Dar es Salaam. Kasi ya ukuaji wa uchumi inatarajiwa kushuka kutoka asilimia 7.0 mpaka kufikia asilimia 5.6 mwaka huu kutokana na ukame na kutokuwapo kwa mazingira rafiki kwa sekta binafsi.
Sababu nyingine za kuporomoka huko ni Serikali kuhamisha akiba yake ya fedha kutoka benki za biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na hatua ya Serikali kubana matumizi katika ununuzi wa bidhaa na huduma.
Kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Kimataifa ya Fedha (IIF) iliyotolewa Aprili 25 kuangazia Tanzania, ukuaji wa uchumi ulianza kwa kasi ndogo mwaka huu, lakini unatarajiwa kuongezeka pale miradi mikubwa ya reli ya kisasa na bomba la mafuta la Uganda itakapoanza.
Hata hivyo, msemaji wa Wizara ya Fedha, Ben Mwaipaja alisema wizara yake haijapata taarifa zozote za ripoti hiyo na kuhoji vigezo walivyotumia kuonyesha kupungua kwa kasi ya ukuaji uchumi mwaka huu.
Alisema taasisi kubwa za fedha duniani kama Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zimetabiri ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwamba utakuwa kwa zaidi ya asilimia sita na kueleza wasiwasi wake kuhusu ripoti hiyo.
"Sijui hiyo ripoti imetoka lini lakini nashindwa kuelewa wametumia vigezo gani. Ninachofahamu ni kwamba uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi kwa zaidi ya asilimia sita kama WB na IMF walivyofanya tafiti zao," alisema Mwaipaja.
Hata hivyo, ripoti ya mwisho ya Benki ya Dunia inaonyesha kuwa kasi ya uchumi wa Tanzania ilipungua kutoka asilimia 7.2 mwaka 2015 hadi asilimia 6.9 mwaka jana.
Ripoti ya IIF inabainisha kwamba ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) hadi robo tatu ya mwaka jana ulishuka mpaka asilimia 6.2. Kiwango hicho kiliendelea kubaki katika robo ya nne ya mwaka 2016 na mwanzoni mwa huu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka huu uchumi utakua kutokana na miradi katika sekta za ujenzi, usafirishaji, mawasiliano, madini na biashara ambazo Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa.
Lakini, ripoti hiyo inasema uchumi utaendelea kukua kwa kasi endapo Serikali itatekeleza kikamilifu mipango yake ya maendeleo na kuwa moja ya nchi zinazokua kwa kasi Kusini mwa Jangwa la Sahara.
"Ili kuwa nchi ya viwanda, Serikali imeongeza tozo kwenye bidhaa kama vile saruji na chuma na kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa madini ili kuongeza msukumo wa kuchuja mchanga huo hapa nchini," inasema ripoti hiyo.
Tayari Serikali imezindua ujenzi wa reli ya kisasa kati ya Dar es Salaam na Kigoma na awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa Reli Kati ya Dar es Salaam na Morogoro. Reli hiyo inatarajiwa kurahisisha usafirishaji mizigo, abiria na biashara ya ndani na nje ya nchi.
Mapato ya Serikali kupungua
Ukusanyaji wa mapato ambao uliongezeka kwa asilimia 20 katika mwaka wa fedha wa 2016/17, unatarajiwa kushuka mpaka asilimia tisa mwaka 2017/18 kwa sababu shughuli za kiuchumi zitasimama.
Ripoti hiyo ya IIF inaeleza kwamba ongezeko la mapato kwa mwaka 2016/17 lilitokana na hatua ya Serikali kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kupanua mawanda ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ikijumlisha huduma za fedha na utalii.
Mapato yasiyotokana na kodi yanatarajiwa kubaki vilevile kwa mwaka 2017/18 baada ya kiwango kilichokadiriwa cha asilimia 77 kuongezeka mwaka huu.
Hata hivyo, wakati mapato ya ndani yakizidi kuimarika, misaada kutoka nje (wastani wa asilimia 1.7 ya GDP kuanzia 2007 - 2014), imeshuka baada ya wahisani kuizuia kutokana na suala la uchaguzi wa Zanzibar.
Kulingana na mapendekezo ya bajeti, IIF inakadiria Pato la Taifa kuongezeka mpaka kufikia asilimia 44 mwaka 2017 kutoka asilimia 41 za mwaka jana. Ongezeko la mwaka jana lilichagizwa na ongezeko la usafirishaji wa dhahabu na ukuaji wa sekta ya utalii.
0 comments:
Post a Comment