Social

Thursday, March 16, 2017

Mwenyekiti CCM Iringa aeleza machungu ya kufukuzwa



ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Dk Jesca Msambatavangu amesema baada ya kufukuzwa uanachama wa chama hicho, hatma yake kisiasa inategemea majibu atakayopewa na Mwenyezi Mungu.
Akizungumza nyumbani kwake mjini hapa, alisema; “Mungu ndiye atakayenionesha njia siwezi kuwa na majibu ya haraka, kilichonikuta hakina tofauti na kufiwa.”
Mbali na kufananisha tukio lililomkuta na msiba, alisema maamuzi ya kufukuzwa uanachama yaliyofanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, hakuyapokea kwa mshtuko mkubwa kwa sababu alisikia taarifa hizo zikisemwasemwa kabla ya kikao hicho.
Pamoja na kwamba hajui tuhuma iliyomfukuzisha uanachama kwa kuwa hajapewa rasmi barua ya kufukuzwa, alisema taratibu zilizofikia maamuzi hayo zilifuatwa.
“Kwa hiyo nikipewa barua rasmi ya kufukuzwa uanachama nadhani nitakuwa na la kuzungumza kwa sababu ndani ya barua hiyo kutakuwa na sababu ya kufukuzwa kwangu,” alisema na kuongeza kuwa ameanza na atajitahidi kwa kadri ya uwezo wake na kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu kuishi nje ya mfumo wa CCM alioupenda kutoka moyoni mwake na kwamba ambao alikuwa tayari kupoteza maisha yake kwa ajili ya chama.
“Sisi Wakristo tunaamini kila jibu lina mtihani wake. Huu ni mtihani wangu, Mungu ameruhusu nipite njia hii na yeye ndiye atakayekuwa wa mwisho kutoa hukumu sahihi juu ya hili, kwa sababu sikuwahi kufikiria kama kuna siku nitafukuzwa uanachama,” alisema Msambatavangu.
Akiwatia moyo wanaCCM wanaobaki ndani ya chama hicho, alisema; “askari mmoja akifa vitani, ni wajibu wengine wakachukua silaha yake na kuendeleza vita hiyo.”
Alisema kabla ya mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM mwaka 2015, yeye na wanaCCM wengine wengi walimuunga mkono Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.
“Tulimuunga mkono tukijua hiyo haikuwa dhambi kwa kuwa ni mwanaCCM mwenzetu na tuliamini angeweza kupokea kijiti kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete na kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa mbele zaidi,” alisema.
Alisema kama ambavyo wao waliamua kumuunga mkono Lowassa, wapo wana CCM wengine waliwaunga mkono wagombea wengine, na kwa mujibu wa taratibu za chama hicho na ndio sababu wengi walijitokeza kugombea nafasi hiyo.
Alisema baada ya CCM kukamilisha mchakato wa kumpata mgombea wao, walikuwepo waliohama chama hicho, lakini yeye na wanaCCM wengine wengi waliokuwa wanamuunga mkono Lowassa walibaki na kukisaidia chama kupata ushindi kwa sababu huo ndio wajibu wao.
Alisema kwa sasa ataelekeza nguvu zake kuimarisha shughuli zake za ujasiriamali.

0 comments:

Post a Comment