Dar es Salaam. Wakati Spika wa Bunge, Job Ndugai akijiandaa kuunda kamati itakayochunguza uchimbaji na usafirishwaji wa mchanga wa dhahabu, Rais John Magufuli ameteua kamati ya wataalamu watakaofanya uchunguzi ili kubaini kiwango cha madini kilichomo ndani ya makontena yaliyozuiwa kusafirishwa kwenda nje kuyeyushwa.
Lakini, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ameonyesha kushangazwa na kinachoendelea katika sakata hilo la mchanga wa dhahabu, akisema kuzuia makampuni yanayochimba madini kusafiri sha mchanga kwenda nje ni kukiuka mikataba na sheria ya madini.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi imeeleza kuwa kamati hiyo yenye wajumbe wanane, inatakiwa kuanza kazi haraka iwezekanavyo.
Kijazi aliwataja wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni pamoja na Profesa Abdulrahman Hamis Mruma, Profesa Justinian Rwezaura Ikingula na Profesa Joseph Bushweshaiga.
Wengine ni Dk Yusuf Ngenya, Dk Joseph Yoweza Philip, Dk Ambrose Itika, Mohamed Zengo Makongoro na Hery Issa Gombela.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa wajumbe wote wa kamati hiyo wanatakiwa kufika ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu jijini Dar es Salaam Machi 31 saa 4:00 asubuhi.
Kuundwa kwa kamati hiyo kumekuja wakati Rais Magufuli akifuatilia utekelezaji wa amri aliyoitoa Machi 2 kuzuia usafirishaji wa mchanga kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuyeyushwa ili kupata mabaki ya madini yaliyoshindikana baada ya hatua ya kwanza ya uchenjuaji kufanyika mgodini.
Mchanga huo unatoka mgodi unaoendeshwa na kampuni ya Acacia, ambayo inaeleza kuwa asilimia kubwa ya madini yaliyomo ni shaba, zaidi ya asilimia 15, dhahabu na fedha ambazo ni takriban asilimia 0.02. Michanga hiyo inatoka kwenye migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu.
Lakini Lissu, ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki alisema kuzuia madini hayo kusafirishwa kwenda nje ni kukiuka mikataba na sheria ya madini, akisema madini mengine si yetu.
"Hili halizungumzwi kabisa na liko katika mikataba. Madini mengine si yetu kwa sababu haihesabiwi katika asilimia nne ya dhahabu," alisema mwanasheria huyo wa kujitegemea alipotembelea ofisi za Mwananchi jana.
"Kwa purposes (hoja) za kodi hatuna cha kwetu isipokuwa asilimia nne ya royalty (mirabaha)."
Alisema Sheria ya Madini ya mwaka 1998 inaeleza bayana kuwa kama mwekezaji akipewa leseni, chochote atakachochimba na kukiuza ni mali yake.
"Haki yetu ni asilimia 4 tu ya mirabaha. Kwa kifupi, kwenye madini tumewapa (wawekezaji) madini bure, tena kisheria," alisema.
Lissu alionyesha kushangazwa na hatua zinazochukuliwa sasa kuchunguza mchanga huo, akisema Rais Magufuli alikuwa katika Baraza la Mawaziri wakati Sheria ya Madini ya mwaka 1997 na 1998 zikipitishwa.
"Kwanza kwa mujibu wa mkataba, wawekezaji wana haki ya kusafirisha mchanga kwenda nje. Pili tulipokea na kutunga sheria ya madini ya mwaka 1998 wakati wa Serikali ya Mkapa na ilieleza kuwa madini yatakayochimbwa ni mali ya mmiliki, sasa sielewi serikali inapata wapi ujasiri wa kuzuia mchanga usisafirishwe. Kiufupi hatuna chetu," alisema Lissu.
Alisema mwaka 1997, Serikali iliwasilisha miswaada miwili ya sheria kwa hati ya dharura. Alizitaja sheria hizo kuwa ni Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Fedha na Sheria ya Uwekezaji.
Alisema sheria hizo ziliwapa wawekezaji uwezo wa kusafirisha nje faida yote na masuala mengine ya kulinda wawekezaji.
Alisema mwaka 1998, Serikali ilipitisha sheria nyingine iliyoondoa masharti ya umilikaji, ikitaka wawekezaji wawe na umiliki kamilifu. "Sasa Magufuli anapinga nini? Complete ownership? Transferability? Wasiposafirisha mchanga waupeleke wapi?" alihoji Lissu.
"Kwanini aende kupinga sheria bandarini. Rais akitaka kufuta sheria anakwenda bandarini? Si bungeni?"
