Tukio la kufunzana ndani ya CCM kutokana na athari za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, linatoa picha tofauti ya namna ambavyo aina ya uongozi kwenye chama unaweza kusababisha matokeo yenye kupishana.
Rais John Magufuli alipitia jaribio zito kuelekea kuteuliwa na CCM kuwa mgombea urais, kwa sababu ndani ya chama kulikuwa na wagombea wengine wenye nguvu zaidi.
Wagombea hao wenye nguvu ndiyo ambao walibeba matarajio makubwa kwamba mmoja wao angeweza kupewa tiketi ya kugombea urais kupitia CCM. Hali hiyo ndiyo hasa kiini cha tofauti zilizoibuka mwaka 2015 ndani ya chama hicho.
Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe walikuwa wagombea walioonekana kuongoza mbio za kuteuliwa.
Jina la Lowassa lilitajwa zaidi kuliko wagombea wengine. Na hata alipokatwa ndiyo lililosababisha watu wapige kelele na hata wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM kuimba kwamba imani yao ilikuwa kwa Lowassa.
Hicho ambacho kilitokea CCM ni kidogo mno kwa kile ambacho kilikikumba Chama cha Republican nchini Marekani wakati wa uteuzi wa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Novemba 8, 2016.
Kilichojiri Republican
Rais wa 45 wa Marekani, Donald Trump, alipata wakati mgumu zaidi ndani ya chama chake. Vigogo wa Repubican hawakumtaka na walipendekeza muwania tiketi mwenzake, Ted Cruz ndiye apitishwe ili kukiokoa chama hicho.
Haikuwa siri kwa Trump kuwa vigogo wa chama hawakumtaka. Alipingwa na wazee pamoja na matajiri ambao ndiyo nguzo ya kiuchumi ya wagombea wa Republican. Jitihada nyingi zilifanyika kumzuia asipate nafasi ya kugombea.
Trump alibaki kuwa mtu pendwa kwa wanachama wa kawaida wa Republican, hususan wajumbe wa makongamano yenye kupiga kura kwenye majimbo ya kuchagua mgombea urais wa chama.
Hali hiyo ilimfanya aonekane ni mpiganaji vitani mithili ya jeshi la mtu mmoja. Kwamba kila upande kwenye chama alikuwa anashambuliwa akose tiketi.
Faraja yake pekee ilikuwa wanachama waliomuunga mkono, zaidi ni wajumbe wenye kupiga kura ambao walimfanya aongoze kila alikopita.
Kipindi Trump alipokuwa anapata ushindi kila alikopita dhidi ya wawania tiketi wenzake, upande wa pili Republican ilikumbwa na mgawanyiko mkubwa kuwahi kutokea, kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya chama hicho.
Wakati viongozi wakimkataa, vilevile lilikuwapo kundi kubwa la wanachama wa Republican walioripotiwa sehemu mbalimbali wakichoma moto kadi zao za uanachama, kuonyesha hasira zao kwa Trump kupata kura nyingi dhidi ya wawania tiketi wenzake.
Yalitokea matamko mbalimbali ya wanachama wa Republican, wakiwamo viongozi wakubwa walioahidi kutoshiriki kabisa kumpigia kura kwa kuwa hawakumtaka, vilevile hawakuwa tayari kumpigia kura mgombea wa wapinzani wao, Democrats yaani Hillary Clinton.
Lilikuwapo kundi lingine wanachama na viongozi wa Republican ambao waliahidi bila kificho kuwa wangempigia kura Clinton kwa sababu hawakuwa tayari kuona Trump anakuwa Rais wa Marekani.
Aliyekuwa Rais wa 41 wa Marekani, George HW. Bush mwenye umri wa miaka 91, alisema wazi kwamba alijiweka kando katika uchaguzi huo kwa sababu hakuwa na mpango wa kumuunga mkono Trump.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa rais huyo mstaafu (Bush baba) kutomuunga mkono mgombea wa chama chake cha Republican katika uchaguzi.
Bush baba aliungana na mwanaye (George W. Bush) ambaye ni Rais wa 43 wa nchi hiyo aliyetangaza pia kujiweka kando katika uchaguzi huo na kutomuunga mkono Trump.
Ifahamike kuwa marais wastaafu waliotokana na Republican waliobaki hai ni wawili, kwa maana ya Bush mtoto na baba. Hivyo, Trump hakuungwa mkono na marais wote wastaafu wa chama chake waliopo hai.
Aliyekuwa mgombea urais wa Republican mwaka 2012, Mitt Romney aliahidi kutomuunga mkono Trump na alikwenda mbali zaidi kwa kukataa kuhudhuria mkutano mkuu wa kumtangaza rasmi Trump kuwa mgombea, uliofanyika Cleveland, Marekani.
Aliyekuwa mgombea urais wa Republican mwaka 2008, John McCain naye alitoa taarifa yake ya kutomuunga mkono Trump. Hivyo wabeba bendera wote wa Republican katika nafasi ya urais kwenye miongo mitatu iliyopita walimkana Trump.
Pia, athari ya matajiri wapenzi wa Republican kugawanyika ilikuwa kubwa.
Matokeo yake Trump aliweka rekodi ya kuwa mgombea urais aliyechangiwa fedha kidogo zaidi za kampeni katika historia ya chama hicho.
