Social

Friday, March 10, 2017

Wazazi wafurika Rita kufuatilia vyeti vya kuzaliwa


Dar es Salaam. Mitihani ya Taifa inayotarajiwa kufanyika mwaka huu kwa madarasa ya nne na saba imesababisha ofisi za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) zilizopo katika mitaa ya Posta na Makunganya jijini Dar es Salaam, kufurika wazazi na walezi wanaofuatilia vyeti vya kuzaliwa.
Ofisi hizo ambazo zipo jirani na ilipokuwa Kilabu Bilicanas, zimekuwa zikijaa watu kuanzia asubuhi hadi jioni huku ikielezwa wengi wanaofika ni wazazi kutoka sehemu mbalimbali Dar es Salaam na mikoani wanaofuatilia vyeti vya watoto wao.
Kaimu Ofisa Mtendaji wa Rita, Emmy Hudson alisema jana kuwa, wimbi hilo la watu lilianza kujitokeza hivi karibuni baada ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi kutoa mwongozo unaowataka wanafunzi wa madarasa hayo kuwa na vyeti kama kigezo mojawapo cha kufanya mitihani ya Taifa.
 Emmy alisema kutokana na mwongozo huo, idadi ya wananchi wanaofika kushughulikia vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wao imekuwa ikiongezeka siku hadi siku.
 "Huo mwongozo nadhani ndiyo unaofanya watu wajae kiasi hiki. Ukifika asubuhi jengo zima huko chini utaona watu wengi," alisema Emmy.
 Hata hivyo, kaimu mtendaji huyo alisema katika kushughulikia suala hilo wamejipanga vyema ili kutowakatisha tamaa wananchi.
 Alisema huduma za utoaji vyeti pia zinafanyika katika ofisi zao zilizopo katika halmashauri zote za Jiji la Dar es Salaam. 

Alipotafutwa kuzungumzia mwongozo wa wanafunzi wa madarasa hayo kuwa na vyeti vya kuzaliwa kabla ya kufanya mitihani ya Taifa, Ofisa Habari wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi, Mwasu Swale alielekeza aulizwe Kaimu Kamishna wa Elimu, Nicolaus Bureta.

Hata hivyo, juhudi za gazeti hili kumpata Bureta hazikuzaa matunda baada ya kuelezwa kwamba yupo safarini kikazi ambako hata simu yake ya mkononi haipatikani.

Kila mwaka, wanafunzi wa darasa la nne hufanya mitihani ya Taifa ya majaribio ambayo huwawezesha kuingia darasa la tano. Kwa darasa la saba, mitihani ya kuingia kidato cha kwanza hufanyika mwezi Septemba.

Wakati huohuo, Rita inatarajia kuanza kampeni ya usajili wa vizazi kwa watoto wa chini ya miaka mitano katika mikoa ya Geita na Shinyanga kuanzia mwezi ujao.

Emmy alisema usajili huo utafanyika kwa miezi sita katika wilaya tatu za Mkoa wa Shinyanga na tano na mkoani Geita.

0 comments:

Post a Comment