Social

Thursday, March 16, 2017

Vita dhidi ya viroba haikuwatendea haki wafanyabiashara, wawekezaji

By Prof Honest Ngowi
Uamuzi wa Serikali kupiga marufuku iliyokuwa biashara halali ya pombe za viroba, umezua tafakuri kubwa kwa wadau wa uchumi.
Mjadala umekuwa mkubwa zaidi baada ya taarifa ya mfanyabiashara mkoani Dodoma kudaiwa kujiua baada ya kukamatwa akiwa na shehena ya pombe hii. Maelekezo mapya ni kwamba pombe hii sasa inapaswa kuuzwa katika vifungashio vyenye ukubwa ‘unaokubalika’.
Utekelezaji
Nia ya Serikali ambayo ni kuzuia matumizi ya kinywaji hiki kwa sababu ya ujazo wake mdogo ni njema, inapaswa kuungwa mkono. Inadaiwa kuwa, wapo watu wengi hasa vijana na wanafunzi wanaotumia pombe hii kiasi cha kulewa kupindukia na kuathiri nguvukazi ya taifa.
Madhara ya afya kutokana na ulevi huongeza gharama za matibabu kwa taifa. Pamoja na nia hii njema, uchambuzi wa kiuchumi na biashara ni muhimu ili kuboresha utekelezaji wa katazo hili na mengine yanayoweza kufanana na hili kwa sasa na siku zijazo.
Mali ghalani na katika mzunguko
Wachambuzi wenye jicho la kisheria kama Onesmo Ole Ngurumwa watakubaliana na mtizamo wa kiuchumi na biashara kuwa, katika kupiga marufuku biashara yoyote ambayo ilikuwa ni halali kuna vitu vya kuzingatia.
Makala haya yanaakisi kwa kiwango kikubwa uchambuzi wa Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Ole Ngurumwa. Ili kuepuka madhara ya kiuchumi ni busara kuhakikisha bidhaa zilizopo ghalani na kwenye mzunguko kihalali haziathiriki na katazo husika.
Hii ni kwa sababu sheria haipaswi kufanya kazi kinyume. Katika muktadha wa viroba, katazo linapaswa kutumika na kuwa halali kwa bidhaa zitakazozalishwa na kuingizwa katika mzunguko baada ya katazo tajwa.
Kama kuna utengenezaji na uagizaji halali ulikwishafanyika kabla ya marufuku na bidhaa zipo njiani au kwenye mzunguko, ni busara biashara na miamala ile ikamilike kabla utekelezaji wa sheria mpya haujaanza.
Siyo afya kiuchumi na kibiashara kukamata shehena zilizokuwapo katika mzunguko kabla ya katazo. Pamoja na mambo mengine, wahusika wa shehena hizi halali wanaweza kuwa wamekopa kutoka vyanzo mbalimbali na kulipa kodi, ushuru na tozo mbalimbali za Serikali.
Muda wa mpito
Umuhimu wa kuwa na muda wa mpito baada ya uamuzi kutolewa na utekelezaji wake umeandikwa na kuzungumzwa mara kadhaa. Kwenye ukurasa huu, niliwahi kuandika na kuzungumzia umuhimu huu kulipotolewa tamko la kusitisha luninga mtandao.
Pia, niliandika muktadha wa utekelezaji wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) ya mwaka 2014. Pamoja na mambo mengine, uamuzi wa kisheria, kisera na kiudhibiti lazima uwe na jicho la kibiashara na kiuchumi ikiwamo kutoa kipindi cha mpito cha kutosha ili kutowavuruga waliokuwa wanafuata taratibu zilizokuwapo awali.
Hiki ni kipindi ambacho wadau wanapata muda wa kujipanga kutekeleza matakwa mapya. Katika muktadha wa viroba, ni muda wa kutosha kusimamisha uzalishaji wake, kumaliza usambazaji wa kilichokwishazalishwa na kumaliza utumiaji wa mali iliyopo sokoni.
Misingi ya kiuchumi na kibiashara ya hoja hii, ni kutambua kuwa kuna mitaji iliyokopwa na kuwekezwa katika mnyororo wa thamani katika bidhaa inayokatazwa baada ya kuridhika na tathmini iliyofanywa.
Ushirikishaji
