Hapana shaka kwamba jina linalovuma nchini kwa sasa ni la Nape Nnauye. Iwe kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na hata vijiweni ndilo linalotajwa sana. Huyu kwa sasa ndiye habari ya mjini.
Jina hilo limepata 'kiki' zaidi juzi baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wake katika nafasi ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mbali na tukio hilo, siku moja kabla Nape alipokea ripoti ya uchunguzi wa kamati aliyoiunda kuchunguza tukio la uvamizi wa studio za Clouds Media Group na kusema kuwa kusimamia ukweli kuna gharama zake.
Na juzi alipozungunza na vyombo vya habari huku akishindana na nguvu za dola zilizokuwa zinamtaka asizungumze, Nape alifafanua kauli yake kuwa sasa analipa gharama za kusimamia ukweli.
Mbali na umaarufu huo wa ghafla kwenye njia zote za upashanaji habari, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema hatua hii inayoambatana na msimamo thabiti wa Nape kuhusu kulipa gharama za kusimamia ukweli ina maana kubwa kwake kisiasa.
Hata Nape mwenyewe anasema ili mbegu iote na kutoa matunda ni lazima ife na kuwa hicho ndicho alichofanya na mbegu yake itastawi.
Inawezekana kuondolewa kwenye nafasi ya uwaziri lisiwe suala la msingi, bali la kujadili wakati huu ni kitu gani kinachomaanishwa na hatua hiyo ya mbunge huyo wa Mtama.
Pengine kila mtu anajiuliza nini hatima ya mbunge huyo kisiasa, kwa nini alikubali yaishe na kwamba hana kinyongo na hiyo inaonyesha taswira gani katika siasa za Tanzania?
Mwanasiasa na waziri wa zamani, Njelu Kasaka anasema nafasi bado ipo ya Nape kufanya kitu kingine kulingana na umri wake na kuwa mtazamo wa watu kwake utazidi kumsafisha na kumng'arisha au kumfubaza, lakini kwa sasa alichofanya kinamkuza.
Anasema mbali ya hayo, pia anakomaa na kutambua anatakiwa kuwa nani kwa sababu gani na anataka kupata nini baada ya kuamua upande anaotaka kuwapo.
Kasaka anasema kilichotokea siyo funzo kwake tu, bali kwa Taifa nzima kila mmoja anatakiwa kutambua na kuelewa kinachoendelea nchini na pia jamii inapaswa ielewe mwelekeo wake na wa nchi kwa ujumla.
Hata hivyo, anasema hakuna mwenye uhakika mabadiliko haya yanatokana na nini, lakini kwa karibu yananasibishwa na uvamizi wa Clouds Media Group, hivyo wateuliwa wajifunze nini kifanyike yanapotokea mambo kama hayo.
"Waliokabidhiwa madaraka wanatakiwa wabaki na somo katika fumbo hili na wajifunze kuwa ikitokea hali kama hiyo wanyamaze kimya, wasichukue hatua, warudi kwa aliyewateua kuuliza wachukue hatua gani," anasema Kasaka.
Mwanasiasa huyo anasema wateule wakipata jibu la maswali yote juu ya hatua wanazotaka kuchukua ndiyo wajue wanatawala kuanzia wapi hadi wapi.
Anasema inawezekana Nape anakwenda kuwa dhahabu inayohitaji kupita kwenye moto ili ikamilike, lakini hata ikipita kwenye moto kabla ya kutengenezwa haiwezi kukamilika, hivyo watu ambao pia ni wafuasi wake ndiyo watengenezaji wa hiyo dhahabu.
Kuhusu wateule kufanya vitu kwa kumridhisha aliyewateua badala ya kutimiza majukumu yao, anasema, "inategemea walipoteuliwa walipewa maelekezo ya wajibu gani, mipaka na madaraka yao hadi wapi, hiyo ndiyo itaamua aina ya utendaji wao," anasema.
Wakati Kasaka akisema hayo, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa anasema ingawa awali hakuwa akizipenda siasa za Nape kwa sababu zilikuwa za chuki, uchonganishi na kukatisha tamaa, baadaye alibadili upepo na kurudi kwenye mstari.
Anasema kinachoendelea hivi sasa hakimgusi Nape na wala si tatizo lake peke yake, bali nchi nzima kwa sababu kuna uvunjivu wa demokrasia, kutosimamia sheria na taratibu kwa makusudi na hali ikiwa hivyo nchi nzima inayumba na kinachotokea sasa ni madhara ya mambo hayo.
Mchungaji Msigwa anasema Nape amejipambanua kutokubaliana na siasa za kupangiwa nini cha kufanya, bali za uwazi na kusimamia haki na kile anachokiamini kuwa ni sahihi katika nafasi aliyoteuliwa.
