Hospitali ya Aga Khan imeanza kutumia teknolojia mpya ya matibabu ya uondoaji wa vivimbe na uvimbe mkubwa katika mlango wa kizazi 'fibroids'.
Kwa teknolojia hiyo, mgonjwa aliyefanyiwa aina hiyo ya matibabu anaweza kupumzika kwa saa 48 na baada ya hapo kuendelea na majukumu yake mengine kama kawaida.
Madaktari bingwa wa hospitali hiyo kwa kushirikiana na daktari bingwa na mtaalamu wa mionzi kutoka Uingereza, Dk Nigel Hacking, juzi walifanya upasuaji huo kwa wanawake tisa waliokuwa na tatizo la uvimbe lijulikanalo 'uterine fibroids' kupitia utabibu mpya wa kiteknolojia wa Uterine Fibroids Embolization (UFE).
UFE ni upasuaji mpya au tiba mbadala ya kuondoa uvimbe katika nyumba ya uzazi na tiba hii si upasuaji, bali wataalamu hutumia kamera ya X-Ray kupitisha na kupeleka dawa kwenye nyumba ya uzazi palipo na uvimbe kwa kutumia mirija ya kusafirishia damu.
Dawa hiyo huzuia mishipa ya damu inayopeleka virutubisho kwenye uvimbe na kuvifanya vivimbe visinyae na kuondoka kabisa. Tiba hiyo ambayo hufanyika kwa saa moja, haihitaji upasuaji mkubwa kama ilivyo kwa upasuaji wa kawaida wa uvimbe.
Hii ni mara ya kwanza kwa tiba hiyo kufanyika nchini na kwa Afrika Mashariki, ni Kenya pekee ambayo hutoa huduma hiyo.
0 comments:
Post a Comment