Social

Saturday, March 11, 2017

Mabao ya Neymar yaua mtu


Taarifa kutoka Catalan zinafichua kwamba kushangilia kulikofanywa na mashabiki 96,000, waliokuwa uwanjani Nou Camp baada ya Barcelona kupindua matokeo dhidi ya Paris Saint-Germain, kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano iliyopita kwamba kulisababisha tetemeko la ardhi.
Luis Suarez, Lionel Messi, Neymar, Sergi Roberto na bao la kujifunga yalitosha kwa Barca kushinda 6-1 na hivyo kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 6-5 baada ya kukumbana na kipigo cha mabao 4-0 kwenye mechi ya kwanza iliyofanyika Paris, Ufaransa.
Lakini, hiyo si kitu, mabao hayo ya akina Messi na Neymar hasa lile la Sergi Roberto limeondoka na maisha ya mtu huko Nigeria.
Shabiki mmoja aliyefahamika kuwa ni wa Barcelona, Tari Waha alianguka na kufariki dunia wakati alipokuwa akishangilia mabao ya timu hiyo kwenye mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Tari Waha, mwenye umri wa miaka 45, ambaye ni mmiliki wa duka ni shabiki wa kutupwa wa Barcelona na alikuwa akitazama mechi hiyo katika kibanda cha kuonyeshea mechi huko Upper Luggere, Yola.
Mwanzoni ilionekana kama Barca wasingeweza kufuzu hatua ya robo fainali baada ya kuchapwa 4-0 kwenye mechi ya kwanza na kisha PSG kufanikiwa kupata bao la ugenini jambo lililowafanya wababe hao wa Nou Camp kuhitaji kufunga mara tatu zaidi wakati dakika zilikuwa zimebaki chache sana katika muda wa kawaida.
Tari alionekana akishangilia kwa nguvu sana kila bao ambalo Barca walifunga katika mechi hiyo na wakati Barca walipofunga bao la tano, lililowekwa wavuni kwa mkwaju wa penalti na Neymar, Tari alipiga kelele sana wakati anashangilia kabla ya kuanguka na kufariki.
Rafiki wa marehemu, ambaye alijitambulisha mwenyewe kwa jina la Zakaria alisema kwamba watazamaji wengine waliokuwa kwenye ukumbi huo kutazama mechi hiyo walimwahisha Tari hospitali mahali ambako walithibitisha kuwa alikuwa tayari ameshakufa.
Matokeo hayo ya Barca na PSG yamekuwa na matukio ya ajabu ajabu baada ya kuripotiwa kwamba huko Paris, PSG imethibitisha kwamba kundi la mashabiki wenye hasira wameharibu vibaya magari ya wachezaji wa timu hiyo huko kwenye Uwanja wa Ndege wa Le Bourget.
Kundi hilo la mashabiki walikuwa na hasira walikusanyika kwenye uwanja huo wa ndege juzi Alhamisi asubuhi ambapo timu ya PSG ilitarajia kurejea ikitokea Barcelona ilikokwenda kuchapwa 6-1 na kutopwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

0 comments:

Post a Comment