Social

Tuesday, February 7, 2017

Walikosa uhakiki TIN Dar wajilaumu wenyewe na Sophia Mwambe



HIVI karibuni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilianza kuboresha taarifa za usajili wa namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN) ili kuondokana na mfumo wa kizamani wa usajili wa namba hiyo.
TRA ilitangaza kufanya uboreshaji huo tangu Agosti hadi Oktoba mwaka 2016, lakini iliamua kuongeza muda wa mwezi hadi Novemba 30 mwaka jana baada ya kuwepo kwa watu wengi kutaka kufanya uboreshaji huo. Hata hivyo, Serikali iliamua kuongeza tena muda wa siku 60 hadi Januari 31, mwaka huu.
Lakini licha ya kuongezwa kwa siku zote hizo bado kuna baadhi ya wananchi walishindwa kuhakiki taarifa zao huku wengi wao wakiamua tu kukaa na kusubiri mpaka siku za mwisho ndipo wajitokeze.
Mbali na changamoto zilizoelezwa na wananchi kuhusu mwenendo wa uhakiki ambapo wengi walilalamikia watoa huduma kuendesha taratibu na kuchangia msongamano mkubwa jambo ambalo ni la kweli, lakini wakati wa kuanza kwa uboreshaji huo watu vituo vingi vilikuwa na watu wachache.
Baada ya kutangazwa kuongezwa kwa muda wa kufanya uhakiki huo bado kuna watu ambao waliamua kukaa na kusubiri siku ya mwisho na hii inatokana na utamaduni ambao umejijengeka wa kusubiri dakika za mwisho iwe ni katika kujiandikisha, kusajili au kufanya uhakiki katika masuala mbalimbali yenye manufaa.
Kuendekeza utamaduni huu ulisababisha katika siku ya mwisho ya uhakiki huo kuwa na idadi kubwa ya watu ambao wangeweza kufanya uhakiki wao kabla ya muda huo wa mwisho kwani baadhi ya ofisi za mamlaka hiyo zilikuwa hazina watu wengi, hivyo kuepusha kuitupia mamlaka hiyo lawama.
Utamaduni huu wa wananchi kupenda kusubiri mpaka siku za mwisho sio tu kwa TRA bali hata katika uandishishaji wa kupiga kura hali ilikuwa hivyo lakini siku za mwisho wananchi wengi wanajitokeza huku wakitupa lawama kwa wahusika ilhali makosa wanayo wenyewe.
Ni wakati sasa kwa Watanzania kubadilisha mitazamo pale panapotakiwa kufanyiwa kazi wanapaswa kuchangamka na kwenda na muda na sio kusubiri siku ya mwisho ambayo ni lazima iwe na changamoto kwa kuwa itakuwa na watu wengi.
Ingawa TRA wametoa nafasi kwa wale ambao hawakufanikiwa kuhakiki taarifa zao kufanya hivyo kabla hawajahamia mikoani, lakini bado kuna umuhimu wa watu kuzingatia muda kwani si Dar es Salaam pekee ambao wanatakiwa kufanya uboreshaji huo.
Kwa baadhi ya wananchi ambao wameshindwa kuutumia muda huu ulioongezwa na TRA kwa uzembe wao, hawapaswi kuilaumu mamlaka hiyo bali wajilaumu wao wenyewe kwa kuzembea ama kudharau kwa kujua kuwa TRA itaongeza tena muda kwa ajili ya kufanya uhakiki kwa watu ambao hawajafikiwa.
Mwito wangu kwa wananchi wa mikoani ambako uboreshaji huo utakwenda wajitokeze kwa wingi na kufanya ukakiki kwa wakati utakaopangwa kuliko kukaa na kusubiri mpaka muda ukaribie kuisha ndipo wajitokeze na kuishia kulalamika.
Yapo maendeleo yanaweza kuja lakini kwa kuwa kuna utamaduni wa kuchelewa tutachelewa na kushindwa kufikia malengo na badaye tunaishia kulalamikia wahusika ambao hawakuhusika kutuchelewesha.
Siku zote watu wanaofanikiwa huwa wanafanya mambo yao kwa wakati hakuna maendeleo yanayoweza kuja kwa watu ambao ni wazembe kuchangamkia fursa hizo, ni lazima tubadili mitazamo yetu na sio mpaka usukumwe ndipo ufanye kitu.
Tunaishukuru TRA kwa kuamua kuongeza nafasi lakini sitamani kuona wananchi walioshindwa kufanya uhakiki wakilalamika kutaka muda tena baada ya kumalizika kwa muda huu, uhakiki huu unapaswa kwenda mikoani ni lazima wananchi mchangamke ili mtoe nafasi kwa wananchi wengine wa mikoani.

0 comments:

Post a Comment