Na hii hasa ni kwa wale walioshika nyadhifa ndani ya chama, lakini baadaye wakahama kabla ya kuamua tena kurudi.
"Kiongozi atakayehama kisha akajiunga na chama kingine, akirudi na akataka kugombea tena nafasi yoyote ya uongozi, atalazimika kusubiri miaka mitatu," alisema katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole katika mahojiano maalumu na waandishi wa Mwananchi.
Alisema hayo ni masharti yaliyowekwa katika ibara ya 13 ya katiba ya CCM iliyofanyiwa marekebisho na kupitishwa mjini Dodoma mapema mwezi huu.
Alisema kifungu hicho kimeongezwa kwenye mabadiliko ya katiba, ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja baada ya CCM kushuhudia mawaziri wakuu wawili wa zamani, wenyeviti wa mikoa, madiwani na viongozi wengine wa serikali za mitaa wakitangaza kuhamia upinzani.
Hata hivyo, baadhi walirejea baada ya Uchaguzi Mkuu ambao CCM haikushinda kwa kishindo kama zilivyokuwa chaguzi nyingine kutokana na wapinzani kupata viti zaidi vya ubunge na udiwani.
Polepole alisema kiongozi yeyote aliyeondoka atatakiwa kwenda kwenye tawi lake kuomba kurejea, huo ukiwa ni mtindo tofauti na wa sasa ambao viongozi walioihama CCM hupokelewa kwa bashasha katika mikutano ya hadhara ya viongozi wa kitaifa.
"Wanachama wapya wanapokelewa kwenye matawi," alisema.
Mkutano huo ulifanya mabadiliko kwenye maeneo matatu ambayo ni utawala, muundo na mfumo pamoja na uongozi ambayo yalianza kwenye Mkutano Mkuu uliompa Rais John Magufuli uenyekiti wa chama.
Polepole alisema katika Mkutano Mkuu Maalumu, CCM iliweka misingi ya Serikali iitakayo na wajumbe wote walipewa nyaraka za mabadiliko ya katiba muda mrefu ili kuyaelewa.
"Wamefanya hili kwa sauti moja. Kila mageuzi makubwa yanayofanyika yanaenda sambamba na marekebisho ya katiba ambayo yataidhinishwa na mkutano mkuu," alisema.
Kabla ya mkutano huo, Halmashauri Kuu ya CCM iliridhia adhabu dhidi ya wanachama wanaotuhumiwa kukihujumu chama hicho wakati wa Uchaguzi Mkuu, baadhi wakivuliwa uanachama, kupewa onyo, kuvuliwa uongozi na kutakiwa kuomba radhi.
Adhabu hizo zilizoridhiwa na chama ziliwahusisha wanachama 12, akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba ambaye pia alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu.
"Kosa kubwa CCM ni kukisaliti chama ama kukifanya kishindwe uchaguzi au kinuke mbele ya umma. Ukiwa mbadhirifu wa mali ya umma unasababisha chama kinuke," alisema Polepole.
Alisema adhabu hizo zilianza mara moja zilipotolewa Machi 11 na tayari chama kimeshaanza kuchukua mali walizokuwa nazo waliofukuzwa.
"Ukiwa na mwanachama ambaye kwa matendo yake anakigawa chama, haleti umoja au kada ambaye kwa matendo yake anachafua taswira ya chama kwa umma, huyo anatakiwa achukuliwe hatua," alisisitiza Polepole.
Mchakato wa Katiba
Polepole, ambaye alikuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, pia alizungumzia mchakato uliokwama wa mabadiliko ya Katiba.
Alipoulizwa inakuwaje inakuwa rahisi kwa chama kubadili katiba yake badala ya Katiba ya nchi, Polepole alisema: "Katiba ipo kwenye mikono salama na muda muafaka ukifika mchakato wake utaendelea."
Katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari, Rais John Magufuli alipoulizwa kuhusu mchakato wa Katiba mpya, alisema aachwe kwanza ainyooshe nchi.
Akifafanua kauli hiyo ya mwenyekiti wake, Polepole alisema kwa mazingira yaliyopo ni ngumu kuukamilisha mchakato huo.
"Rais alisema anainyoosha nchi; atafanya hivyo kwa Serikali kisha kwa chama. Kwa taarifa yako, walioipinga Katiba Mpya ni CCM na kwa hali ilivyo, lazima wataikataa tena ikiletwa. Lakini baada ya kunyooshwa itakuwa rahisi," alisema.
