By Herieth Makwetta, Mwananchi hmakweta@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Wasanii wa
muziki wa kizazi kipya na wale wa Bongo Movie, wameonywa kwamba kujiingiza kwao
kwenye siasa kunaweza kuwa chanzo cha kudidimiza vipaji vyao na kutoweka katika
ulimwengu wa sanaa.
Gazeti hili lilifanya uchunguzi
kuhusiana na taarifa za siasa kuwamaliza wasanii ambapo wadau mbalimbali
walitoa maoni yao, akiwamo waziri mwenye dhamana na wasanii, Nape Nnauye na
mwanamuziki mkongwe nchini, John Kitime
Taarifa zilizozagaa ni kwamba wasanii
wengi waliovuma miaka ya nyuma, kwa sasa wametoweka baada ya kushiriki kampeni
za kisiasa za Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Uchaguzi huo uliokuwa na joto kali la
kisiasa kutokana na nguvu waliyokuwa nayo wagombea wawili, John Magufuli wa CCM
na Edward Lowassa aliyesimamishwa na Ukawa kupitia Chadema, ulionekana
kuyumbisha wasanii wengi.
Mfano, katika uchaguzi huo wasanii
wengi walishiriki kupigia kampeni wagombea urais, kuna waliokuwa CCM na wengine
Ukawa. Na baada ya hapo wengi wametoweka katika ulimwengu wa sanaa.
Kitime ambaye pia ni mchambuzi wa
masuala ya sanaa, alisema kutokana na uchanga wa demokrasia, msanii
anaposhabikia chama fulani wakati mashabiki wake wana mrengo tofauti unajengeka
uadui na kupoteza mashabiki.
“Hasara zilizopo kwa msanii ni kupoteza
mashabiki kwa kuwa demokrasia yetu bado haijakua, lakini pia anaweza kupoteza
mwelekeo ikiwa chama alichokishabikia hakitashika dola huenda ikamwathiri pia
kwa kukosa fursa nyingi na kuwekwa pembeni katika kila shughuli,” alisema
Kitime.
Alisema hata hivyo kizazi cha sasa
kimekuwa huru kujipambanua ukilinganisha na enzi zao.
Kitime aliweka wazi kwamba huenda hiyo
ndiyo sababu ya wanamuziki wakongwe kushindwa kujihusisha na masuala ya kisiasa
kwa sasa.
Alisema licha ya wasanii wengi
kujipambanua pia walio wengi wanaangalia zaidi faida zitokanazo na masuala ya
kampeni za kisiasa pasipo kung’amua hasara zake baadaye.
Kitime alisema miaka ya 1970 hadi 1980
wasanii walio wengi ilikuwa lazima wawe na kadi za chama cha TANU na ilikuwa
kama kitambulisho cha uraia.
Kadi ya chama ilitumika msanii
alipotaka nafasi ya kusafiri nje ya nchi au hata kuitumia kufungua akaunti
benki, kibali cha shoo pia ilikuwa ni kadi ya chama.
“Kwetu ilikuwa ni kama kitambulisho,
kwa maana hakukuwa na chaguo la ziada, ilitulazimu kuwa huko na tulitumbuiza
kwa kuwa wananchi wote walikuwa katika chama kimoja. Hakuna mtu ambaye alikuwa
anazifikiria hasara za upande wa pili, tulishiriki katika masuala ya Mwenge wa
Uhuru, sherehe mbalimbali za kitaifa yaani kadi ilituwezesha hivi vyote,”
alisema Kitime.
Kitime alisema wasiwasi wake unakuja
kwa kile alichokiita demokrasia na siasa za vyama vingi ambapo alisema vyama
vinawatumia wasanii kujinufaisha.
Uchaguzi wa mwaka 2015 wapo waigizaji
walioamua kudhihirisha kuwa wanashabikia chama fulani kwa mfano Jackline
Wolper, Aunty Ezekiel, Shamsa Ford walitangaza kuwa wanashabikia Chadema wakati
wasanii Batuli, Wastara Juma, Jenifer Kyaka ‘Odama’ Wema Sepetu, Steve Nyerere,
JB na wengine waliishabikia CCM.
Hata hivyo, baadaye Wolper na wenzake
waliokuwa Chadema kipindi hicho hicho cha uchaguzi walitangaza kujiunga CCM
wakidai walipotea njia.
