Social

Saturday, June 17, 2017

Kulifungia Mawio ni kutisha wananchi, wasema wananchi Tanzania

Dar es Salaam.Wadau wa habari, wasomi na wanasiasa wamepinga uamuzi wa kulifungia kwa miaka miwili gazeti la Mawio, wakisema kitendo hicho ni kuwatisha wananchi ili wasiikosoe Serikali.
Serikali ilitangaza kulifungia gazeti la Mawio juzi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuwataja marais wawili wa zamani, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete likiwahusisha na sakata la mchanga wa madini.
Uamuzi huo ulitolewa siku moja baada ya Rais John Magufuli kutaka marais hao walioongoza serikali za awamu ya tatu na nne wasihusishwe na sheria mbovu na mikataba ya madini kwa kuwa hawakutajwa katika ripoti iliyotathmini athari za kiuchumi na kisheria za kusafirisha mchanga wa madini nje ya nchi kwa ajili ya kuyeyusha.
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema hana budi kuifungia Mawio, akitaka lisitishe kuchapisha nakala ngumu au ya mtandaoni katika kipindi cha miezi 24.
Alisema ametumia mamlaka aliyopewa na Sheria ya Huduma za Habari Namba 12 ya mwaka 2016, kifungu cha 59.
Katika barua hiyo, Dk Mwakyembe alisema licha ya utetezi wao, habari hiyo si tu imekiuka agizo la Serikali, lakini pia imekiuka kifungu 50 (a),( b),(c), (d) na (e).
Hii ni mara ya pili kwa Mawio kupata adhabu hiyo baada ya Serikali kulifutia usajili gazeti hilo Januari 15, 2016 kabla ya kushinda mahakamani.
Watu waliohojiwa na Mwananchi kuhusu uamuzi huo, walisema kukiuka haki ya wananchi kupata habari.
“Gazeti haliandiki maoni ya wahariri tu, bali hutoa nafasi ya wananchi kutoa mawazo tofauti na kwa uhuru,” alisema katibu mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga.
Alisema magazeti hayawezi kuandika habari zinazowahusu mawaziri kusaini mikataba tata na kuacha kuwahusisha marais waliokuwapo wakati ikisainiwa.
“Katika mfumo wa collective responsibility (uwajibikaji wa pamoja), rais ndiye mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri,” alisema.
“Waziri akitajwa kusaini mkataba tata wa madini, rais ambaye ndiye mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri hawezi kuacha kujadiliwa au kuhusishwa.”
Kajubi alisema katika usimamizi wa rasilimali za nchi, chombo cha habari hakiwezi kuwekewa miongozo ya kuwazuia baadhi ya watu wasijadiliwe.
“Kufungiwa kwa gazeti la Mawio kunaonyesha namna Serikali ya Awamu ya Tano inavyokosa ustahimilivu. Mazingira haya hatujayaona katika Serikali zilizopita,” alisema.
Alisema vyombo vya habari haviwezi kuandika yaliyomo kwenye tume ya kuchunguza mchanga wa madini tu bali vitafanya uchambuzi wa sekta nzima ya madini ili kuwaelimisha wananchi.
Maoni kama hayo alikuwa nayo Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (Rucu), aliyesema suala la mchanga wa madini sasa ni mjadala wa kitaifa unaohitaji mawazo tofauti kutoka kwa wananchi.
“Serikali isiogope kusikia mawazo tofauti kutoka kwa wananchi kupitia vyombo vya habari. Ikubali kuyasikia yote hata kama yana maumivu ili iweze kuboresha sekta ya madini,” alisema.
“Wananchi waachwe watoe maoni yao katika mjadala huu wa madini, kuvifungia vyombo vya habari kwa sababu ya kuwajadili marais wastaafu ni kuwatisha.”
Profesa Mpangala alisema ili kujenga sekta imara ya madini kwa sasa wananchi waachwe waeleze kasoro ili zifanyiwe kazi na Serikali.
Naye kaimu mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema kufungiwa kwa gazeti la Mawio ni kuzuiwa kwa uhuru wa kujieleza.
“Serikali isiwachagulie wananchi maoni ya kutoa kwenye vyombo vya habari. Waachwe wajadili kwa uhuru kuhusu rasilimali za nchi,” alisema.
Akiungana na wenzake, makamu mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile alisema gazeti linaweza kuwa na makosa, lakini kufungiwa na mtu mmoja haikubaliki.
Alisema ni lazima tujenge ustaarabu wa kuzitegemea mahakama kuwahukumu wenye makosa.
“Hata kama waziri atakuwa amechukizwa na habari iliyoandikwa na Mawio ni lazima tutumie ustaarabu wa kuziachia mahakama ziamue badala ya uamuzi kufanywa na mtu mmoja,” alisema.
Alisema Katiba iko wazi kuwa marais hawawezi kushtakiwa kwa makosa waliyoyafanya walipokuwa madarakani.     

0 comments:

Post a Comment