Social

Wednesday, May 3, 2017

London: Bado dakika 180 tu


UNAHITAJIKA uchawi wa aina yake kuizuia Chelsea kutwaa ubingwa wa England msimu huu. Juzi walimaliza kazi nzito iliyokuwa inawakabili baada ya kuichapa Everton mabao 3-0 pale Goodson Park.
Ratiba ya Chelsea katika mechi zilizobaki inaashiria kwamba, mashabiki wake duniani kote wanaweza kuanza kujiandaa kuweka mivinyo katika friji zao kwa ajili ya kusheherekea ubingwa licha ya Tottenham kuendelea kuwaghasi.
Tottenham ilishinda mabao 2-0 dhidi ya mahasimu wao, Arsenal dimba la White Hart Lane, lakini Chelsea imebakiza mechi mchekea ambazo zinawafanya waanze kukenua mapema zaidi. Katika ratiba yao watacheza na timu moja tu iliyo katika 10 bora katika msimamo wa ligi mpaka sasa.
Jumatatu usiku Mei 8, Chelsea itakuwa nyumbani kuikaribisha Middlesbrough ambayo imeendelea kuchungulia shimo ya kushuka daraja licha ya kumfukuza kocha wake aliyeipandisha Ligi Kuu, Aitor Karanka.
Siku nne baadaye Ijumaa Mei 12, Chelsea itakuwa ugenini kucheza na West Brom ambayo ndio timu pekee iliyo katika 10 bora ndani ya msimamo wa sasa Ligi Kuu England. Hata hivyo, Chelsea haitazamiwi kupata upinzani mkali katika pambano hilo.
Siku ya Jumatatu Mei 15, Chelsea itakuwa nyumbani Stamford Bridge kuikaribisha Watford katika pambano ambalo inaweza kutangaza ubingwa wa England siku hiyo kama mambo yatakwenda sawa katika mechi mbili zinazokuja sasa.
Kama Chelsea itashindwa kutangaza ubingwa katika siku hiyo bado itaweza kutangaza katika siku ya mwisho ya msimu Mei 21, ambapo watakuwa nyumbani dhidi ya Sunderland ambayo imeshashuka daraja wikiendi hii baada ya kuchapwa na Bournemouth ikiwa nyumbani.
Wakati ratiba ikionekana kuwa rafiki sana na Chelsea, mambo hayapo hivyo sana kwa wapinzani wao wa karibu Tottenham ambao, licha ya kushinda nyumbani juzi dhidi ya Arsenal lakini wamebakiwa na mechi nne na tatu kati ya hizo watakuwa ugenini.
Pambano pekee ambalo watakuwa nyumbani watakuwa wakikabiliana na kikosi cha Jose Mourinho, Manchester United katika dimba la White Hart Lane Jumapili Mei 14. Lakini kabla ya hapo Tottenham watalazimika kwenda London wikiendi ijayo kupambana na West Ham Ijumaa hii katika dimba la London la West Ham.
Bada ya Manchester United, Tottenham watalazimika kusafiri kwenda kucheza na Leicester City ugenini katika dimba la King Palace Alhamisi Mei 18. Leicester kwa sasa imerudi katika makali yake baada ya kumfukuza kocha aliyewapa ubingwa, Claudio Ranieri na nafasi yake imechukuliwa na kocha wa muda, Craig Shakespeare.
Pambano la mwisho kwa Tottenham litakuwa dhidi ya Hull City Mei 21 ugenini tena. Kama Hull City itakuwa haijapoteza matumaini ya kubakia Ligi Kuu mpaka siku hiyo basi pambano hilo litakuwa gumu zaidi kwa Spurs.
Kwa upande wa Chelsea tena, baada ya kumaliza ligi inaweza kubeba taji jingine la FA pale itakapokwenda Wembley kukipiga na Arsenal katika pambano la fainali Mei 27 wakati huu kikosi cha Wenger kuwa ovyo.

0 comments:

Post a Comment