MABADILIKO ya Uongozi yaliyofanyika ndani ya Chama Cha Mapinduzi Zanzibar (CCM) mkoani Dodoma hivi karibuni, yamepokewa kwa maoni tofauti huku viongozi wapya wakitakiwa kujenga chama imara badala ya kukigawa kwani kinakabiliwa na kazi kubwa kupambana na upinzani.
Hayo yalisemwa na baadhi ya wanachama waliohojiwa na gazeti hili kutokana na mabadiliko ya nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar.
Katika mabadiliko hayo, Dk Abdalla Juma Mabodi aliteuliwa kushika wadhifa huo badala ya Vuai Ali Vuai.
Mwanachama wa CCM na mkazi wa Mkele, Ali Juma Sadiki alisema CCM inakabiliwa na kazi kubwa kupambana na upinzani wa CUF, hivyo Naibu Katibu Mkuu mpya anapaswa kwenda hadi katika ngazi ya chini kuimarisha chama.
Sadiki alisema ni kweli kwamba ari ya wanachama wa CCM imeshuka Zanzibar pamoja na jumuiya zake na ndiyo maana baadhi ya vijana wamekihama chama kwenda upinzani.
Alisema katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015, baadhi ya vijana walikataa kuipigia kura CCM na kwenda upande wa upinzani, hali ambayo kwa kiasi fulani iliathiri maendeleo ya chama na ushindi wake.
"Naibu Katibu Mkuu mpya aliyeteuliwa anakabiliwa na majukumu mengi, lakini kubwa kurudisha imani ya wanachama pamoja na kujenga chama imara kukabiliana na upinzani wa CUF ambao ni mkubwa na kasi yake haijapungua," alisema.
Naye Muridu Juma mkazi wa Makadara, alisema Uongozi mpya wa CCM Zanzibar una kazi kubwa kurudisha ari ya vijana waliokikimbia chama.
Alisema Umoja wa Vijana wa CCM unatakiwa kufumuliwa na kuundwa ili kuyaunganisha makundi ya vijana.
Asha Juma, wa Kitengo cha Itikadi na Uenezi cha Makao Makuu ya CCM Pemba, alisema wamepokea mabadiliko hayo kwa matumaini makubwa na yatasaidia kuimarisha chama.
0 comments:
Post a Comment