JAJI wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sekela Moshi amewapa siku 10 mawakili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Longido mkoani Arusha, Onesmo ole Nangole kuwasilisha maelezo yao kwa maandishi kuomba kukata rufaa nje ya muda.
Alisema mahakamani kuwa mawakili wa Nangole, Method Kimomogolo na John Materu wametakiwa kufanya hivyo hadi Machi 22, mwaka huu na mawakili wa aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Stephen Kiruswa, wanapaswa kujibu maombi hayo kwa maandishi kabla ya Aprili 3, mwaka huu.
Alisema baada ya pande zote kuwasilisha maelezo kwa maandishi, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha itafanya majumuisho ya kuangalia kama hoja za pande zote mbili zimekidhi misingi ya kisheria na hilo litafanyika Aprili 7, mwaka huu.
Baada ya kupitia na kujiridhisha, Aprili 11, mwaka huu, Mahakama Kuu itatoa hukumu, kutupilia mbali maombi hayo au kupanga kusikiliza.
Juni 29, mwaka jana Jaji Silvangirwa Mwengesi aliyekuwa akisikiliza kesi, alimvua ubunge Nangole kwa kile alichoeleza kuwa taratibu za uchaguzi katika jimbo hilo zilikiukwa, ikiwamo baadhi ya vituo kura idadi ya kura kutofautiana na karatasi za majumuisho, uchakachuaji wa kihesabu na kutokea vurugu katika chumba cha majumuisho ya kura zilizosababishwa na Nangole na wapambe wake.
Nangole hakukubaliana na uamuzi huo na kuamua kukata rufaa katika mahakama hiyo. Jopo la majaji watatu wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jopo hilo, Jaji Sauda Mjasiri, Jaji Mussa Ibrahimu na Jaji Mussa Kipenka walikaa ili kuisikiliza rufaa hiyo.
Kabla ya kuanza, mawakili wa mjibu rufaa Daudi Haraka, Edmund Ngemela na Dk Masumbuko Lamwai walipinga kusikilizwa kwa madai kuwa imekosewa kisheria kwa kuwa haikuwajumuisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi Jimbo la Longido, hivyo inapaswa kutupiliwa mbali.
0 comments:
Post a Comment