Hata baada ya kushinda, Trump ameweka rekodi ya kuwa Rais wa Marekani ambaye katika kampeni zake, mikutano ya uchangishaji fedha ilidorora kuwahi kutokea.
Wapo matajiri wa Republican walijitokeza na kumuunga mkono Clinton kwa kuandika hadharani kaulimbiu ya Hillary Clinton iliyosema I am with her, wakimaanisha wanamuunga mkono Hillary Clinton na si mgombea wa chama chao.
Magufuli na Trump
Mpaka hapo unaweza kuona kuwa Trump alipita kipindi kigumu mno. Ni rahisi kukiri kwamba Rais Magufuli alipitia wakati rahisi kwenye chama kuliko Trump.
Tofauti iliyopo kati ya Trump na Magufuli ni kuwa wakati Trump alitengwa na viongozi pamoja na vigogo wa chama, Rais Magufuli alibebwa na viongozi wa juu kisha vigogo wa CCM walipambana kuhakikisha ushindi unapatikana.
Viongozi na vigogo wa Republican, walisimama waziwazi kuwashawishi wanachama, hususan wajumbe wa makongamano ya kuchagua mgombea urais, wasimchague Trump, wakieleza kuwa angekigawa chama hicho.
Viongozi na vigogo wa CCM walisimama kifua mbele kushawishi wanachama wa CCM kumpokea Rais Magufuli na kumchagua kwa maelezo kuwa ndiye alikuwa chaguo bora kwa chama hicho.
Trump alisimama peke yake, Rais Magufuli alizungukwa na vigogo wa chama. Marais wote wastaafu walio hai, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete walikuwa pamoja naye.
Marekani, Trump alikuwa na wakati mgumu kwa sababu Rais aliyekuwa madarakani, Barack Obama alikuwa akimfanyia kampeni mpinzani wake yaani Hillary, wakati Tanzania, Rais aliyekuwa madarakani, Jakaya Kikwete aliingia vitani hasa kumtafutia kura Rais Magufuli.
Ugumu mwingine kwa Trump ni kwamba chama chake kilikuwa cha upinzani wakati Rais Magufuli, CCM yake ndiyo ilikuwa chama tawala, hivyo alikuwa na nafasi nzuri ya kuzidi kubebwa na chama chake.
Matokeo ya baadaye
Trump hata baada ya kushinda urais na kuanza kuongoza Serikali ya Marekani, amekuwa akikumbana na ukosoaji kutoka kwenye chama chake pindi anapofanya uamuzi ambao uongozi wa Republican hauuafiki.
Mathalan, uamuzi wake wa kuweka zuio kwa raia wa mataifa ya Kiislam kuingia Marekani ulipingwa na Republican kwamba ni wa kibaguzi.
Rais Magufuli yeye amekuwa akiungwa mkono na chama chake. Zaidi alikabidhiwa uongozi wa CCM, hivyo kuunda sekretarieti ambayo ameitaka mwenyewe. Wakati huo Trump yeye siyo kiongozi wa Republican.
Rais Magufuli ndiye sauti kuu ya CCM kwa sasa, wakati Trump kwenye chama hana mamlaka yoyote. Ndiyo maana Trump hata baada ya changamoto zote alizopitia, urais wake haumpi nguvu ya kumtimua yeyote kwenye chama.
Hiyo imekuwa bahati ya Republican kwamba mamlaka za chama na Serikali zimetenganishwa. Rais anayetokana na chama hicho anapewa heshima ya urais, lakini anabakia kuwa ni mwanachama wa kawaida.
Kama Republican wangekuwa na utaratibu kama wa CCM wa kumpa Rais wa nchi uongozi wa chama chao, Trump angefyeka viongozi wote wa juu na angeweza kuwatimua uanachama vigogo wote ambao walimchachafya alipokuwa anawania tiketi ya kuwa mgombea urais kisha alipokuwa mgombea urais.
Machi 10, mwaka huu aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Sophia Simba pamoja na wanachama wengine 11 wa CCM waliokuwa wakishika nyadhifa mbalimbali CCM, walivuliwa uanachama kwa tuhuma za usaliti.
Julai, 2016, Rais Magufuli alipokuwa anahutubia Mkutano Mkuu wa CCM baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa chama hicho, alisema kuwa kama yeye ndiye angekuwa mwenyekiti kipindi wajumbe wa NEC wanaimba wana imani na Lowassa, basi wangepotea. Machi 9, mwaka huu, Rais Magufuli alipokuwa anatetea mabadiliko ya chama hicho, alirejea tukio hilo la wajumbe kuimba wana imani na Lowassa, kuonyesha kuwa lilimkera mno.
Kutokana na Rais Magufuli kukerwa na wana CCM waliomuimbia Lowassa na uamuzi wa chama chake kutimua wanachama, kuwavua uongozi baadhi yao na wengine kuwapa onyo ni dhahiri kilichotekelezwa ni mkinzano wa kifkra na mtazamo miongoni mwa wajumbe wa Nec.
Na kutokana na ukweli kuwa Trump alipata wakati mgumu sana Republican kuliko Magufuli CCM, hizo ndizo tofauti zilizopo baina ya vyama hivi.
Sasa basi, kwa hali hiyo ni wazi kwamba kama mazingira ya Trump ndani ya Republican yangemkuta Rais Magufuli CCM, bila shaka angetimua wote na kukisuka chama chake upya kwa kadri anavyotaka yeye.
0 comments:
Post a Comment