MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imevionya na kuvitoza faini vituo vya utangazaji vya televisheni na radio kutokana na kukikua maadili ya utangazaji.
Vituo vilivyoonywa ni Radio Times FM, Clouds FM, Channel Ten, na Stars Tv.
Akisoma uamuzi wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Mwenyekiti wa kamati huyo, Valerie Msoka amesema vituo hivyo vimebainika kukiuka sheria na kanuni za utangazaji chini ya Sheria ya Utangazaji ya 2005.
Amesema kituo cha Times FM katika kipindi cha Twenzetu katika sehemu ya mkubedo walifanya mahojiano na mwanamke ambaye anadaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mdogo wa mume wake katika muda ambao hautakiwi kisheria.
Msoka amesema kutokana na kosa hilo, Times FM imepewa onyo kali, kuomba radhi kwa siku nne na kulipa faini ya Sh milioni tatu ambazo zitatakiwa kulipwa ndani ya siku 30.
Msoka amesema, Channel Ten, kimepewa onyo kali na kutakiwa kuomba radhi kwa siku tatu katika taarifa ya saa moja jioni.
Amesema hatua hiyo ni baada ya kukutwa na hatia ya kutaja jina la eneo na jina la mama wa mtoto ambaye amelawitiwa wakati wa kuhitimisha taarifa ya Novemba 16 mwaka 2016, jambo ambalo ni kinyume na sheria ya utangazaji ya mwaka 2005.
Msoka amesema pia Kamati ya Maudhui imewakuta na hatia kituo cha Star TV kutokana na kipindi chao cha komedi cha Futuhi cha Oktoba 13, 2016 kilichoonesha mchezo ambao unadhalilisha taaluma ya ualimu na sekta ya elimu, kujenga hofu kwa wanafunzi wadogo, kupandikiza chuki kwa wanafunzi na kumonyonyoa maadili.
Amesema kutokana na kosa hilo, Star TV ambao wamekutwa na hatia kutokana na kukiuka Sheria ya Utangazaji inayotaka vituo vyenye leseni ya utangazaji kutengeneza vipindi vyenye ubora na staha na vyenye maudhui yasiyopandikiza chuki, wamepewa onyo kali, kuomba radhi kwa siku tatu katika taarifa ya habari na kulipa faini ya Shi milioni tatu ndani ya siku 30.
Clouds FM, Oktoba 3 mwaka 2016, katika kipindi cha Jahazi ambapo watangaziji wakiwa wanachambua taarifa za mchungaji kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha pili, mmoja wa mtangazji aliigiza sauti ya mchungaji, jambo ambalo lilidharirisha uchungaji na kudharirisha imani ya kidini, jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Alisema kutokana na kosa hilo, Clouds Entertainment FM imepewa onyo kali na kuomba radhi kwa siku tatu katika vipindi vya saa moja asubuhi.
“Vituo vyote vina haki ya kukata rufaa kama hawakubaliani na uamuzi wa kamati. Pia kwa vito vyote uombaji radhi unatakiwa kuanza leo,” amesema.
0 comments:
Post a Comment