Social

Thursday, February 9, 2017

Zuma atuma vikosi vya jeshi kulinda bunge


Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, ameamrisha vikosi vya kijeshi vipatavyo 440, kutoa usalama katika majengo ya bunge, wakati atakapokuwa akilihutubia taifa leo Alhamisi.
Vyama vya upinzani vimelaani hatua hiyo na kusema hiyo ni "kutangaza vita".
Hotuba za hapo awali za Bw Zuma, zilikumbwa na maandamano na fujo, huku wabunge wa upinzani wakitoa wito wa kujiuzulu kwake.
Kwa muongo mmoja uliopita, Bw Zuma amekuwa akiandamwa na madai ya kashfa ya ufisadi.
Taarifa kutoka kwa Ofisi ya rais na iliyotolewa siku ya Jumanne, inasema kuwa Bw Zuma aliamrisha kutumwa kwa vikosi hivyo vya wanajeshi, ili kushirikiana na maafisa wa polisi kutoa ulinzi.
Hii ni mara ya kwanza kwa wanajeshi wa nchi hiyo, kudumisha usalama, badala ya kuhusika katika sherehe.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa katika vyombo vya habari nchini humo, duru za kiusalama zimeonya kuwa kutatokea maandamano makubwa katika hafla hiyo.
Duru hizo zilisababisha hofu, kwamba huenda polisi wakashindwa kukabiliana nayo.
Hotuba za awali za kitaifa, zilikumbwa na fujo ndani ya bunge.


Tangu waliposhinda viti katika uchaguzi mkuu mwaka 2014, wanachama wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), wamekuwa wakitatiza hotuba ya rais Zuma na vikao vingi vya bunge kwa kupiga kelele na kumfokea hadharani rais kuhusiana na madai hayo ya kashfa ya ufisadi.

0 comments:

Post a Comment