Juni 2015 Mrembo wa Taji la Miss Tanzania
mwaka 2006, Wema Sepetu alitangaza rasmi nia ya kuwania ubunge wa viti maalum
mkoa wa Singida kwa tiketi ya CCM.
Wema aliyedai kuwa yeye ni mwana CCM
tangu mwaka 2010, hivi karibuni alitangaza kuhamia Chadema Februari 24 mwaka
huu. Tangu aanze harakati hizo za siasa Wema hajatoa filamu mpya.
Hata hivyo, Meneja wa Yamoto Band, Said
Fella alisema ushiriki wa kundi hilo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 si
sababu ya kuporomoka kisanii.
“Kwetu siasa ina nafasi yake na muziki
hali kadhalika, ndiyo maana waliposhiriki kwenye kampeni meneja wao alikuwa
Chambuso, sikusimama mimi na vivyo hivyo kwa sasa bado wapo na wanafanya muziki
kama kawaida,” alisema Fella.
Mwimbaji wa muziki wa Zouk nchini,
Mwasiti Almas alisema alishiriki katika siasa kwa vipindi viwili tofauti,
lakini alijitahidi kuwa mtumbuizaji zaidi kuliko kujipambanua anashabikia chama
gani na hicho ndicho walio wengi wanakikosea.
“Unapokuwa msanii fanya sanaa na achana
na siasa, haya mambo mawili hayachangamani kwa kuwa mashabiki wako ni wa pande
zote, ukijitangaza unashabikia wapi umeumia,” alisema Mwasiti.
Kuhusiana na hilo, Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alisema hoja kwamba wasanii kuingia
kwenye siasa kunawapoteza inahitaji upembuzi wa kina.
Alisema kuna mambo mengi yanaweza
kuchangia, lakini alitoa mfano wa soko la filamu kwa kuwataka wazalishaji
kueleza namna soko lilivyoshuka.
Nape alisema badala ya kwenda na kauli
za jumla ni vema kuwa na takwimu ambazo zinaelezea awali waliuza nakala ngapi
kwa filamu moja na sasa wanauza ngapi.
Hata hivyo, alisema amekuwa akifuatilia
soko la filamu za ndani ya nchi kwa ukaribu tangu amekuwa waziri wa wizara
hiyo, hivyo kuwabana zaidi wezi wa kazi zao kulifanya soko hilo kuyumba.
“Mmeshuhudia nafanya oparesheni
mitaani, najua kilichoshusha kazi za wasanii wa ndani ni piracy ‘wizi wa kazi
za wasanii’, kazi za sanaa zilizopo mtaani ambazo hazijalipiwa kodi ndizo
zimeshusha mauzo ya kazi za wasanii, hili ndilo suala la msingi, haya mengine
ni hisia za watu ambao mimi nisingependa nilizungumzie,” alisema Nape.
Rapa msomi kutoka Kundi la Weusi,
Nickson Simon maarufu ‘Nikki wa Pili’ alisema wanasiasa ndiyo ambao huwatumia
wasanii na siyo siasa.
Alisema kwa sasa wanasiasa kuwatumia
wasanii ni jitihada zilizofilisika kwa maana siasa inatakiwa kubebwa na mambo
ya kijamii, mwanasiasa anatakiwa kuongea kuhusiana na mambo yanayoifika jamii
na namna ya kukabiliana nayo.
“Mwanasiasa unapoamua kuwatumia wasanii
maana yake unataka kutumia propaganda, hizo ni siasa zisizo bora kwani unaanza
kutegemea wasanii badala ya fikra, uchambuzi, dhana,” alisema.
Alisema hiyo huleta migongano kwa maana
wanasiasa haohao baadaye huanza kuhoji maadili ya kazi za wasanii, lakini
kipindi cha uchaguzi wapo ambao walikuwa wanalipwa waimbe nyimbo ambazo hazifai
kwa jamii.
“Mwanasiasa anapomtumia msanii hajali
maadili yake anachoangalia ni idadi ya wafuasi wa msanii. Ukubwa wa msanii
ndiyo mtaji kwa mwanasiasa huyo wakati wa kampeni,” alisema.
Nikki wa Pili alisema hiyo ndiyo sababu
hata filamu zao hukosa maadili.
0 comments:
Post a Comment