By Mwandishi Wetu, Mwananchi
mwananchipapers@mwananchi.co.tz
Dar es
Salaam. Wakati Tanzania Bara ikikosa mikopo na misaada nafuu iliyotarajia
kutoka kwa wahisani, Zanzibar imepokea zaidi ya mara nne ya ilichotarajia.
Ripoti ya
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Fedha kwa
nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016/17 iliyotolewa mwezi huu, inaonyesha kuwa
jumla ya misaada kutoka kwa wahisani ilikuwa Sh22.1bilioni wakati matarajio
yalikuwa Sh5.4 bilioni.
Wakati
ripoti ya BoT ikieleza hayo, ripoti ya utekelezaji wa bajeti iliyotolewa na
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwa nusu mwaka, ilionyesha kati ya
Julai hadi Novemba, 2016, Tanzania ilipokea misaada ya Sh287.5 bilioni ambayo
ni sawa na asilimia 28.4 ya lengo la ambalo ni Sh1.01 trilioni ndani ya kipindi
hicho.
Waziri
alisema washirika wa maendeleo waliahidi kuichangia bajeti ya Serikali Sh3.6
trilioni lakini katika kipindi hicho jumla ya misaada na mikopo nafuu
iliyotolewa ilikuwa Sh603.9 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 21.5 ya lengo la
Sh2.8 trilioni katika kipindi hicho.
Waziri
alisema Serikali ilishindwa kutimiza masharti magumu yaliyowekwa na wahisani au
wakopeshaji.
Katika
kipindi hicho mapato ya ndani ya Serikali ya Zanzibar yalifikia Sh250.2 sawa na
asilimia 106.1 ya makadirio ya makusanyo. Ongezeko la makusanyo hayo limetokana
na kuimarika kwa ukusanyaji wa kodi za uingizaji wa bidhaa (import taxes), Kodi
ya Ongezeko la Thamani (VAT) pamoja na ukusanyaji wa ushuru wa bidhaa (excise
duties).
Kwa mujibu
wa ripiti ya BoT, katika nusu mwaka ya kwanza, urari wa biashara Zanzibar
ilikuwa na ziada ya Dola 35.4 milioni za Marekani kutoka nakisi ya Dola 40.9
milioni kwa kipindi kama hicho mwaka uliopita wakati Tanzania Bara ilikuwa na
nakisi ya Dola bilioni moja za Marekani ikiwa imepungua kwa asilimia 33.2
kutoka Dola 1.5 bilioni.
Wakati
Zanzibar ikikusanya zaidi ya makadirio, Tanzania Bara ilibana matumizi na
kuongeza fedha kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ripoti
inasema katika nusu ya kwanza, mapato yaliyokusanywa na kuwekwa kwenye akaunti
za Serikali zilizoko BoT yalikuwa Sh8.07 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia
22.1 ya mwaka 2015/16 lakini ni asilimia 96.0 ya makadirio ya kipindi hicho.
Mkakati wa
Serikali wa kubana matumizi umefanikiwa kuokoa asilimia 2.3 baada ya kuelekeza
Sh6.45 trilioni kwenye matumizi ya kawaida ikilinganishwa na mwaka 2015/16.
Matumizi
ya maendeleo yalikuwa Sh2.08 trilioni ambayo ni ongezeko la asilimia 14.7
ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliotangulia.
Licha ya
kuongeza uwekezaji, Serikali imepunguza deni la nje kwa asilimia 1.1 kutoka
Dola 17.18 bilioni za Marekani, Juni 2016 mpaka Dola 16.99 bilioni lililokuwapo
Desemba. Lakini, deni la ndani liliongezeka kwa asilimia 4.5 na kufika Sh10.47
trilioni kutoka Juni mpaka Desemba 2016.
Ongezeko
la deni la ndani lilitokana na kuuza dhamana na hati fungani ili kugharamia
bajeti ya Serikali.
Profesa wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana alisema licha ya umuhimu wa
mchango wa wahisani, nchi za Kiafrika zinapaswa kujitegemea katika utekelezaji
wa bajeti zao.
“Ufanisi
wa Zanzibar katika kupokea misaada unaonyesha wahisani hawakuwa na masharti
kama ilivyokuwa bara. Pamoja na kilichotokea, tumeona Serikali ikitekeleza
miradi mingi bila kuwategemea wahisani,” alisema.
Aliitaja
miradi ya ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro, hosteli
ya wanafunzi UDSM, nyumba za askari Magereza Ukonga na Serikali kuhamia Dodoma
na kusema, “Haya yote yasingewezekana kwa kuwategemea wahisani.”
0 comments:
Post a Comment