Dar es Salaam. Waziri mpya wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe anakutana na kazi ya kumalizia changamoto saba alizoanzisha mtangulizi wake, Nape Nnauye.
Dk Mwakyembe aliapishwa rasmi jana baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kufanya mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri, ambapo Mwakyembe ameteuliwa kushika nafasi hiyo, huku wizara aliyokuwepo mwanzoni ya katiba na sheria, akiteuliwa Profesa Paramaganda Kabudi.
1. Viwanja
Moja ya changamoto kubwa ambayo imeonekana kuwa kikwazo kwenye wizara hiyo ni uvamizi wa maeneo ya wazi yaliyotegwa kwa ajili ya shughuli za michezo, utamaduni na burudani pamoja na uchakavu wa viwanja vingi vya michezo nchini hasa vile vinavyomilikiwa na chama cha Mapinduzi (CCM).
Juni mwaka jana, Nape aliahidi kushughulikia ukarabati wa viwanja vyote vinavyomilikiwa na CCM pia kuhakikisha maeneo yote ya wazi yaliyovamiwa kurudishwa ahadi ambayo ilianza kufanya kazi kwa kurekebishwa kwa viwanja vya Samora mkoani Iringa na ule wa Jamhuri Dodoma huku pi uwanja wa Namfua ulioko Singida nao ukianza kurekebishwa.
Hata hivyo, bado kuna viwanja vingi viko chakavu kama Jamhuri Morogoro, Majimaji Songea na Kambarage Shinyanga wakati huohuo bado zoezi la kurudisha maeneo ya wazi likionekana kusuasua.
2.Migogoro ya vyama
Changamoto ya migogoro iliyopo kwenye vyama vya michezo, ni mtihani wa pili unaomkabili
Mwakyembe kutokana na athari yake kwenye maendeleo ya michezo husika.
Miongoni mwa migogoro ambayo Waziri huyo anakwenda kukutana nao ni ule uliopo kwenye ngumi za kulipwa ukihusisha oganaizesheni ya ngumi za kulipwa (TPBO), kamisheni ya ngumi za kulipwa (TPBC) na chama cha ngumi za kulipwa (PST).
3.Hakimiliki wasanii
Hadi Nape anaachana na wizara hiyo, kilio cha wasanii juu ya wizi wa kazi zao ndio kilikuwa, kimeanza kushughulikiwa ambapo waziri huyo wa zamani mara kadhaa aliongoza kampeni ya kukamata watu wanajishughulisha na kazi haramu ya kudurufu nyimbo na video za wasanii wa muziki na filamu.
Hata hivyo Nape hadi anaondoka, vita ya kupigania haki ya kazi za wasanii ilikuwa bado haijamalizika, mzigo anaokutana nao Mwakyembe kwa sasa.
"Wasanii tunaibiwa sana mpaka inakatisha tamaa, kwani tunajikuta tunatumia gharama kubwa kuandaa kazi zetu huku tunachokipata ni kidogo.
Kwa mfano kuna makampuni ya huduma za mawasiliano ambayo yanatumia nyimbo za wasanii kwenye miito ya simu na kuwakata hela wateja wanaotumia. Hata hivyo makampuni hayo hayatengeneza mfumo ambao utamfanya msanii afahamu nyimbo yake imetumika mara ngapi na anatakiwa apate kiasi gani," alisema msanii Diamond katika mahojiano maalum na gazeti hili.
4. Anguko la michezo
Michezo mbalimbali ipo katika hali mbaya nchini huku kukiwa na rekodi ya kutofanya vizuri pindi wanamichezo au timu mbalimbali zinapokwenda kuiwakilisha Tanzania nje ya nchi.
Hata hivyo chini ya Nape, mwanga wa ukombozi wa sekta ya michezo ulianza kuonekana hasa baada ya timu ya taifa ya soka ya vijana wenye umri usiozidi miaka 17 'Serengeti Boys', kufanikiwa kufuzu fainali za mataifa Afrika kwa vijana wenye umri huo zitakazofanyika Gabon huku pia mwanariadha Felix Simbu akishinda mbio za Mumbai Marathon zilizofanyika India.
Pamoja na mafanikio hayo, bado michezo mingine inaonekana imelala jambo linalompa kazi ya ziada Mwakyembe kuifufua.
5. Tiketi za kielektroniki
Miongoni mwa mafanikio ambayo Nape aliyapata ni kuhakikisha utekelezaji wa agizo la matumizi ya mfumo wa tiketi za kielektroniki katika uingiaji kwenye viwanja vya soka nchini.
Tayari Uwanja wa Taifa na ule wa Uhuru, mfumo huo ulishaanza kutumika lakini bado viwanja vilivyobaki, mfumo huo hautumiki, jukumu ambalo ni wazi linapaswa kufanywa na Mwakyembe kwa sasa.
6. Sera ya michezo
Tanzania bado inatumia sera ya zamani ya taifa ya michezo na moja kati ya changamoto ambazo Nape aliahidi kushughulikia ni hiyo.
Ni wazi kuwa Waziri Mwakyembe atakutana na jukumu la kuhakikisha sera ya michezo inabadilishwa kutokana na maagizo yaliyotolewa na waziri mkuu, Kassim Majaliwa pindi alipokutana na viongozi vyama vya michezo, Februari mwaka jana.
"Sera ya michezo imepitwa na wakati kwani ilipitishwa na Bunge mwaka 1967 na kufanyiwa marekebisho mwaka 1971 na sera yake ikachelewa kidogo hadi mwaka 1995 na ilitungwa sheria kabla ya sera.
Naagiza wizara na baraza la michezo shirikisheni wadau, muandae sera itakayokidhi mahitaji ya michezo nchini," aliagiza waziri mkuu katika mkutano huo.
7. Katiba za vyama
Mbali na agizo la sera ya michezo, waziri mkuu pia aliwahi kuagiza wizara hiyo kuhakikisha vyama vya michezo vinarekebisha katiba zao ili kutotoa mwanya kwa viongozi kujilimbikizia madaraka.
"Katiba za vyama vingi vya michezo zinawabeba viongozi waliopo madarakani. Hivyo baraza la michezo linatakiwa kusimamia na kuondoa neno ridhaa na kuwa ya kulipwa," aliagiza Waziri Mkuu.
Hadi waziri Mwakyembe anaapishwa jana, vyama vichache tu vyo vimethubutu kubadili katiba zao huku vingi vikishindwa kufanya hivyo.
8. Vazi la taifa
Mwanzoni wakati alipoteuliwa kwenye nafasi hiyo, Nape aliahidi kuhakikisha kunapatikana vazi la taifa na hadi anaondoka, bado mchakato huo unaendelea ambao ni wazi kuwa Mwakyembe ataurithi.
0 comments:
Post a Comment