MFUMO wa kubaini uzembe kazini, urasimu na utendaji mbovu na kuwajua watendaji wazuri na wasiowajibika, umezinduliwa.
Mfumo huo umeandaliwa kwa lengo la kufuatilia ahadi za mgombea urais alizotoa wakati wa kampeni, maelekezo yaliyo ndani ya ilani ya CCM na maagizo ya viongozi kwa watendaji wa wizara, idara na taasisi husika, ambao pia wanatakiwa kutoa mrejesho wa utekelezaji wake kupitia mtandao huo.
Kwenye mfumo huo wa kielektroniki zimeingizwa ahadi zote 316 alizotoa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015, pia ahadi, maelekezo na maagizo 690 yaliyo ndani ya Ilani ya CCM ya 2015 hadi 2020, yameingizwa pamoja na maagizo mbalimbali ya viongozi wa juu serikalini.
Akizindua mfumo huo katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu mjini hapa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema utasaidia kuongeza ufanisi na uwajibikaji serikalini.
Alisema serikali imefanya mabadiliko kimfumo na kiteknolojia ikishirikiana na Kitengo cha Mawasiliano cha Serikali (E-government) kuhakikisha utekelezaji wa ahadi za serikali ya viongozi wa juu serikalini unafanyika.
Alisema mfumo huo pia umeingiza kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 - 2020/21) ili kuhakikisha Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza ahadi zake ilizotoa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Alieleza kuwa mfumo huo utasaidia kufuatilia usimamizi wa shughuli za serikali maagizo mbalimbali ambayo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amekasimiwa madaraka kupitia Katiba Ibara namba 52 (1) ya kusimamia shughuli za kila siku za serikali.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu, Dk Hamis Mwinyimvua alisema mfumo utaonesha ahadi zinazoangukia kila wizara, idara na taasisi pamoja na maagizo yaviongozi yanayotakiwa kutekeleza na hatua gani yamefikiwa.
Dk Mwinyimvua alisema mfumo huo pia utasaidia kuonesha vikwazo mbalimbali vinavyokwamisha utekelezaji wa maagizo au miradi mbalimbali na kutafuta njia ya kuviondoa ili kuhakikisha malengo ya kutekeleza ahadi hizo yanafikiwa kwa wakati.
0 comments:
Post a Comment