Social

Wednesday, May 24, 2017

Kuwait yaingilia mauaji Kibiti Tanzania


Dar es Salaam. Ubalozi wa Kuwait  nchini umeishauri Serikali kutumia busara zaidi katika kutatua na kudhibiti mauaji yanayoendelea mkoani Pwani na kufanyika kwa uchunguzi wa kina.
Mpaka sasa tayari takriban watu 31, wakiwamo viongozi na askari wa Jeshi la Polisi, wameshauawa katika wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi imezifuatilia kuanzia Mei mwaka jana.
Akizungumza na waandishi wa habari hizi,  Katibu wa Kwanza wa  Ubalozi wa Kuwait Mohammad Alamiri ambaye alimwakilisha Balozi wa nchi hiyo amesema kwamba watu wanaouawa  Kibiti ni wale wasiokuwa na  hatia.
 "Tanzania ni nchi yenye amani lakini haya mauaji yanaitia doa kwa kiasi kikubwa ni vizuri uchunguzi ukafanyika ili kubaini nini hasa chanzo cha mauaji hayo ambayo yanaangamiza wasiokuwa  na hatia," amesema Alamiri.
Amesema pia angeshauri Jeshi la Polisi kukamata wauaji halisi badala ya kuwakamata watu ambao hawakuhusika kabisa na mauaji hayo jambo ambalo linaleta hofu kwa wakazi wa maeneo hayo.
Katibu huyo amesema Serikali inapaswa kuwashirikisha wananchi  katika kupambana na mauaji ya polisi na raia yanayoendelea kutokea katika wilaya hizo hususan kipindi hiki cha kuelekea mwezi mtukufu wa ramadhani unaotarajiwa kuanza  mwishoni mwa wiki.
Kumekuwapo na mlolongo wa matukio ya mauaji katika Wilaya za Kibiti na Mkuranga na kinachozua maswali ni kitendo cha wauaji kutochukua mali yoyote.
Mei, 2016 Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Said Mbwana, aliuawa kwa risasi.
Oktoba, 2016, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho hicho, Ally Milandu, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wanne.
Novemba, 2016 wenyeviti wawili wa vitongoji wa kijiji hicho, waliuawa kwa kupigwa risasi.
Januari, 2017 watu ambao Jeshi la Polisi hadi sasa halijawafahamu waliomuua mfanyabiashara, Oswald Mrope kwa kumpiga risasi mbele ya familia yake.
Februari 3, 2017 watu wasiojulikana walivamia nyumba ya mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga na kuichoma moto huku yeye mwenyewe akifanikiwa kuwatoroka.
Tukio la kuuawa kwa askari saba limetokea ikiwa ni siku chache baada ya askari wa Jeshi la Polisi kuwaua kwa risasi watu  watatu waliokuwa wamevalia buibui.
Watu  hao ambao walikuwa na pikipiki mbili, walikuwa wakijaribu kukwepa vihunzi vya polisi vilivyokuwa vimewekwa katika daraja la Mkapa.
Mei 18, Mwenyekiti wa CCM tawi la njia nne, kata ya mtunda, alipigwa risasi na kuuawa usiku. Mtoto wake aliyejeruhiwa kwa risasi ya tumbo nae pia amefariki dunia.

0 comments:

Post a Comment