Social

Tuesday, May 16, 2017

Waasi, Serikali ya Ivory Coast wafikia makubaliano



Abidjan, Ivory Coast. Serikali imetangaza kupitia kituo cha televisheni cha serikali (RTI) kwamba imefikia makubaliano na askari walioasi na kuahidi kulipa madai yao ndani ya siku nne.
Tangazo hilo lililodumu chini ya dakika mbili lilitangazwa juzi na Waziri wa Ulinzi wa Ivory Coast, Alain-Richard Donwahi. Hata hivyo, waziri huyo hakueleza utaratibu utakaotumiwa kwa kulipa madai askari hao.
Lakini baadaye wazungumzaji wawili wa wanajeshi hao walisema wamekataa ombi hilo na kuitaka serikali imlipe kila mwanajeshi Faranga CFA milioni tano mpaka saba karibia dola 12,000.
Kutokana na kauli hizo ilikuwa vigumu kusema kama wito wa utulivu uliotolewa na waziri huyo Jumatatu usiku ulitekelezwa na askari waasi au la. Katika mji wa pili wa ukubwa nchini humo wa Bouake, hali ya wasiwasi iliendelea kushuhudiwa, na askari walioasi waliendelea kuonekana mitaani, huku risasi ziliendelea kufyatuliwa hewani.
Askari walioasi walikuwa wakisubiri jana usiku kama malipo wanayoendelea kudai yaani faranga CFA 7 milioni zitalipwa kwa pamoja kwa kila askari, kwa mkatomkato, mara moja au kwa kila mwezi.
"Makubaliano yalifikiwa kuhusu utaratibu wa kuondokana na mgogoro huu. Kwa hiyo tunatoa wito kwa askari walioasi kurejea kambini na kuhakikisha usalama wa wananchi," alitangaza Donwahi

0 comments:

Post a Comment