Social

Wednesday, April 19, 2017

Pence: Marekani itaijibu Korea Kaskazini

Südkorea Besuch US Vizepräsident Mike Pence (picture-alliance/AP Photo/L. Jin-Man)
Korea Kaskazini ndiyo kitisho hatari zaidi kwa amani na usalama katika kanda ya Asia Pacific. Hayo ni kwa mujibu wa makamu wa rais wa Marekani Mike Pence.

Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence
Pence aliyasema hayo wakati alipokuwa akiwahutubia wanajeshi wa Marekani na Japan Jumatano, katika kambi ya jeshi la Marekani iliyoko Yokosuka, kusini mwa mji wa Tokyo nchini Japan.
Akiwa amevalia gwanda la kijeshi, Pence alisema utawala wa rais Donald Trump utashirikiana na washirika wake kama Japan na China na mataifa mengine makuu duniani ili kuiwekea shinikizo la kiuchumi na kidiplomasia Korea Kaskazini, lakini akawaambia wanajeshi hao kwamba, kuwa tayari ndiyo jambo muhimu.
"Kama alivyoweka wazi rais Trump kwa ulimwengu, kipindi cha subira kimeisha," alisema Pence.
Makamu huyo wa rais aliwasili mjini Tokyo Jumanne kwa ziara ya siku mbili, baada ya kukamilisha ziara ya siku tatu nchini Korea Kusini.
Marekani itajibu shambulizi lolote la nyuklia
"Muungano wa Marekani na Japan ndio nguzo ya amani, maendeleo na uhuru wa Asia Pacific," alisema pence. "Na wacha niweke wazi, chini ya rais Donald Trump, Marekani inashikilia muungano huu na haitobadili msimamo wake wa kutetea yale yote tuliyoyajenga pamoja katika kipindi hiki kilichopita," aliongeza kiongozi huyo.
Japan Besuch US-Vize-Präsident Mike Pence (Reuters/K. Kyung-Hoon)
Mike Pence akipokewa na naibu Waziri Mkuu wa Japan Taro Aso
Pence aliendelea kusema, yeyote atakayepinga maamuzi ya Marekani anastahili kufahamu kwamba,  watashinda shambulizi lolote dhidi yao na watajibu kwa njia mwafaka kama Marekani, matumizi yoyote ya zana za nyuklia.
Makamu huyo wa rais vile vile alieleza kwamba usalama wa kuzuru maeneo yaliyoko katika bahari ya kusini mwa China utalindwa, eneo ambalo China imekuwa ikisema liko katika himaya yake ingawa ni eneo lililo na mzozo wa umiliki.
"Marekani siku zote itatafuta amani, lakini chini ya rais Donald Trump, tuko tayari kujilinda na kushambulia, hilo munastahili kufahamu," alisema Pence. "Chini ya uongozi wa rais Trump Marekani itaendelea kuwalinda watu wetu na wandani wake na kuzidisha mshikamano baina yetu, kesho na kila siku," aliongeza makamu huyo wa rais wa Marekani.
Mikakati ya Trump inawiana na ile ya Obama
Uongozi wa Trump umeonesha ishara ya nguvu zake kuhusiana na matukio ya hivi majuzi ya Korea Kaskazini, kwa kumtuma Pence Jumatatu katika eneo lenye ulinzi mkali wa kijeshi linalogawanya Korea Kaskazini na Kusini. Lakini haibainiki kitakachotokea baada ya hapo.
Nordkorea Militärparade in Pjöngjang Kim Jong Un (picture-alliance/dpa/W. Maye-E)
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un
Mbali na yote hayo, mikakati ya Trump katika eneo hilo inaonekana kuwiana na ile aliyokuwa nayo rais wa zamani Barack Obama, ingawa Trump hatabiriki na ameonesha kwamba yuko tayari kutumia nguvu.
Ziara ya Pence kwa nchi mbili washirika wa Marekani huko Asia Mashariki ambayo pia ni ziara inayoshuhudia makamu huyo wa rais kuzuru nchi nne miongoni mwao Indonesia na Australia, inakuja wakati ambapo kuna taharuki kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.
Korea Kaskazini imeongeza juhudi za mipango yake chini ya kiongozi Kim Jong Un, kwani ilifanya majaribio ya mashambulizi mawili ya nyuklia na kufanya mashambulizi mengine 20 mwaka jana pekeyake.
Mwandishi: Jacob Safari/DPA/APE
Mhariri: Josephat Charo

0 comments:

Post a Comment