Social

Friday, March 24, 2017

Mastaa Yanga waishi kwa wasiwasi




MASTAA wanne wa Yanga ni kama wanamkwepa kocha mkuu wa timu hiyo, George Lwandamina baada ya wenyewe kutokuwa na uhakika na maisha yao klabuni hapo.
Mastaa hao Pato Ngonyani, Malimi Busungu, Matteo Antony na Beno Kakolanya wamekuwa na maisha magumu klabuni hapo tangu kuwasili kwa Lwandamina na sasa hawafahamu kama watasalimika na panga la kocha huyo ama la.
Kakolanya ambaye kazi yake ni kuzuia mpira usiingie wavuni amekuwa na kazi ngumu ya kupata namba mbele ya Ally Mustapha 'Barthez' na Deo Munishi 'Dida'. Chipukizi huyo alisema kwamba hadi anakubali kuitumikia timu hiyo alikuwa anafahamu kwamba ushindani ni mkubwa klabuni hapo.  Kakolanya alisema alitambua  kwamba isingekuwa kazi nyepesi kupata namba moja kwa moja mbele ya  Barthez na Dida, ila alijiandaa kwa ushindani wa kuonyesha alichonacho.
"Najua kwa nini walinisajili na ndiyo maana nikipata nafasi najituma na kuonyesha uwezo wangu,Yanga walitaka kipa wa kuwapa changamoto makipa wao, lakini isingekuwa rahisi kwamba watapigwa chini," alisema
Straika aliyeanza kwa kasi kabla ya kupotea, Busungu hakutaka kuzungumza kwa kirefu zaidi ya kudai kwamba atafuata nyayo za Mtanzania Elias Maguli ambaye anacheza soka la kulipwa Oman katika klabu ya Dhofar.
"Sitaki kuzungumzia hilo kwa sasa ila ipo siku nitafanya kama alivyofanya Maguli, aliondoka Simba kwenda Stand United lakini kwa sasa anasakata soka la kulipwa Oman, hivyo naamini kwamba soka ni safari," alisema.

0 comments:

Post a Comment