Social

Tuesday, May 30, 2017

Mchanga wa dhahabu waibua mjadala bungeni Tanzania




Dodoma. Sakata la mchanga wa dhahabu uliozuiwa kwa amri ya Rais John Magufuli jana liliacha vumbi bungeni huku Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akitahadharisha nchi kupata hasara kubwa.
Mchango wa Lissu ulionekana kuchafua hali ya hewa bungeni, hadi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama akiomba Lissu aamriwe kufuta baadhi ya maneno.
Lissu alichangia kwa hisia kali na kutoa maneno makali dhidi ya Rais Magufuli, Mhagama alisema maneno hayo si lugha ya kibunge kwa mujibu wa kanuni ya 64 ya Kanuni za Bunge.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alikubali na kuyafuta maneno hayo baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu kumuamuru afute.
Hayo yalijitokeza wakati wa kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyosomwa na Balozi Dk Augustine Mahiga kwa mwaka fedha wa 2017/2018.
Mbunge wa kwanza kuibua sakata hilo alikuwa Mbunge wa Arusha mjini (Chadema), Godbless Lema akisema suala la mchanga huo litaligharimu Taifa ana kwamba tayari Acacia wanafungua kesi Uingereza.
Akijibu hoja za Lissu na Lema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju amewataka wabunge kuungana na kuiunga mkono Serikali kwa hatua ilizochukua kuhusu mchanga wa dhahabu.
"Kwenye hili hakuna sababu ya kulaumiana ni mapema mno kuilamu Serikali kwa hatua ilizochukua. Kati yetu hakuna aliyewahi kuiona mikataba hii. Naomba tutambue sisi ni familia moja," amesema.

0 comments:

Post a Comment