Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inamshikilia Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na katibu mkuu wa shirikisho hilo, Celestine Mwesigwa.
Malinzi alikamatwa na Takukuru juzi, huku habari za ndani zikidai kuwa anashikiliwa kwa matumizi mabaya ya ofisi.
Akizungumza jana jijini hapa, msemaji wa Takukuru, Musa Misalaba alisema taasisi hiyo inaichunguza TFF kwa madai mbalimbali ambayo hakutaka kuyaweka hadharani.
"Ni kweli tunaichunguza TFF, lakini sababu ya uchunguzi wetu itabaki kuwa siri hadi uchunguzi utakapokamilika. Tunawashikilia viongozi wake kwa tuhuma mbalimbali.
Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa bosi wake alijibu kwa ufupi kwamba hawezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa.
Malinzi, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka minne, amekamatwa wakati shirikisho hilo likiwa katika kinyang'ayinro cha uchaguzi na ameshajitosa kutetea nafasi yake.
Pamoja kukiri kumshikilia Malinzi na Mwesigwa, Misalaba alifichua mpango wa kuwanasa vigogo wengine zaidi, ambao wameshiriki katika makosa ambayo taasisi hiyo inayachunguza ndani ya TFF.
"Ni kweli kwamba tunaendelea na uchunguzi dhidi yao na viongozi wengine wa TFF. Uchunguzi tumekuwa nao kwa muda mrefu na bado unaendelea," alisema.
"Lakini suala la kujua tunawashikilia kwa makosa gani, nadhani bado tungoje majibu. Uchunguzi huu tunaoufanya, unaendeshwa kwa misingi ya sheria, taratibu na kanuni ambazo hazituruhusu kuweka wazi tulipofikia kwa sasa."
Taarifa kuwa wawili hao wangefikishwa mahakamani jana, zilisababisha baadhi ya wadau kufika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Badala yake, Takukuru ikaongea na waandishi wa habari katika ofisi zake za makao makuu zilizopo Upanga jijini Dar es Salaam.
Kabla ya waandishi wetu kuondoka ofisi hizo, mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Godfrey Nyange "Kaburu" naye alifika eneo hilo, ingawa haikufahamika mara moja sababu za kwenda ofisi hizo.
Kaburu, ambaye pia ni makamu wa rais wa klabu ya Simba, alifika na kuingia moja kwa moja kwenye jengo la utawala.
0 comments:
Post a Comment