HATIMAYE meli ya kwanza kati ya tatu zinazojengwa katika Bandari ya Itungi kwenye Ziwa Nyasa wilayani Kyela imeteremshwa majini leo, Februari 24, 2017.
Meli hizo zinaundwa na mzawa, Kampuni ya Songoro Marine ya Mwanza ambapo ujenzi wake unahusu meli tatu, mbili za mizigo na moja ya abiria na mizigo.
Tukio la leo la kuteremshwa kwa meli hiyo ya kwanza lilishuhudiwa na Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo, Dk. Harrison Mwakyembe, viongozi wa serikali na Chama cha Mapinduzi wilayani Kyela.
Mkurugenzi wa kampuni inayojenga meli hizo, Saleh Songoro ameiambia tovut5i ya gazeti la Raia Mwema kuwa kazi ya leo ilikuwa kuteremsha tu meli hiyo majini na kwamba meli ya pili ya mizigo wanatarajia kuiteremsha majini siku ya Jumanne ijayo.
Hata hivyo amesema uwashaji wa meli hizo pamoja na majaribio bado, bali kilichofanyika leo ni kuziingiza majini na kuendelea na kazi za umaliziaji wake.
Songoro anasema kuwa wanatarajia kuanza kuziwasha baada ya wiki mbili huku suala la majaribio akisema litategemea kukamilika kwa taratibu za msingi na za kitaalamu katika ujenzi.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, ujenzi wa meli ya tatu ambayo ni ya abiria na mizigo utaanza Jumatatu ijayo.
Kukamilika kwa ujenzi wa meli hizo tatu unatarajiwa kumaliza tatizo la usafiri kwenye Ziwa Nyasa pamoja kuliingizia taifa mapato, hususani kupitia meli zake za mizigo zenye uwezo wa kubeba tani 1,000 kila moja na cherezo iliyopo kwenye Bandari hiyo ya Itungi.








0 comments:
Post a Comment