By Bakari Kiango, Mwananchi
bkiango@mwananchi.co.tz
Dar es
Salaam. Katibu wa waumini wanaomuunga mkono Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana
Tanzania, Dk Jacob Chimeledya, Thomas Gambo amesema kinachompa kiburi Dk
Valentino Mokiwa ni kuungwa mkono na baadhi ya mapadri, makasisi na mashemasi
ambao aliwawekea mikono akiwa askofu wa Dayosisi ya Dar es Saalam.
Akizungumza
kwa niaba ya wenzake jana, Gambo alisema Dk Chimeledya atafanya ibada ambayo
itahusisha kumsimika Naibu Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, itakayoamua
mustakabali wa mgogoro wa uongozi uliopo.
Ibada hiyo
itafanyika Kanisa Kuu la Dar es Salaam. Hata hivyo, hawakutaja siku bali
alisema katika ibada hiyo, Askofu Chimeledya atafanya mambo mbalimbali ikiwamo
kutangaza kubadilisha uongozi wa dayosisi na kuwapa upya viapo mashemasi na
mapadri.
Dayosisi
ya Dar es Salaam imekuwa katika mgogoro tangu Askofu Chimeledya amtake kiongozi
wake, Dk Mokiwa ajiuzulu kwa madai kuwa anatumia madaraka yake vibaya na tuhuma
za ubadhirifu.
Hata
hivyo, Dk Mokiwa alikataa kujiuzulu, akisema mkuu wake alikiuka taratibu ikiwamo
kufanya uamuzi ambao uko chini ya mamlaka ya dayosisi na kutopeleka uamuzi huo
kwenye Nyumba ya Maaskofu kama taratibu zinavyotaka.
Gambo
alisema: “Siku hiyo tutawajua mashemasi na mapadri wanaomuunga mkono Askofu
Chimeledya na Dk Mokiwa.”








0 comments:
Post a Comment