Social

Friday, March 10, 2017

Vigogo TFF washinda kesi

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru vigogo wawili wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Martin Chacha na Juma Matandika baada ya kuwaona hawana kesi ya kujibu.
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amewaachia huru washtakiwa hao baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi saba wa upande wa mashtaka na kuona upande wa mashtaka umeshindwa kuthibisha shtaka pasipo kuacha shaka.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Shaidi amesema katika ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka unaonesha hakuna mtu aliyelalamika zaidi ya sauti kusambaa katika simu na mitandao.
Alisema ushahidi wa mashahidi saba wa upande wa mashtaka haukuonesha je ni kweli walikwenda TFF ama la, wala hakukuwa na uthibitisho ni kweli walitoka Geita kuja Dar es Saalam.
Kuhusu sauti zilizotambuliwa za Martin na Juma kupitia CD, Hakimu Shaidi amesema watu wana sauti za kufanana na hata kuigizana ni hatari tukiegemea huko hivyo ni lazima pawepo na uthibitisho.
"Kesi ya jinai ni kuthibitishwa pasipo kuacha shaka hapa kuna mashaka," amesema hakimu Shaidi.
Kutokana na kanuni za TFF mchezaji akibainika kudanganya alipaswa kuadhibiwa yeye, lakini timu hainyang'anywi pointi.
Hawa hawakuwa na mamlaka ya kunyang'anya pointi, hivyo wasingeshtakiwa kwa  kuomba rushwa labda utapeli.
Hivyo Hakimu Shaidi aliwaachia huru washtakiwa kwa sababu hawana kesi ya kujibu.
Kesi hiyo ilikuwa inaendeshwa na  Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai ambaye aliwaita mashahidi saba kutoa ushahidi na vielelezo   dhidi ya washtakiwa hao na kuufunga ushahidi wao Januari 27,2017.
Katika kesi hiyo, shahidi wa mwisho wa upande wa mashtaka alikuwa ni mchunguzi kutoka kitengo cha maabara ya uchunguzi wa kielektroniki Takukuru, Jonson Kisaka (30) ambaye alieleza jinsi alivyoifanyia uchunguzi simu ya mkononi ya Salum Kulunge iliyorekodi majadiliano ya kuomba rushwa ya Sh 25 milioni.
Ameeleza vifaa  vya kielektroni wanavyovifanyia uchunguzi ikiwamo kompyuta, simu, IPad na memory card na kwamba ni kutoka kwa washtakiwa na mashahidi na wanavifanyia uchunguzi vikiwa vimezimwa.
Amesema kifaa kinachotakiwa kufanyiwa uchunguzi yeye kama uchunguzi anakiweka katika mtambo wa kwanza kikiwa kimezimwa , mtambo ambao unachukua taarifa zote za simu husika tangu simu ilipotoka katika kampuni hata kama mtumiaji alizilifuta.
Baada ya kufanya hivyo taarifa hizo zinakuwa katika mfumo ambao hauwezi kutafsirika hivyo anatumia mtambo wa pili ambao unatasiri taarifa hizo, unazichambua na kutengeneza taarifa.

0 comments:

Post a Comment