Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewataka wakurugenzi akiwamo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), wajipime iwapo utendaji wao unafaa kuendelea na nyadhifa walizonazo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya Veta, Profesa Ndalichako alisema miradi mingi ya maendeleo imekwama pasipo sababu za msingi.
Waziri huyo alisema miradi hiyo yenye thamani ya Sh14.5 bilioni imekwama kutekelezwa, zikiwamo karakana 11 ambazo hazijajengwa, nne zikiwa Mkoa wa Lindi, Manyara (4) na Pwani (3).
"Siridhishwi na utendaji wa Veta, watendaji wamekuwa watu wa michakato kila wakiulizwa wanasema mshauri elekezi hajapatikana. Vyuo vina mahitaji makubwa. Kinachonishangaza kumekuwa na kigugumizi katika ujenzi. Ni nani anayezuia fedha zisitoke," alisema Profesa Ndalichako.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Dk Bwire Ndazi alisema miradi hiyo ilikuwa inakwamishwa na utaratibu wa michakato ambayo imekuwa ikichukua muda mrefu kutekelezeka.
Dk Ndazi alisema utaratibu wa kuwapata wazabuni, kuwatangaza na hatua ya uchoraji huchangia ucheleweshaji.
0 comments:
Post a Comment