Social

Wednesday, April 12, 2017

Tume ya Serikali ya Haki za Binadamu, wanaharakati wahoji, wakemea vitendo vya utekaji


Dar es Salaam. Matukio ya utekaji yanayoendelea nchini yanazidi kupingwa na taasisi tofauti ambazo zinaitaka Serikali kuchukua hatua haraka.
Miongoni mwa taasisi hizo ni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), ambayo ni idara huru ya Serikali iliyoanzishwa chini ya ibara ya 129 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.
Taasisi nyingine ni Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), ambao umekemea vitendo hivyo.
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, tume hiyo inaeleza kuwa matukio ya kuvamiwa kwa kampuni za tasnia ya habari na mawasiliano au kuwateka watu, yanaashiria kutoweka kwa uvumilivu wa uwepo wa maoni tofauti katika jamii.
"Uchambuzi wa Tume unaonyesha kuwa waliotekwa wamefanyiwa hivyo kutokana na tasnia yao, au kutumia haki yao ya msingi ya uhuru wa maoni na kujieleza," inasema taarifa hiyo iliyosainiwa na mwenyekiti wake, Bahame Tom Nyaduga.
Taarifa hiyo inasema haki hizo zimeainishwa na kulindwa katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), kifungu cha 19 cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (1966), na Ibara ya 9 ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (1986).
Katika taarifa hiyo, tume imelishauri Jeshi la Polisi kutangaza mapema hatua ilizochukua kuhusu mtu aliyeonekana na silaha akimtishia Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye.
"Tume inapenda kusisitiza kwamba katika nchi yenye demokrasia, Serikali ina wajibu na jukumu la kulinda haki hizi, na pia kuwalinda wananchi dhidi ya matendo yanayodhalilisha utu wao, utesaji, na matendo yote yanayowanyima uhuru na haki zao za msingi, ikiwamo haki ya maoni na uhuru wa kujieleza," inasema taarifa hiyo.
Tume inavishauri vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi, kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio hayo na kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha Ben Saanane, ambaye ni mshauri wa mwenyekiti wa Chadema, anapatikana. Pia, jeshi hilo lihakikishe watekaji wa Salma Said na Ibrahim Mussa (Roma Mkatoliki) na wenzake wanapatikana na kuchukuliwa hatua za kisheria, inasema taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, THRDC imekemea na kulaani vitendo vya utekaji vinavyoendelea huku Serikali ikikaaa kimya.
Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa aliwaambia waandishi wa habari kuwa jambo hilo linapaswa kukemewa kwa sauti moja kwa kuwa linaweza kumkuta Mtanzania yeyote.
"Wasiwasi wetu kama watetezi ni hofu ambayo imetanda miongoni mwa wanajamii kuhusu uhuru wa maoni na usalama wa wale wanaosimama na kuikosoa Serikali katika baadhi ya mambo," alisema Olengurumwa
Olengurumwa alisema mtandao umebaini kuwa watetezi wa haki za binadamu, wanasheria, wasanii na waandishi wa habari kwa sasa hawako salama na huenda wakawa kwenye orodha ya watakaokumbana na ukatili.
Waliitaka Serikali kuwalinda watu wake kwa umakini badala ya kukaa kimya kama iliyo sasa.
Pia, mtandao huo ulisema Serikali inapaswa kuzingatia misingi ya kimataifa ya haki za binadamu kama inavyoelezwa katika mikataba ya Umoja wa Mataifa.
Mwenyekiti wa Taifa wa Watu wenye Ualbino, Nemes Temba alisema wanachama zaidi ya 130 wa mtandao huo wa THRDC, hawakuridhishwa na kitendo cha kutekwa kwa Roma Mkatoliki na kwamba maelezo yanadhihirisha wazi kuwa wananchi wameingiwa na hofu ya kuongea ukweli kwa kuogopa kutekwa au kukamatwa.
"Vitendo hivi vya kutekwa na kupotea kwa watetezi wa haki za binadamu haukuwa utamaduni wa Tanzania na cha kushangaza vimekuwa vikitokea kwa wananchi wengi na hakuna hatua zilizochukuliwa mapaka sasa," alisema Temba.     

0 comments:

Post a Comment