Social

Saturday, March 11, 2017

Warioba: Serikali ijiandae kukabiliana na njaa nchini


Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema kutokana na upungufu wa chakula uliopo nchini, Serikali ijiandae katika kukabiliana na hali hiyo.
Pia, amewataka viongozi kuacha kubishana, badala yake waungane kutoa elimu kwa wananchi ya namna watakavyotumia mvua zinazonyesha kwa ajili ya kilimo cha mazao yanayovumilia ukame.
"Hivi sasa kuna dalili za upungufu wa chakula na hili ni tatizo, hivyo Serikali ijiandae. Tusianze kubishana kama kuna njaa au kuna upungufu wa chakula au huyu kasema hivi, yule kasema hivi kwa sababu mabishano hayo hayatawasaidia wananchi," alisema Jaji Warioba jana wakati akizindua kitabu cha Mtandao wa Wanawake na Katiba.
Mbali na hilo, kiongozi huyo alisema kinachotakiwa kwa sasa ni jamii kupewa elimu na taarifa za hali ya hewa ili iweze kujua  hali halisi ya mvua na namna itakavyozitumia kwa kilimo.
Kuhusu mapambano ya dawa za kulevya, alisema hayapaswi kuwa ya mtu mmoja, bali Taifa zima liungane na viongozi wasione kama ni tukio la kawaida.
Jaji huyo mstaafu alisema viongozi wanapaswa kwenda kwa wananchi kuwapa elimu ili wajue madhara na namna ya kujiokoa na tatizo hilo kwa lengo la kulinda kizazi kilichopo na vile vinavyokuja. "Napenda tushirikiane kwa pamoja katika kuongeza nguvu kuzuia, kupambana na kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kuwasaidia wale ambao wamepata madhara kutokana na matumizi ya dawa hizo," alisema.
Awali, wakati akizindua kitabu hicho, Jaji Warioba aliwapongeza wanawake walioshirikiana pamoja katika kuainisha matatizo na kujenga mkakati wa kuyashughulikia bila kujali itikadi za vyama vyao vya siasa.
Alisema walichofanya ni kutanguliza mbele masilahi ya Taifa na siyo ya vyama wanavyoviwakilisha kiitikadi.
Mwenyekiti wa Mtandao  wa Wanawake na Katiba, Profesa Ruth Meena alisema lengo  la kuandikwa  kwa kitabu hicho chenye kurasa 59 kilichopewa jina la 'Nguvu Zetu, Sauti Zetu' ni kuainisha haki za sasa za wanawake.
"Katika suala la ukombozi wa mwanamke hakuna itikadi ya chama na sauti zetu ndizo zinatukomboa, hivyo linapofikia suala la mwanamke basi wote tuzungumze na tupaze sauti," alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi ambaye ni mtunzi wa kitabu hicho alisema kimeainisha maeneo muhimu yanayohusu haki za wanawake na kwamba, dibaji ya kitabu hicho iliandikwa na Jaji Warioba.

0 comments:

Post a Comment