Social

Wednesday, March 1, 2017

Kampuni za viroba nchini zaanza kulia hasara



Dar es Salaam. Siku moja kabla ya kuanza utekelezaji wa katazo la pombe kali ndani ya vifungashio vya plastiki maarufu viroba, Kampuni ya Perfect Printers Ltd, inayohusika na usambazaji wa vifungashio hivyo imeeleza kupata hasara ya Dola za Marekani 65,000 sawa na Sh140 milioni.
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Perfect Lyimo akizungumza na gazeti hili jana alisema hasara hiyo inatokana na tani 100 zilizotengenezwa na kulipiwa ambazo ni oda ya kampuni inayozalisha vinywaji aina ya pombe kali.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa Februari 18, na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipohutubia wakazi wa Mji Mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, akisema biashara hiyo ukomo wake utakuwa Machi Mosi.
Katika ufafanuzi wake, Majaliwa alisema tayari wamekaa na wenye viwanda na kukubaliana wanaotengeza pombe hizo waziweke kwenye ukubwa unaokubalika.
Hata hivyo, Lyimo aliliambia gazeti hili jana kuwa tani hizo zinatokea Durban, Afrika Kusini ambako zinazalishwa. “Kwanza kuna tani 25 ambazo zinatakiwa kufika Dar es Salaam Machi 6, kutokea Afrika Kusini. Mzigo mwingine ni kontena la tani 25 tunategemea ndani ya wiki tatu zijazo utaletwa,” alisema na kuongeza:
“Pamoja na mzigo huo, pia kuna tani 50 ambazo zimeshatengenezwa na tumeshalipia tayari, zote tumeshalipia dola 65,000 hizo ni gharama za ununuzi na usafirishaji tu nje ya kodi na tozo za upakuaji na upakiaji wa mzigo bandarini.”
Lyimo alisema hakuna namna yoyote ya kuokoa hasara hiyo hadi sasa, kwani huandaa vifungashio kulingana na oda ya kampuni inayozalisha ‘viroba’. Alisema pamoja na hasara hiyo, Serikali itakosa VAT na tozo nyingine za upakuaji bandarini. Alifafanua akisema kampuni iliyowaagiza mzigo huo haitaweza kupokea tena kutokana na katazo hilo la Serikali na hakuna mbadala wa matumizi ya vifungashio hivyo ili kuokoa hasara itakayotokea.
Mkurugenzi wa Sera na Ushawishi wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), Hussein Kamote akizungumza na gazeti hili alisema Serikali ilitakiwa kuanza na utoaji adhabu kwa wafanyabiashara wanaouza viroba hivyo kama njugu mtaani kwa kuwa ni kinyume cha sheria.


Alisema taratibu zinaeleza viroba hivyo vinatakiwa kuuzwa katika maduka na maeneo maalumu ya starehe yenye leseni.

0 comments:

Post a Comment