ALIYEKUWA Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, jana Alhamisi mchana alimwaga machozi wakati akizungumza na waandishi wa habari punde baada ya kuondolewa katika Baraza la Mawaziri.
Nape ambaye amewahi kuwa Katibu Mwenezi na Itikadi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alivuliwa uwaziri jana asubuhi na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe.
Mbunge huyo wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi, alimwaga machozi baada ya kuzuiwa kufanya mkutano na waandishi hao katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza akiwa juu ya gari lake, Nape aliahidi kuendelea kusimamia ukweli japo anafahamu una gharama zake ambazo ndiyo kama ilivyomtokea kwa uwaziri wake kutenguliwa.
Nape aliingia matatani na uteuzi wake kutenguliwa punde baada ya kuunda Kamati ya Saa 24 kuchunguza uvamizi unaodaiwa kufanywa katika Kituo cha Televisheni cha Clouds Media Group na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo juzi ripoti hiyo ilikabidhiwa kwake na kuahidi kuifikisha kwa wakubwa zake.
"Sikuombwa kuwa waziri hivyo hakukuwa na ulazima wa kupewa taarifa kwamba nitakoma kuwa waziri, namshukuru Mheshimiwa Rais (John Magufuli) kwa kuniamini kwa kipindi cha mwaka mmoja," alisema Nape.
"Nasikitika kwamba nilikikuta chama katika shimo na kupambana kukiinua hadi kukifikisha hapa kilipo, halafu watu wachache wanakuja hapa na bastola kunitisha. Niwaombe tu Watanzania tuendelee kuwa watulivu na kudumisha amani," alisema na kumpongeza Mwakyembe kwa kupewa nafasi yake.
0 comments:
Post a Comment