By Julius Mnganga, Mwananchi
jmathias@mwananchi.co.tz
Dar es
Salaam. Ongezeko la mikopo isiyolipika na kupungua kwa faida kwa takriban Sh50
bilioni mwaka 2016, kunaiweka njiapanda Benki ya CRDB na inabidi hatua za
haraka zichukuliwe kurekebisha mwenendo.
Faida ya
benki hiyo kubwa nchini imepungua na kuhitimisha dalili zilizojitokeza kwenye
robo ya tatu ya mwaka 2016 ilipotangaza kupata hasara ya takribani Sh2 bilioni.
Faida ya CRDB imeshuka kutoka Sh122.3 bilioni iliyopatikana mwaka 2015 mpaka
Sh73.4 bilioni mwaka jana na kuwa miongoni mwa benki ambazo hazikufanya vizuri
katika kipindi hicho.
Kupungua
kwa faida ambayo kwa miaka mitano iliyopita imekuwa ikiongezeka, kunaweza kuwa
kumesababishwa na mambo kadhaa ambayo yanaonyesha ugumu ambao taasisi hiyo
kubwa nchini ilikumbana nao kwa mwaka 2016.
Mikopo
zaidi ya kiwango cha amana
Ripoti ya
mwaka ya hesabu za fedha za benki hiyo inaonyesha uwezekano wa kusitishwa kwa
utoaji wa mikopo ili kuweka mambo sawa baada ya kuzidi ukomo uliopo kwa mujibu
wa kanuni za Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Miongoni
mwa vipengele vilivyokiukwa ni kifungu cha 7 cha Kanuni za Benki na Taasisi za
Fedha za mwaka 2014 kinachozitaka kutokopesha zaidi ya asilimia 80 ya amana
walizonazo.
Mpaka
mwisho wa mwaka, CRDB ilikuwa imefikisha asilimia 84, jambo linalomaanisha kuwa
haitaendelea kutoa mikopo mpaka itakapofanya mabadiliko na kurekebisha kasoro
hiyo.
Hiyo ni
muhimu kwa sababu, kwa mujibu wa wataalamu, shughuli kubwa ya benki yoyote ya
biashara, ni mikopo ambayo imetengenezewa kanuni na taratibu ambazo ni lazima
zifuatwe.
Kuonyesha
inachukua hatua, katika robo ya mwisho wa mwaka, kiasi cha mikopo kilichotolewa
na benki hiyo kilipungua kwa Sh84 bilioni ingawa amana za wateja hazikubadilika
ndani ya kipindi hicho, tofauti na ilivyokuwa katika robo ya tatu ya mwaka
wakati amana hizo zilipoongezeka kwa asilimia moja.
Kwenye
robo ya nne ya mwaka, benki hiyo ilikuwa imetoa mikopo yenye jumla ya Sh3.234
trilioni, ikilinganishwa na Sh3.318 trilioni ya robo iliyoishia Septemba.
Ripoti ya
kundi la benki hiyo yenye matawi nje ya nchi, inaonyesha mikopo yake imekuwa
ikiongezeka kila mwaka. Katika taarifa yake ya mwaka 2015, mikopo iliongezeka
na kufikia Sh3.34 trilioni kutoka Sh2.576 trilioni iliyokuwapo mwaka 2014
wakati kwa robo ya mwisho ya mwaka 2016 kundi lilitoa jumla ya mikopo ya Sh3.27
trilioni ikipungua kutoka Sh3.361 iliyokuwapo katika robo ya tatu.
Mikopo isiyolipika
Tatizo
jingine ni mikopo isiyolipika. Hadi Desemba 2016, CRDB ilikuwa na mikopo
isiyolipika kiasi cha Sh111.4 bilioni kikiwa kimeongezeka kwa takriban mara
mbili ndani ya robo ya mwisho, kutoka Sh66.7 bilioni iliyokuwapo katika robo
iliyoishia Septemba 2016.
Kiwango
hicho ni sawa na asilimia 13 ya mikopo iliyotolewa, hivyo kuifanya kuvunja
kanuni nyingine ya BoT inayotaka kiasi hicho kisizidi asilimia tano ya mikopo
yote. Mikopo hiyo kwa kundi ilikuwa asilimia 11 ambazo, kama ilivyo kwa
asilimia 13 za benki, iliendelea kutobadilika kati ya robo ya tatu na ya nne.
Kamisheni
zashuka
Hesabu za
mwaka za CRDB zinabainisha kupungua kwa mapato yatokanayo na biashara ya
kimataifa (fees and commissions) ambayo huiwezesha benki kupata kamisheni
kutokana malipo yanayofanywa baina ya mteja na muuzaji.
Mapato
hayo yalipungua kutoka Sh47.741 bilioni Septemba mpaka Sh43.059 bilioni kwa
Desemba. Hata mapato ya kundi yalishuka pia kutoka Sh50 bilioni mpaka Sh42.734
bilioni ndani ya kipindi hicho.
Amana
zaongezeka
Kutoka
robo ya tatu kwenda ya nne mwaka 2016, amana za wateja wa CRDB ziliongezeka.
Taarifa inaonyesha amana hizo zilifikia Sh3.996 trilioni Desemba kutoka Sh3.98
trilioni, likiwa ni ongezeko la Sh16 bilioni ndani ya kipindi hicho.
Licha ya
amana za wateja kuongezeka kwa kiasi hicho, ukuaji wa amana zote (deposit
growth) ulishuka kutoka asilimia moja iliyokuwapo katika robo ya tatu mpaka
sifuri hadi kufikia Desemba.
