MJANE wa Rais mstaafu na Baba wa Taifa la Afrika Kusini, Nelson Mandela, Graca Machel amewataka viongozi wa wilaya ya Butiama na maeneo mengine ya mkoa wa Mara kumaliza tatizo la ndoa za utotoni, kwani linakatisha ndoto za watoto wengi.
Mama Graca ambaye pia aliwahi kuwa mke wa Rais wa zamani wa Msumbiji, Samora Machel ambaye alifariki dunia katika ajali ya ndege Oktoba 19, mwaka 1986 katika vilima vya Mbuzini, Jimbo la Mpumalanga, Afrika Kusini, alitoa ombi hilo juzi katika Shule ya Msingi Nyamisisi iliyopo wilayani hapa.
“Ndoa za utotoni ni tamaduni mbaya sana. Hapana kwa ndoa za utotoni, hapana kwa ndoa za utotoni. Ni jukumu lenu viongozi kusaidia kumaliza tatizo hili,” alisisitiza Mama Graca wakati akizungumza na wanafunzi na walimu wa shule hiyo.
Alikuwa akizungumza pia na wazazi, walezi na viongozi wa wilaya hiyo. Alisema kila mtoto ana haki ya kukua na hatimaye kuamua ni wakati gani wa kuolewa au kuoa na ni nani wa kumuoa na si kulazimishwa ili kupata mali.
Mama Graca alisema ameamua kuleta taasisi yake ya Graca Machel Trust (GMT) katika kusaidia watoto walio nje ya shule katika wilaya ya Butiama na maeneo mengine ya mkoa wa Mara ili kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kupata elimu.
Alisema GMT iko tayari kuendelea kushirikiana na Mara Alliance (muungano wa wadau wa maendeleo Mara) na serikali ya mkoa wa Mara kuifanya Butiama mfano wa eneo ambalo halina tatizo la ndoa za utotoni na mila ambazo zina madhara kwa watoto.
Mama Graca pia alizungumza na watoto ambao wako nje ya mfumo ya shule na hivi sasa wameandikishwa kupata elimu chini ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (Memkwa).
Aliwataka watoto hao kutumia fursa hiyo vizuri ili waweze kupata elimu na ujuzi ambao utawasaidia katika maisha yao chini ya mradi ambao unatekelezwa na Mara Alliance, GMT na Mkoa wa Mara.
“Mmepewa fursa ya pili kumaliza elimu ya msingi, soma kwa bidii na msikate tamaa,” aliwaambia watoto hao. Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi alisema tayari kuna watoto 28 ambao wameanza kunufaika na mpango huo katika shule ya msingi Nyamisisi.
Matokeo ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Uchumi na Jamii (ESRF) chini ya mradi huo umebaini watoto 11,666 wenye umri kati ya miaka saba hadi 17 ambao wako nje ya mfumo wa shule katika wilaya za Butiama, Bunda na Tarime.
Matokeo hayo yalitolewa Jumatatu wiki hii katika mkutano maalumu uliohudhuriwa na Mama Machel, wadau wa Mara Alliance wakiongozwa na Mwenyekiti wao Askofu wa Jimbo Katoliki Jimbo la Musoma, Michael Msonganzila na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Vincent Anaano.
0 comments:
Post a Comment