Social

Wednesday, March 22, 2017

Miaka minne ya Malinzi TFF ni mirefu kuliko 30 ya Hayatou CAF



ANA umri wa miaka 70, Issa Hayatou, hakukubali kirahisi mabadiliko. Alisubiri kuondoka kwa aibu katika nafasi yake ya Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika (Caf). Hakutaka kuondoka kwa heshima na ndio maana aling'ang'ania madaraka ili aendelee kukaa katika ofisi za shirikisho hilo jijini Cairo, Misri.
Raia huyo wa Cameroon alisahau kuwa mazingira yamebadilika, kizazi kipya kimezaliwa, kimechoshwa na siasa za kizamani, siasa za makundi ambazo zimelifanya soka la Afrika kudumaa.
Hayatou alichaguliwa kuwa Rais wa Caf mwaka 1988 na ameliongoza shirikisho hilo kwa karibu miaka 30 mpaka alipoangushwa wiki iliyopita na Ahmad Ahmad wa Madagascar kwenye uchaguzi.
Kwa miaka 30 itakuwa si haki kusema hajafanya lolote, lakini pia kwa miaka yote hiyo viongozi wetu wanapaswa kutambua kuwa kung'ang'ania madaraka ni kujiweka katika aibu ambayo si ya lazima.
Hayatou hana nguvu za kuhimili mikiki ya soka la Afrika, lakini bado aligombea nafasi hiyo na kushindwa kwa kupata kura 20 dhidi ya 34 za Ahmad.
Ilifika mahali, Caf ikawa kama genge la watu fulani wachache ambao wangeweza kujifungia kwa jina la Kamati ya Utendaji na kufanya uamuzi wa ovyo ambao ungeshangaza si Afrika tu ila dunia kwa jumla.
Miongoni mwa uamuzi wa ovyo walioufanya, lakini baadaye ulibadilishwa ni kuwa mtu ambaye hayumo kwenye Kamati ya Utendaji alizuiwa kuwania nafasi za juu za Caf.
Ukiondoa hilo kwa jumla, Caf ilikuwa imewekwa chini ya himaya ya watu wachache kiasi kwamba mawazo mapya hayakuruhusiwa wala ubunifu haukuwa sehemu ya maisha ya shirikisho hilo tena.
Miaka 30 ya Hayatou Caf ni sawa na miaka minne ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.
Ni miaka minne ambayo imetumiwa kujiandaa kwa uchaguzi wa pili kuliko kufanya maendeleo ya mchezo wa soka. Ni miaka ambayo imekuwa mirefu kuliko pengine miaka 30 ya Hayatou pale Caf.
Kamati za TFF hazipo huru, zote zinafanya kazi kwa ushawishi wa Rais, ratiba ya ligi zinapangwa au kupanguliwa kwa ushawishi wa kiongozi wa juu.

0 comments:

Post a Comment