Katika zuio la viroba kuna umuhimu wa kufikia uamuzi kwa mbinu shirikishi. Ushirikiswaji sahihi kuhusu kipindi mpito kwa mfano ni muhimu sana. Ungesaidia, pamoja na mambo mengine, kubaini muda ambao una uhalisia ili kutoumiza upande wowote.
Ili kuepuka madhara ya kiuchumi na kibiashara, ingekuwa vyema muda huu ukaafikiwa na wadau wote na siyo upande mmoja. Wadau hawa lazima wawe wawakilishi mahiri wa wadau wote na ikibidi kuwapo wasuluhishi wasiofungamana na upande wowote.
Pamoja na mambo mengine, lazima kufanya uchambuzi na upembuzi yakinifu wa wadau. Ni vizuri kuwatambua waathirika wa kwanza, uzoefu wao katika jambo husika, nguvu zao na jinsi watakavyoathirika na katazo husika.
Uchambuzi wa haraka utaonyesha wadau wa viroba ni pamoja na taasisi za fedha, wazalishaji, wasambazaji, wahifadhi, wauzaji na wanywaji. Wengine ni mamlaka za mapato.
Ukubwa wa vifungashio
Katika kupiga marufuku viroba ni muhimu pia kufahamu misingi ya kiuchumi na kibiashara ya kuwa na ukubwa tofauti wa vifungashio vya bidhaa mbalimbali. Ikumbukwe, kinachokatazwa siyo kilichomo ndani mbali na ukubwa wa vifungashio.
Kiuchumi na kibiashara ukubwa wa kifungashio hutegemea mambo mengi, yakiwamo tabia za wateja. Wapo wanaotaka ujazo mdogo sana, mdogo, wa kati au mkubwa na mkubwa zaidi.
Sababu ya uchaguzi huo ni uwezo wa kiuchumi na vionjo vya moyo. Kwa wenye vipato vya chini kwa mfano, huweza kununua bidhaa za ujazo mdogo zaidi. Kukataza ujazo huu kunaweza kuwafanya washindwe kutumia bidhaa husika.
Vifungashio kwingineko
Suala la ujazo mdogo wa viroba kukidhi mahitaji ya wateja wenye kipato cha chini halipo kwenye pombe pekee. Utafiti unaonyesha lipo katika bidhaa na huduma mbalimbali, ikiwamo mbolea ambayo huuzwa chini ya kilo 50.
Pamoja na mambo mengine, siyo kila mmoja anahitaji mbolea kilo 50 na siyo kila mmoja anaweza kuinunua. Bidhaa nyingine zenye ujazo tofauti kutegemeana na uwezo na matamanio ya walaji ni maji, juisi, mvinyo na mafuta; ya kula au mitambo.
Nyingine ni sukari, unga, mchele na majani ya chai. Hivi huuzwa hadi kwa vipimo vidogo zaidi kama kijiko kimoja. Mfano mwingine ni bei ya muda wa maongezi katika simu ya mkononi.
Vocha zipo za bei na muda tofauti kutokana na mahitaji na uwezo wa mteja. Kwa mwenye kipato kidogo anaweza kununua kifurushi kinacholingana na uwezo wake kwa siku. Ni vizuri kufahamu misingi hii ya uchumi na viatu vya wenye kipato kidogo.
Ushauri
Haifai kuona viroba vikitumika kwa namna mbaya. Kukataza utengenezaji, uuzaji na utumiaji kama ilivyofanywa na Serikali kuboreshwe kama ilivyojadiliwa katika makala haya.
Hata hivyo, suluhu ya msingi ni kumaliza tatizo la msingi. Katazo hili linashughulikia dalili na matokeo ya tatizo kubwa na la msingi zaidi, siyo mizizi yake.
Tatizo la msingi ni tabia ya ulevi siyo ukubwa wa vifungashio. Kinachofanya mtu anywe kupitiliza ndiyo tatizo la msingi, wala si ukubwa au udogo wa kifungashio. Kama kuna tabia ya ulevi, kuvifanya vifungashio viwe vikubwa inaweza isisaidie.
Watu wanaweza kutafuta fedha na kununua hicho kinywaji cha ujazo ‘unaotakiwa’ na bado wakaendelea na ulevi kama ilivyokuwa katika zama za viroba. Ni muhimu kutatua tatizo la msingi, hili ni jukumu la jamii nzima siyo la Serikali peke yake.

0 comments:

Post a Comment