Lissu alisema kibaya zaidi, Tanzania imeingia mikataba ya kimataifa inayowalinda wawekezaji hivyo kuna uwezekano mkubwa Serikali ikashtakiwa, jambo ambalo alisema litasababisha ilipe fedha nyingi.
Alisema Tanzania imejifunga katika mkataba wa kimataifa wa kulinda wawekezaji (Multilateral Investment Guarantee Agency, MIGA).
"Tumeingia mkataba wa MIGA, ambao mataifa makubwa huutumia kulinda vitega uchumi katika nchi zinazoendelea. Mkataba umetoa ulinzi kwa uwekezaji wa kampuni za kigeni na wanapoona maslahi yao yanaathiriwa na mifumo ya serikali watatumia MIGA kutupiga," alisema
MIGA ni taasisi iliyo chini ya Benki ya Dunia yenye makao makuu Washington, Marekani na ilianzishwa kwa lengo la kuimarisha uwekezaji, kupunguza umaskini na kuinua maisha ya watu kupitia uwekezaji wa nje katika nchi zinazoendelea.
Alitaja mambo mawili yanayohalalisha hatua ya uongozi wa mgodi wa Buzwagi kusafirisha mchanga nje kuwa ni kwa sababu Tanzania haina kinu cha kuchenjua madini ya dhahabu na mengine yanayozalishwa nchini.
Alisema ikiwa serikali ya Rais Magufuli inataka kuzuia kusafirishwa kwa mchanga kwenda nje, inatakiwa kuanza mchakato wa kujitoa kutoka mkataba wa MIGA, vinginevyo nchi italazimika kulipa fedha nyingi.
Lissu alizungumzia uamuzi wa Spika Ndugai kuunda kamati ya kupitia mikataba ya madini, akisema haitakuwa na jipya ikiwa haitazifanyia kazi ripoti mbili zilizowahi kuandaliwa na kamati za Lawrence Masha na Jaji Mark Bomani.
"Kumeshakuwa na kamati mbili huko nyuma, kamati ya huyu Lau Masha na kamati ya Mark Bomani. Hiyo kamati itakayoundwa lazima ipitie ripoti hizo na kujiridhisha, vinginevyo mambo yatakuwa ni yaleyale," alisema.
Alisema kamati hizo zilieleza udhaifu wote, lakini hadi sasa ripoti zao hazijafanyiwa kazi.
Ripoti ya kamati ya Jaji Mark Bomani mwaka 2008 na ile ya mwaka 2006 iliyoongozwa na Laurence Masha zilipitia migodi ya madini katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Mbeya, Mara na Tabora na zilizungumzia uharibifu wa mazingira, migogoro baina ya wawekezaji na wananchi na pia ilieleza kuwa uchimbaji wa madini haujaleta matunda katika uchumi.
Akitangaza amri hiyo ya kuzuia kusafirisha mchanga nje ya nchi alipokuwa akizindua kiwanda cha vigae cha Mkuranga mkoani Pwani Machi 2, Rais Magufuli alisema nchi imekuwa ikiibiwa, hasa madini.
"Tunachukua mchanga, tunausafirisha mpaka nchi nyingine ya mahali fulani. Eti wakachambue, wakatoe dhahabu iliyomo, na titarium na vanadium na nini. Wanavichambua huko na mchanga wanabaki nao hukohuko wanakwambia hatukupata kitu," alisema Rais Magufuli wakati huo.
"Sasa ni marufuku kusafirisha mchanga. Inawezekana matangazo haya yako live, na Waziri (wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter) Muhongo unisikilize. Hakuna kusafirisha mchanga kupeleka nje. Kama ni kuusafirisha tuulete hata hapa, tujenge kiwanda cha kuchuja, tutakuwa tunaona kuliko kupeleka nje."
Alikuwa akitimiza ahadi yake aliyoitoa Agosti 29 mkoani Geita ambako alisema katika Serikali yake hakuna mchanga utakaosafirishwa kwenda nje.
Wakati huo, Rais alisema anataka makampuni yanayochimba madini, yajenge kiwanda cha kuchenjua dhahabu hapa nchini kwa kuwa mchakato wake ni mdogo.
"Ukitoka kwenye mitambo hii ya madini yetu, utakuta ni Tanzania tu ndiko tunasafirisha michanga kwenda nje, na tunaambiwa kuwa ni michanga. Na wakati wa kurudi ile michanga hatuioni. Inapita kwenye barabara zetu eti inakwenda kusafishwa," alisema Rais wakati huo.
"Nataka kwenye utawala wangu hakuna mchanga utakaokwenda nje kusafishwa. Wajenge viwanda hapa, vijana wetu wapate ajira hapa, wasafishe madini hapa, tutajua zinc ni kiasi gani, copper ni kiasi gani. Tanzania tupate pesa. Tumechezewa vya kutosha. Hiyo ndiyo Tanzania ninayoitaka."