Alifafanua kilichotokea kwenye Bunge Maalumu la Katiba kati ya chama tawala na vyama vya upinzani kwamba ilikuwa ni kuviziana ili kutofautiana.
"Wapinzani walikuwa wanasubiri kuona CCM watakuwa upande upi ndiyo maana walipoona wameipinga, wao wakaikubali," alisema.
Polepole alisisitiza kuwa kinachotakiwa ni nchi kunyooshwa kwa kuimarisha nidhamu ya viongozi wa umma ili kuhakikisha wanatoa huduma kwa kiwango ambacho Watanzania wanakitarajia.
"Viongozi wanatakiwa kuwasilikiliza wananchi, kuelewa kero zao na kuzitatua kwa moyo mmoja na nguvu zote. Hiyo ndiyo ajenda ya CCM," alisema Polepole.
Alibainisha kwamba msimamo wake juu ya Katiba Mpya haujabadilika baada ya kuwa kiongozi wa CCM, lakini anaungana na imani ya Rais kwamba baada ya wananchi na viongozi kunyooshwa ndipo mchakato huo utatekelezeka bila usumbufu.
Hata hivyo, alisema jambo hilo litachukua muda mrefu.
"Hili huwezi kulitengeneza ndani ya wiki moja. Baada ya kunyoosha Serikali, tunakwenda pia kunyooshana wenyewe kwa wenyewe ndani ya CCM. Tumeifanyia maboresho katiba ya chama. Tukifanya hivyo jambo la Katiba ya nchi ni rahisi ni lazima viongozi waweke mbele masilahi ya nchi," alisema.
Alisema kipindi hiki cha mpito ambacho Rais anainyoosha nchi na Serikali, ufanisi wa kuwaletea maendeleo wananchi umeongezeka na kujidhihirisha kwenye upatikanaji wa maji, elimu na uboreshaji wa miundombinu.
Suala la kuandikwa kwa Katiba mpya lilianza Desemba 31 mwaka 2011, wakati Rais Jakaya Kikwete alipozindua mchakato huo ambao ulionekana kuwa kipaumbele cha Taifa. Kufanikisha hilo, aliteua wajumbe 30 ambao waliongozwa na Jaji Warioba. Wajumbe 15 walitoka kila upande; Bara na Zanzibar.
Hata hivyo, Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na tume hiyo iligonga mwamba mwanzoni wakati wajumbe wa Bunge la Katiba wakijadili muundo wa Muungano, hali iliyofanya wajumbe wengine, hasa kutoka vyama vinne vya Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi kususa.
Baadaye vyama hivyo viliunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uliokubaliana hadi kusimamisha mgombea mmoja wa urais katika Uchaguzi Mkuu 2015.
Wachambuzi
Akizungumzia mabadiliko ya katiba ya CCM, Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba, Hebron Mwakagenda alisema yanalenga kumpa mamlaka zaidi Rais Magufuli ndani ya chama ndiyo maana ameyaharakisha.
"Ukiangalia mabadiliko aliyofanya Rais Magufuli kwenye katiba yao ni kujiongezea madaraka tofauti na Katiba ya nchi inayowapa wananchi madaraka zaidi na hakuna kiongozi anayependa hilo. Ndiyo maana utaona anachelewa kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya," alisema Mwakagenda.
Hata hivyo alisema wanaendelea na mikakati ya kufufua mijadala ya mabadiliko ya Katiba ili kufanikisha mchakato wake.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini tawi la Josiah Kibira la mkoani Kagera, Dk Azavel Lwaitama alisema kilichofanyika ni kuwaondoa makada wanaoweza kuhoji vinginevyo katika uchaguzi wa mwaka 2020.
"Japo taarifa ya kuwafukuza uanachama haitaji kosa mahsusi bali ukiukwaji wa maadili, lazima niwe makini kama mwalimu. Waliosema 'wana imani na Lowassa' ni wengi. Sasa huo usaliti uko wapi?" alihoji.
"Waliompigia kura Rais Magufuli hadi akafika kwenye tatu bora ni haohao wafuasi wa Lowassa kwa sababu hawakuondoka kwa maana wasingempigia (Bernard) Membe. Kwa sababu ushindani ulikuwa ni kati ya Membe na Lowassa, baada ya mmoja kuenguliwa, wafuasi wake ndiyo wamempa Magufuli, huo usaliti uko wapi?"
Dk Lwaitama alisema mabadiliko hayo yamelenga kujenga chama cha mtu mmoja kwa kupunguza idadi ya wajumbe wa NEC na kamati kuu ili ikifika mwaka 2020 kusiwe na upinzani ndani ya chama.
0 comments:
Post a Comment