By Cledo Michael na Taus Ally
mwananchipapers@mwananchi.co.tz
Dar es
Salaam. Wakati Mwenyekiti wa Kampuni ya Quality Group, Yusuf Manji akipata
matibabu chini ya ulinzi wa polisi katika Hospitali ya Aga Khan, Meneja Mradi
wa kampuni hiyo na katibu wake jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu.
Washtakiwa
hao, Jose Kiran (Meneja Mradi) na Prakash Bhatt (Katibu), walipandishwa
kizimbani wakikabiliwa na shtaka la kukiuka amri ya ofisa wa uhamiaji na
kujaribu kutoroka.
Walisomewa
mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cpyrian Mkeha.
Mwendesha
Mashtaka wa Uhamiaji, Method Kagoma akiwasomea mashtaka, alidai kuwa Februari
20, washtakiwa wakiwa ni raia wa India na waajiriwa wa Quality Group Ltd,
walimzuia ofisa wa uhamiaji kufanya kazi zake.
Alidai
kuwa, watuhumiwa walikataa kuripoti katika ofisi za uhamiaji zilizopo jijini
Dar es Salaam na kujaribu kutoroka nchini kupitia Mpaka wa Horohoro.
Washtakiwa
walikana kutenda kosa hilo na wako nje kwa dhamana baada ya kukamilisha
masharti yaliyomtaka kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja ambaye alisaini bondi ya
Sh5 milioni. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 7, kwa ajili ya usikilizwaji wa
awali pamoja na kuunganishwa na kesi ya washtakiwa wenzao 14.
Wakati huo
huo; Mfanyabiashara Manji anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga
Khan.
Awali
Manji alilazwa katika Taaasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Muhimbili,
alikofikishwa baada ya hali yake kudhoofika alipokuwa ameshikiliwa katika Kituo
Kikuu cha Polisi kwa tuhuma zilizohusu matumizi ya dawa za kulevya.
Mwandishi
wa gazeti hili alifika hospitalini hapo jana saa 4:12 asubuhi ili kujua hali ya
mfanyabiashara huyo.
Alimshuhudia
Manji akiwa hospitalini hapo huku polisi mmoja akiwa eneo hilo.
Baada ya
kufika mapokezi, mwandishi alimueleza mhudumu wa zamu kuwa alifika kutaka kujua
hali ya Manji, lakini alimjibu kuwa hafahamu chochote na badala yake alimtaka
aende kwa askari wa ulinzi ili ampe maelekezo. Hata hivyo, askari huyo alitoa
maelekezo kuwa amuone mtu mwingine aliyekuwa jirani yake akiwa kavalia suti,
kuwa ndiye mwenye majibu ya maswali yake.
Hata
hivyo, kabla ya kumfikia mtu huyo, askari huyo alimuita tena mwandishi na
kumtaka akazungumze na daktari anayemtibu Manji. Kabla ya mwandishi hajaanza
safari ya kwenda kumuona daktari huyo, Manji alifika mapokezi akitokea wodini
na kumtaka muuguzi amtolea nakala ya karatasi aliyokuwa ameishika mkononi.
Kabla muuguzi hajafanya hivyo, alifika mwanaume mmoja mweusi na alimtaka Manji
arejee wodini.
Msemaji wa
hospitali hiyo, Olayce Lotha alipoulizwa kuhusu hali ya Manji, alisema
mfanyabiashara huyo ametaka uongozi wa hospitali kutotoa taarifa zake kwa
vyombo vya habari au mtu yeyote nje ya familia yake.
0 comments:
Post a Comment