Social

Friday, March 24, 2017

SANITAS yapata wajumbe wapya wa bodi


Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu mstaafu nchini Jaji Mark Bomani ameteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Sanitas yenye jumla ya wajumbe tisa.
Jaji Bomani amewahi kuwa Jaji Mkuu wa Pili wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alishiriki kuunda mfumo wa sheria wa Namibia baada ya Uhuru wa nchi hiyo.
Pia, ana uzoefu mkubwa katika kufikia makubaliano kimataifa, akiwa mshauri wa Mwalimu Nyerere na Nelson Mandela wa Afrika Kusini wakati wa juhudi zao za kutafuta amani ya Burundi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji na Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Dk Krishnamurthy Venkateswaran alisema Sanitas imekuwa ikitoa huduma kwa wagonjwa kutokea Mikocheni Dar es Salaam tangu mwaka 2013.
Alisema kwa miezi 40 ya utoaji huduma imeweza kufikia uwezo wa kuhudumia wagonjwa 350 kwa siku, kwa kutumia utaalamu wa hali ya juu na vifaa vya kisasa.
"Sanitas imekuwa ikihudumia kwa kutoa huduma za magonjwa sugu na magonjwa ya dharura ikiwamo magonjwa ya mifupa," alisema Venkateswaran.
Alisema pia, imekuwa ikiandaa mpango wa tiba maalumu kwa wataalamu wa magonjwa mbalimbali katika masuala ya afya ambayo yanaikabili Tanzania.
Uzoefu wa mwenyekiti huyo wa Bodi ni katika ujasiriamali ambao umeisaidia hospitali hiyo kufikia ilipo.
Mtaalamu wa magonjwa ya mifupa, Dk Gautama Kodikal kutoka Bangalore, India, ni mwenyekiti wa Bodi ya Sanitas akiwa na uzoefu wa muda mrefu katika tiba na amekuwa msaada mkubwa katika kutoa mwongozo kuhusu namna ya kupanua huduma za hospitali hiyo.
Mwingine ni mtaalamu wa masuala ya utawala ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kibenki kutoka India, Shailesh Shah ambaye anatarajiwa kuanza kuweka mfumo wa kisasa wa usimamizi wa fedha katika hospitali hiyo baada ya kuungana na Bodi jana.
Ofisa Mkuu wa Tiba wa Manispaa ya Kinondoni, Dk Aziz Msuya ambaye ni mjumbe mshauri wa Bodi, amekuwa akiisaidia hospitali hiyo katika masuala ya taratibu na sheria zinazosimamia sekta ya afya kwa kuhakikisha ubora wa huduma zinazotolewa.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdullah Mwinyi naye pia ni mmoja kati ya wajumbe wa Bodi hiyo.
Akizungumza baada ya kutangazwa rasmi, alisema licha ya kwamba amekuwa akijihusisha na masuala ya kisheria, kwake ni muafaka kushughulika na masuala ya afya.
Wengine ni Petronella Mwasandube, Gean Cabral, Simon Ezekiel na Ally Kifu ambao ni wajumbe wa Bodi.

0 comments:

Post a Comment