Lindi. Wiki moja baada ya Mahakama kutoa uamuzi wa kuruhusu Ally Habibu Haji (Shikuba) kusafirishwa kwenda Marekani anakokabiliwa na shtaka la kujihusisha na dawa za kulevya, jana alifutiwa shtaka lingine na kuachiwa huru kabla ya kukamatwa tena na polisi.
Aliachiwa huru na Mahakama ya Wilaya ya Lindi baada ya upande wa mashtaka kumfutia shtaka kuhusu dawa za kulevya.
Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Aluu Nzowa kutokana na upande wa mashtaka kuwasilisha mahakamani barua ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ya kumuondolea shtaka mshtakiwa huyo.
Shikuba alikuwa miongoni mwa washtakiwa wanne wanaokabiliwa na shtaka la kujihusisha na biashara haramu ya kusafirisha dawa za kulevya.
Washtakiwa wengine ni Athuman Nyamvi, Ahmad Mohamed na Maureen Liyumba.
Akisoma barua ya DPP, Mwanasheria wa Serikali, Veronica Matikira alisema, "Mheshimiwa hakimu napenda kuiarifu Mahakama yako tukufu kwamba, ofisi yetu ya mkoa imepokea barua kutoka kwa DPP ikimuondoa kwenye kesi hii mshtakiwa wa nne, Ally Habibu, maarufu kwa jina la Shikuba."
Hakimu Nzowa akimfutia shtaka Shikuba katika kesi namba 04/2012, alisema Mahakama hiyo haina pingamizi kwa ombi la DPP hivyo akamuachia huru. Alisema kesi dhidi ya washtakiwa wengine itaendelea leo.
Shikuba alipotoka nje ya jengo la Mahakama alikamatwa na polisi waliokuwa wametanda kwenye eneo la viwanja vya mahakama. Baada ya kukamatwa alifungwa pingu na kupandishwa kwenye gari la polisi.
Washtakiwa waliosalia katika kesi hiyo wanadaiwa kukamatwa Januari 2012, katika Kijiji cha Mchinga Mbili wilayani Lindi wakiwa na dawa za kulevya walizokuwa wakizisafirisha kwenda Afrika Kusini.
Aprili 12, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliruhusu Shikuba na wenzake, Iddi Salehe Mfuru na Tiko Emmanuel Adam wasafirishwe kwenda Marekani kukabiliana na mashtaka ya kujihusisha na dawa za kulevya.
0 comments:
Post a Comment