MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Taifa (UWT) wa Chama cha Mapinduzi, Sophia Simba amesema hatagombea nafasi hiyo katika uchaguzi utakaofanyika mwaka huu.
Simba ametoa msimamo huo jana alipokuwa akizungumza na wanawake wa Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam ikiwa ni wiki ya kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8, kila mwaka.
Alieleza sababu zinazomfanya kutogombea tena kuwa ni tangu alipofanikiwa kupata nafasi hiyo mwaka 2007, ilikuwa ni azma yake kuitumikia jumuiya hiyo kwa vipindi viwili tu na si zaidi ya hapo.
Amesisitiza kuwa wote waliokaribu naye wanalitambua hilo. Pia amesema ataachia kiti baadaye mwaka huu baada ya kuitumikia jumuiya hiyo kwa mapenzi, utii, uaminifu na uadilifu mkubwa kwa kipindi cha kutosha, ndiyo maana anaona ipo haja apumzike na kuwaachia wanawake wenzake waendeleze pale alipoachia.
"Nitakikabidhi kijiti hiki kwa uongozi utakaochaguliwa, kama ilivyo mila na desturi za chama chetu. Sina shaka kabisa wapo wanawake wengine wenye uwezo wa kuendeleza harakati za kuwaunganisha wanawake katika kupigania maslahi na haki zao za msingi, haki na ustawi wa watoto na masuala ya jamii kwa ujumla.
"Likiwemo jukumu kubwa la kisiasa na la kipaumbele ndani ya jumuiya ya UWT, ambalo ni kuhakikisha kuwa chama chetu cha Mapinduzi kinaendelea kushika dola," alisema Simba.
Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa ameamua kuwatangazia mapema ili kuwaweka huru na kuwapa muda wa kujipanga vizuri wale wote wanaokusudia kugombea nafasi hiyo kubwa ndani ya jumuiya na pia kutoa majibu kwa wale waliokuwa wakimuuliza na kumhamasisha aendelee kugombea.
Simba ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu , Halmashauri Kuu ya CCM na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, awali alisema ana imani kwamba wanawake wa umoja huo watajitokeza kwa wingi katika kushiriki kikamilifu kuchagua na kuchaguliwa kupitia jumuiya na nafasi za uongozi ndani ya chama hicho.
Mwaka huu ni wa uchaguzi ndani ya chama hicho na jumuiya zake.
0 comments:
Post a Comment