Dar es Salaam. Wakati kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe akilalamikia mchakato wa kupata uwakilishi katika Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Mwanasheria Mkuu wa Chadema ameutetea akisema hautatoa mwanya tena kwa CCM kuchagua wabunge wenye mwelekeo wao.
Katika hatua nyingine, CCM, ambayo itatoa wabunge sita kati ya tisa wanaotakiwa kuingia kwenye bunge hilo, jana iliteua majina ya wanachama wake 12 kwa ajili ya kupigiwa kura na Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Katika barua aliyoiandika juzi, Zitto anasema kwenye Gazeti la Serikali, Toleo Namba 11 la Machi 17, katibu wa Bunge alitangaza rasmi uchaguzi huo na aliambatanisha masharti ya uteuzi wa wagombea.
"Tangazo hilo ambalo kimsingi ni sheria, limeweka sharti kwamba vyama vyenye haki ya kuteua wagombea ni vile vyenye uwakilishi bungeni. Kila chama cha siasa kilitakiwa kuteua wagombea watatu kwa kila nafasi inayogombewa isipokuwa tu kwa kundi C ambapo Chama cha Mapinduzi hakiruhusiwi kuweka mgombea," alisema.
Zitto alibainisha kuwa vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni vimefanya mchakato wa uteuzi wa wagombea kwa mujibu wa kanuni na tangazo hilo, pia ACT Wazalendo imefanya mchakato wake wa uteuzi.
Alisema uamuzi wa Spika pia umeacha kuzingatia ukweli wa haki kwamba chama chochote cha siasa kinaweza kugombea nafasi yoyote katika makundi yote, isipokuwa CCM haiwezi kugombea nafasi ya kundi C peke yake.
Alisisitiza kuwa nyongeza ya tatu ya kanuni za Bunge inatumia mgawanyo wa viti kwa makundi yaliyoundwa miaka 15 iliyopita hivyo kutozingatia mgawanyo wa jinsia na pande za Muungano kwa makundi mengine.
"Kwa mfano, ni CCM peke yake ambayo inalazimishwa na kanuni kuzingatia uwiano wa kijinsia na pande za Muungano na hivyo kutokana na kupungua kwa nafasi za CCM katika Bunge la Afrika Mashariki, sura ya Muungano na usawa wa kijinsia kwa uwakilishi wa Tanzania kwenye bunge hilo inapungua hivyo kwenda kinyume na Mkataba wa Afrika Mashariki," anasema Zitto.
Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Bunge la Afrika Mashariki, Bobi Odiko alisema kwa kawaida wabunge wa Eala wanachaguliwa na Bunge husika la nchi mwanachama.
Alisema mfumo huo hutumiwa na mabunge hayo kwa kufuata idadi ya wabunge wa chama na kuamua jinsi ya kugawana nafasi hizo tisa.
"Kila Bunge lina kanuni ya kuchagua wabunge, mfano mwaka 2012 wabunge wa CCM, walizidi idadi ndani ya Bunge la Tanzania hivyo wakapata nafasi sita kati ya tisa, mabunge mengine katika nchi tofauti yamekuwa yakifuata mfumo huo," alisema.
Lakini Lissu alisema jana kuwa kanuni ziko wazi na zinakwenda sambamba na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema kanuni hizo zinazungumzia wabunge wa Afrika Mashariki kupatikana kutokana na uwiano.
"Hivyo, CCM ina nafasi sita, Chadema mbili na CUF moja," alisema Lissu.
"Kwa sababu sisi tuna nafasi mbili, Kamati Kuu imepitisha majina mawili tu. Kwa hiyo hawatakuwa na upinzani na maana yake watakuwa wamechaguliwa bila ya kupingwa. Kwenye chaguzi zetu hizi, hata zile za ubunge, usipokuwa na mpinzani, maana yake umeshinda bila ya kupingwa."
Chadema imepitisha wanachama wake wawili, Ezekia Wenje na Lawrence Masha kugombea nafasi hizo.
Lissu alisema waliamua kupigania kanuni hiyo kufuatwa baada ya kuona wabunge wa CCM wanatumia vibaya fursa hiyo.
Alisema awali katika nafasi za wapinzani, vyama vyote vilikuwa vikipeleka wagombea na hivyo CCM kutumia nafasi hiyo kupigia kura wale wenye mwelekeo wa chama chao au dhaifu.
"Sasa hawatapata nafasi hiyo kwa sababu sheria inataka wabunge wa Afrika Mashariki wachaguliwe kwa uwiano na inasema watateuliwa na vyama vyao," alisema.
CCM yateua 12
Katika mchakato kupata wabunge wa Eala, wanachama 12 kati ya 450 wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu, wamepitishwa kugombea uwakilishi huo. Kati ya waliojitokeza, wanawake walikuwa 93.
Walioteuliwa kutoka Tanzania Bara (wanawake) ni Zainabu Kawawa, Happiness Lugiko, Fancy Nkuhi na Happiness Mgalula. Wanaume ni Dk Ngwaru Maghembe, Adam Kimbisa, Anamringi Macha na Makongoro Nyerere.
Kwa Zanzibar, wanawake walioteuliwa ni Maryam Ussi Yahya na Rabia Abdallah Hamid wakati wanaume ni Abdallah Hasnu Makame na Mohammed Yussuf Nuh.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli aliongoza kikao cha Kamati Kuu ambacho kilipokea taarifa ya mchakato wa makada walioomba ridhaa ya kuwa wabunge wa Eala.
Polepole alisema ilizoeleka kwamba majina ya wanachama wanaoomba nafasi hizo yanapita Halmashauri Kuu, Kamati ya Wabunge wa CCM na baadaye Kamati Kuu, lakini mwaka huu wameamua kwamba majina hayo yapite Kamati ya Wabunge na Kamati Kuu.
"Waliochaguliwa ni watu madhubuti, wenye uwezo mkubwa, uzoefu na uadilifu. Ilikuwa ni kazi kubwa kuwapata wachache kwa sababu wengi wana sifa za kupewa dhamana," alisema Polepole.
0 comments:
Post a Comment