Anabainisha kwamba kinachomtokea sasa mwanasiasa huyo kijana kinamkumbusha kuwa katika siasa lolote linaweza kutokea na hakuna asiyejua kilichofanywa na Nape, Mwigulu Nchemba na Januari Makamba katika kuhakikisha CCM inasimama. "Matokeo yake ndiyo hayo, somo alilopata ni "wake up call", kuwa wakati waliokuwa wanadhani wanautafuta siyo walioupata, hivyo anapofanya siasa atambue zinabadilika kulingana na watu waliowaweka madarakani," anasema.
Anasema hawezi kufanya siasa safi ya kusimamia haki, kusema kweli, kulinda masilahi ya wasiokuwa na watu wa kuwasemea endapo atakuwa ndani ya CCM na akiyataka hayo atoke huko, vinginevyo hakuna atakachofanya.
"Aendelee kuwa jasiri kama ataweza, akiwa yupo ndani ya CCM, akitaka kuwa jasiri zaidi atoke ndani ya chama kwa sababu anayoonekana kuyakataa ndiyo yanayokubaliwa na wengi.
"Sababu ya kuyakubali ni moja tu, kumfurahisha aliyewateua au anayewaongoza badala ya kuwafurahisha wanaowatumikia na kwa masilahi ya wote," anasema Msigwa.
Akichambua tukio hilo, msomi wa Sayansi ya Siasa, Dk Bashiru Ally wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema suala hilo na mengine mengi yanayotokea kwenye siasa yanahitaji mjadala mpana unaombatana na kuchambua nani ana masilahi na sababu gani kabla ya kuja na jibu la moja kwa moja.
Hata hivyo, anasema yaliyotokea kwa Nape yanamkuza kisiasa na unaweza kuwa mwanzo mwema kwake wa kujifunza kitu kipya, lakini si kipya kwa watangulizi wake kwa sababu wapo wengi waliokutwa na janga kama lililomkuta.
"Bado ana nafasi, ndiyo kwanza huu ni mwaka mmoja wa uongozi na yeye bado ni mbunge arudi jimboni akaendeleze siasa, akiwa ametambua nafasi yake ipo wapi katika nchi na siasa kwa ujumla," anasema.
Anasema kuwa kuna watu waliwahi kujiuzulu siasa kwa madai ya siasa chafu akiwamo Rostam Aziz aliyeliachia Jimbo la Igunga baada ya CCM kutangazwa "vua gamba'.
Anafafanua kuwa kwa Nape bado ni mwanasiasa, anaingia kwenye vikao muhimu, hivyo kinachomtokea sasa ni kuongeza ukomavu kwenye siasa na ikiwezekana kujipanga upya kwa uimara zaidi.
"Hatakuwa wa kwanza kuenguliwa kwenye nafasi ya uwaziri, wapo wengi atakwenda kukutana nao huko ambao walikuwa kwenye nyadhifa kubwa na wakijiamini, lakini waliowateua walipoamua walitengua uteuzi wao kwa sababu moja ama nyingine," anasema. "Sidhani kama kukosa uwaziri ni kukosa sifa ya kuwa kiongozi tena wa kuchaguliwa, amekaa muda mfupi katika uongozi, lakini alikuwa anafanya vizuri. Ni miongoni mwa mawaziri walioonyesha kuimudu vyema nafasi waliyoteuliwa, sioni kama atapoteza mwelekeo, zaidi atakuwa imara," anasema.
Dk Ali anashauri kuwa hali hiyo isimkatishe tamaa kwa sababu wapo mawaziri waliofanya vyema kwenye awamu zilizopita, lakini awamu hii wapo kando na bado wanafanya siasa safi kwa kiwango kilekile.
Anasema hakuna aliyetarajia kama Anne Kilango Malecela angeteuliwa tena kuwa mbunge, hivyo siasa zinabadilika lakini kwake achukulie hatua hiyo ni ukomavu kuelekea kwenye mapambano kamili ya kisiasa, licha ya kuwa ni mwanasiasa mzoefu.
Kilichomtokea
Alhamisi asubuhi Rais John Magufuli alitangaza mabadiliko madogo kwenye baraza la mawaziri na kumuweka kando Waziri wake wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.
Mabadiliko hayo yalifanya Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria huku aliyekuwa wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe akihamishiwa Wizara ya Habari iliyokuwa chini ya Nape.
Baada ya kuyatangaza, Nape aliyekuwa Arusha kwa shughuli za kikazi alitangaza kupitia mtandao wa Twitter mkutano wa wanahabari jijini Dar es Salaam lakini muda mfupi kabla ya kufanyika ukazuiwa na polisi kufanyika hotelini.
Hata hivyo, aliamua kuufanyia nje ya Hoteli ya Protea huku akikabiliana na askari kanzu waliomtishia kwa bastola. Inaaminika Nape aliingia kwenye mvutano na bosi wake baada ya kuunda kamati ya uchunguzi wa uvamizi wa Clouds Media Group uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, lakini Rais Magufuli alimtaka kiongozi huo wa mkoa aendelee kuchapa kazi.
0 comments:
Post a Comment