Utekelezaji wa amri hiyo ulioanza kufuatiliwa Machi 24 umekuwa na matukio kadhaa. Siku hiyo Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza bandarini na kushuhudia makontena 20 ya mchanga huo yaliyozuiliwa kutokana na agizo lake.
Taarifa iliyotumwa na Ikulu ilieleza kuwa Rais alifanya ziara hiyo ili kufuatilia agizo lake la kuzuia usafirishaji wa mchanga alilolitoa Machi 2.
Siku mbili baadaye, Mamlaka ya Bandari (TPA) ilitangaza kuwa imezuia makontena 262 ya mchanga uliokuwa Bandari ya Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa TPA Deusdedit Kakoko alisema kukamatwa kwa makontena hayo kulitokana na hatua ya Rais kwenda bandarini hapo na hivyo TPA ikafanya msako na kubaini idadi hiyo ya makontena yaliyokuwa tayari kusafirishwa.
Siku moja baadaye, Machi 26, Spika wa Bunge, Job Ndugai alifika bandarini ili kupata maelezo ya kina kuhusu makontena yenye mchanga. Spika aliambatana na wabunge 10, wakiwamo wenyeviti wa kamati za nishati na madini.
Akiwa katika ziara hiyo, Spika aliahidi kuunda kamati kwa ajili ya kuchunguza usafirishwaji wa mchanga huo, biashara ya madini, kiasi cha dhahabu kilichopo na iwapo biashara ina manufaa.
Machi 27, Rais alipokea ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na kumuagiza achunguze kwa kina biashara ya madini nchini ili kujua iwapo Watanzania wananufaika au kinachopatikana ni sawasawa.
Siku hiyo hiyo jioni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara mgodi wa Buzwagi wilayani Kahama na kuchukua sampuli za mchanga katika makontena, kwa ajili ya kuzipima.
Lakini wakati hayo yakitokea, imebainika kuwa Serikali ilishaagiza kufanyika kwa tathmini ya usafirishaji mchanga nje ya nchi na kuangalia uwezekano wa kujenga kiwanda cha uchenjuaji mchanga ulio na mabaki ya madini badala ya kusafirisha nje.
Ripoti ya uchunguzi huo uliofanywa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) mwaka 2011 inaonyesha gharama za kujenga kiwanda hicho wakati huo ilikuwa kati ya dola 500 milioni za Kimarekani na 750 milioni.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa viwanda vilivyojengwa sehemu nyingi vina uwezo wa kupokea zaidi ya tani 150,000 kwa mwaka, wakati uwezo wa nchi kuzalisha mchanga huo ni asilimia 40 tu.
"Wachambuzi wamethibitisha kwamba kiwanda cha kuyeyushia mchanga wa shaba kinahitaji si chini ya tani 150,000 za mchanga kwa mwaka ili kiendeshwe kwa faida," inasema taarifa hiyo.
"Kiwanda cha ukubwa huo utagharimu kati ya dola 450 milioni na 600 milioni za Kimarekani kukijenga pamoja na sulphuric acid kwa ajili ya kusafisha gesi inayotoka kwenye kiwanda hicho.
"Katika uwezo wake wa juu, uzalishaji wa mchanga wa BGM ni kati ya tani 25,000 na 50,000 kwa mwaka katika kipindi chote cha mgodi, kiwango ambacho ni kati ya asilimia 16 na 33 ya kiwanda cha kuyeyusha mchanga wa shaba.
"Ili kujenga kiwanda chenye faida nchini Tanzania, itahitajika kuingiza kutoka nje katika ya asilimia 67 na 84 ya mchanga wa shaba kukiwezesha kufanya kazi au kuongeza uzalishaji wa ndani wa mchanga."
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa ili kiwanda hicho kiweze kufanya kazi, ni lazima kuangalia gharama na upatikanaji wa umeme, ambao ni ghali na hautoshelezi mahitaji ya kiwanda kikubwa kama hicho.
Ripoti hiyo imeonyesha nchi 10 zinazosafirisha mchanga kwenda nje kwa ajili ya kuyeyusha na kusafisha kuwa ni Chile, Peru, Indonesia, Australia, Canada, Brazil, Kazakhistan, Marekani, Argenbtina na Mongolia.
Pia inazitaja nchi zenye viwanda hivyo zinazopokea mchanga kwa wingi kuwa ni India, Japan, China, Korea Kusini, Ujerumani, Hispania, Philippines, Bulgaria, Brazil na Sweden.
0 comments:
Post a Comment