Kila Mtanzania amesikia habari za matukio kadhaa yanayoashiria kukosekana kwa usalama wa kutosha kwa baadhi ya makundi ya watu.
Kipindi cha miezi minne iliyopita, msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema alitoweka katika mazingira tata na hadi leo hajaonekana, lakini mamlaka zinazohusika na vyombo vya usalama havitoi taarifa zinazoonyesha kuwa vinafanya kazi kumsaka au vimeshakata tamaa.
Tumeshuhudia pia, kupitia picha za kamera za CCTV zilizothibitishwa na Clouds Media zikionyesha watu wenye silaha wakiingia studio za televisheni za kampuni wakiongozwa na kiongozi mwenye dhamana ya ulinzi na usalama wa raia mkoani Dar es Salaam. Si wizara wala jeshi la polisi lililotoa taarifa kuhusu kilichotokea.
Waziri wa Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni ndiye pekee aliyeonekana akifuatilia suala hilo kabla ya kuachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri siku aliyotakiwa kuwasilisha ripoti ya uvamizi.
Na siku alipokuwa akienda kuzungumza na wanahabari kuhusu mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri, alisimamishwa na watu wawili nje ya Hoteli ya Protea, mmoja akachomoa bastola kumtishia wakati wakimlazimisha arudi kwenye gari la Serikali alilokuwa amelitumia kufika eneo hilo kuzungumza na waandishi wa habari.
Mashuhuda wa tukio lile ni waandishi wa habari pamoja na polisi waliokuwa eneo hilo ambako baadaye alipita kamanda wa polisi wa Kinondoni. Lakini mamlaka husika hazitoi taarifa kuhusu tukio hilo, na hufanya hivyo pale tu waandishi wanapoulizia.
Wiki hii inamalizika vibaya baada ya kuripotiwa kutoweshwa kwa msanii kijana, Roma Mkatoliki, ambaye imedaiwa ametekwa akiwa kazini. Siku nzima ya juzi na hata jana vyombo vinavyoshughulika na usalama wa raia vilidai havina taarifa za tukio hilo.
Jeshi la Polisi, ambalo limekuwa kimya katika matukio hayo, ndilo linalohaha kukamata wananchi inapotokea tuhuma kuwa wametoa lugha chafu dhidi ya viongozi iwe kwa njia ya simu au mitandao ya kijamii. Katika matukio hayo, Jeshi la Polisi limekuwa likitoa taarifa kuonyesha jinsi lilivyotumia ustadi wake kuwanasa watuhumiwa.
Kuna wakati jeshi hili lilifuatilia kwa kutumia mfumo wa GPS hadi likamkamata binti mmoja aliyekuwa amemteka mtoto wa bosi wake mwanajeshi. Mtoto alitekwa Dar es Salaam lakini mtekaji alinaswa Tanga. Vilevile, jeshi hilo ndilo lilimfuatilia mtu mmoja aliyewatukana hadi akakamatwa akiwa Bukoba.
Hata tukirudi nyuma, watu waliomvizia na kumuua aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, walinaswa kipindi kifupi.
Maswali ni kwamba kwa nini Jeshi la Polisi halionekani kuwa mstari wa mbele kuwasaka wahusika wa matukio haya ya utekaji na kutowekwa kwa wananchi?
Jana, kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema ataunda kamati kuchunguza suala la Roma Mkatoliki baada ya kuulizwa na mwandishi. Kwa nini Jeshi la Polisi likae nyuma katika masuala yanayohusu usalama wa wananchi? Kwa nini mamlaka husika zikae kimya wakati wananchi wanahoji masuala haya hadi bungeni?
Hakuna sababu kwa Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine zinazohusika kuruhusu mijadala inayoweza kuepukika, iendelee kutawala nchini. Na hakuna sababu ya kuachia hofu hii iendelee kutamalaki.
Vyombo husika vichukue hatua kuondoa hofu kwa wananchi kwa kuwapa taariofa, kuwasaka wahusika, kuwakamata na kuwashtaki mahakamani.
0 comments:
Post a Comment