Amana za
wateja kwa kundi ziliongezeka kwa Sh12 bilioni zikitoka Sh4.063 trilioni mpaka
Sh4.051 trilioni ndani ya kipindi hicho, ingawa ukuaji wa amana zote uliendelea
kubaki asilimia moja ndani ya muda huo.
Katika
ripoti yake ya mwaka 2015, CRDB iliainisha vihatarishi vitano vya biashara
ambavyo inakabiliana navyo. Vihatarishi hivyo ni mikopo, kiwango cha fedha
kinachohitajika kukidhi mahitaji ya uendeshaji na hatari zinazosababishwa na
riba na viwango vya kubadilisha fedha.
Vihatarishi
vingine vilikuwa katika kufuata taratibu au uratibu katika uendeshaji na vya
kimkakati. Ripoti hiyo ilibainisha amana za wateja kuwa ndicho chanzo kikubwa
cha mapato ya taasisi hiyo.
Matawi
yaongezeka
Pamoja na
hali ngumu iliyojitokeza katika maeneo kadhaa, benki hiyo ilijiimarisha kwa
kuongeza idadi ya matawi na kuajiri wafanyakazi wapya ili kuhudumia wateja wake
kwa viwango bora.
Kwa mwaka
mzima, benki iliongeza matawi sita kote nchini na kufikisha matawi 180.
Ongezeko hilo lilienda sambamba na idadi ya wafanyakazi ambao jumla yao
ilifikia watu 2,760 kutoka 2,377 waliokuwapo mwaka juzi ikimaanisha kwamba
wafanyakazi wapya 383 waliajiriwa.
Kutokana
na ongezeko la wafanyakazi hao, jumla ya mishahara (salaries and benefits)
ilipanda kutoka Sh139.526 bilioni mwaka 2016 mpaka Sh165.015 bilioni mwaka jana
sawa na ongezeko la Sh25.489 bilioni kwa mwaka huo.
Kundi
liliongeza wafanyakazi 545 kutoka 2,651 waliokuwapo mwaka 2015 mpaka 3,196
mwaka jana baada ya matawi yake pia kuongezeka kutoka 199 mpaka 250 ndani ya
kipindi hicho huku mishahara ya watumishi hao ikipanda kutoka Sh152.796 bilioni
mpaka Sh184.554 bilioni sawa na ongezeko la Sh31.758 bilioni kwa mwaka 2016.
Jitihada
za kuwapata watendaji wa CRDB ili kueleza kuhusu ripoti ya benki hiyo ya mwaka
hazikuzaa matunda. Licha ya kumpata Mkurugenzi wa Uhusiano wa benki hiyo, Tuli
Mwambapa ambaye alitaka atumiwe maswali kwa baruapepe, hakuyajibu.
Hata
mwandishi wetu alipofuatilia na kukutana na meneja uhusiano wake, Godwin
Semunyu ambaye aliomba apewe wiki moja ya kutafuta majibu hayo, hakutekeleza
ahadi yake pia.
Mkurugenzi
wa Usimamizi wa Benki Kuu, Kennedy Nyoni alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi wa
hatua zinazochukuliwa kwa benki zinazokiuka kanuni zilizoweka, alijibu kwa
jumla, “BoT inaweza ikaitaka benki husika kuwasilisha mpango wa kurekebisha
hali hiyo baada ya kujua sababu zilizochangia au kuwataka wamiliki kuongeza mtaji
kufidia kama kuna hasara.”
Wachambuzi
Wakizungumza
na mwandishi wetu, wachambuzi wa masuala ya kibenki walikuwa na maoni tofauti.
Mtaalamu
na mchambuzi wa masuala ya fedha, Reginald Baynit alisema kampuni za simu
zimechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa amana za wateja wa benki za biashara
nchini.
“Wananchi
wengi wanatumia zaidi mitandao ya simu licha ya gharama kubwa zilizopo kutokana
na urahisi wa huduma uliopo,” alisema Baynit.
“Kinachotakiwa
ni ubunifu wa kukabiliana na ushindani uliopo. Mawakala wa benki hizo waliopo
mtaani watasaidia lakini jitihada zaidi zinahitajika,” aliongeza.
Meneja
mmoja wa taasisi ya kimataifa ya ukaguzi wa fedha ambaye hakupenda kutajwa
gazetini, alisema mapato ya benki yanatokana zaidi na riba itokanayo na mikopo
ambayo hata hivyo, lazima itolewe kwa umakini.
“Benki
yenye kiasi kikubwa cha mikopo isiyolipika inajiweka katika hatari ya
kufilisika. Hii ndiyo iliyoifikisha Twiga (Bancorp) ilipo,” alisema na kufafanua
kwamba mikopo hiyo ni mingi nchini.
“Tusipokuwa
makini, mikopo hii itaziangamiza benki nyingi nchini,” alisema.
Kutokana
na kuelemewa na mikopo isiyolipika, miongoni mwa sababu nyingi, mwaka jana,
Benki ya Twiga Bancorp ilishindwa kujiendesha hivyo kuwekwa chini ya uangalizi
wa BoT ambayo inatafuta mdau mwenye uwezo wa kuisimamia ili iendelee kutoa
huduma.
Kuhusu
kuongezeka kwa wafanyabiashara wanaoshindwa kurejesha mikopo yao hivyo kuathiri
ufanisi wa benki za biashara, alisema kunatokana na Serikali kuchelewa kuwalipa
wazabuni wake.
0 comments:
Post a Comment