Social

Friday, February 24, 2017

Wanafunzi wengi waliotajwa kukosa sifa walimaliza chuo kitambo – Saut



By Kelvin Matandiko na Jesse Mikofu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz
Dar/Mwanza. Hatua ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kutoa orodha ya wanafunzi zaidi ya 8,000 ikisema taarifa zao za uhakiki zina kasoro hivyo kuwa hatarini kukosa sifa za kuendelea na masomo, uongozi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) kimesema baadhi ya walioorodheshwa walishamaliza masomo zaidi ya miaka mitatu iliyopita.
Mbali na kauli hiyo, chuo hicho, vyuo vingine vya elimu ya juu na wadau wa elimu wameijia juu TCU wakisema taasisi hiyo ndiyo inayopaswa kubeba lawama.
Juzi, TCU ilitoa orodha ya vyuo 52 ambavyo ilidai wanafunzi wake walidahiliwa katika masomo ambayo hawakustahili na kutoa muda hadi Februari 28 kufanya uhakiki vinginevyo watapoteza sifa za uanafunzi.
Lakini jana, uongozi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine ulisema Serikali ndiyo inayopaswa kuwajibika.
Makamu Mkuu wa Saut ambacho kimetajwa kuwa na wanafunzi 1,046 wasiokidhi vigezo, Dk Thadeus Mkamwa alisema kuwa chuo hicho kilifuata taratibu zote lakini wameshangaa TCU ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kudahili wanafunzi, kutoa taarifa zenye mkanganyiko.
Alikosoa uhakiki huo wa TCU akisema wanafunzi waliotajwa katika chuo hicho, zaidi ya asilimia 70 walihitimu masomo zaidi ya miaka miwili hadi mitatu iliyopita. Alisema takribani mwezi mmoja uliopita, TCU ilitoa barua chuoni hapo ikieleza kuwapo wanafunzi ambao vigezo vyao vina shaka na hasa namba ya utambulisho (index number), hususani kwa wanafunzi wanaotoka nje ya nchi.
“Kigezo kingine ni kwamba baadhi yao vyeti vya diploma havionekani lakini, wao ndiyo wanaidhinisha, sasa tunajiuliza kazi yao ni ipi, haya ya kujitokeza mwishoni wakati watu wameshahitimu? TCU ndiyo wenye mamlaka ya kudahili wanafunzi sisi tunapokea tu majina ambayo wanaidhinisha, hata hizo namba za utambulisho wao ndiyo wamepewa mamlaka kuzihakiki wala si vyuo husika.”
Dk Mkamwa alisema iwapo kuna mabadiliko yanayofanywa bora taratibu zifuatwe kuliko kuleta mkanganyiko unaosababishwa na ukiukwaji wa sheria na taratibu katika sekta hiyo muhimu.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco), Dk Joyce Chonjo alisema wamepokea majina hayo na baada ya kukamilisha uhakiki, watazungumza.
Naibu Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Florens Luoga alisema inawezekana kuna taarifa za wanafunzi wao ambazo hazikukamilika kutokana na mazingira ya udahili wao.
Kwa mujibu wa TCU, kuna wanafunzi 224 wa chuo hicho ambao uhakiki wao una kasoro.

“Kwanza, sisi tunataka kujua TCU walichukua taarifa zipi, tunachotakiwa kufanya ni kuwasaidia kukamilisha taarifa ili tuone orodha hiyo usahihi wake ni upi, kama wapo hapa lazima tuwaondoe lakini lazima kufuata taratibu kwa usahihi na haki,” alisema Profesa Luoga na kuongeza kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wanafunzi hao waliotajwa na TCU wanatoka Msumbiji.

0 comments:

Post a Comment