama hakuwa na nia njema na mimi. Je,
ningeongea matusi mle ingekuwaje? Nimepata uchungu sana maana niliamini
nilikuwa naongea na mama yangu ndiyo maana nikajiachia.
Jina hili
nimelitafuta kwa miaka 25, halafu leo mama anakuja kunichafua, napitia kipindi
kigumu mno lakini namwachia Mungu kwa kuwa nilifanya yote hayo kwa kumkumbatia
Wema, malipo yake ndiyo haya.”
0 comments:
Post a Comment